Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 04:07

Netanyahu kushauriana na Trump kuhusu tishio la Iran


Rais Donald Trump akutana na Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu. Kushoto ni mke wa Netanyahu, Sara na kulia ni mke wa Trump Melania wakiwa ikulu ya White House Machi 5, 2018 jijini Washington,DC.
Rais Donald Trump akutana na Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu. Kushoto ni mke wa Netanyahu, Sara na kulia ni mke wa Trump Melania wakiwa ikulu ya White House Machi 5, 2018 jijini Washington,DC.

Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu yuko mjini Washington kukutana na Rais Donald Trump kutafuta njia za kuzuia jeshi la Iran kuongeza himaya yake Mashariki ya Kati.

Mazungumzo hayo yamekuja wakati Trump anajaribu kupima iwapo ni busara kwa Marekani kujiondosha katika mkataba wa kimataifa uliosainiwa na Iran wenye kusudio la kuzuia nchi hiyo kutengeneza silaha za nyuklia, makubaliano ambayo Netanyahu ameyapinga kuwa hayajitoshelezi.

Lakini Trump hakufanikiwa kupata kuungwa mkono na nchi nyingine zilizosaini mkataba huo ikiwemo Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Umoja Ulaya, China na Urusi, juu ya takwa lake la kuwa mazungumzo hayo yafanyike upya.

Kabla ya kuondoka kuja Washington, Netanyahu alisema, “ Nina kusudia kuzungumzia masuala kadhaa” na Trump, “lakini muhimu kuliko yote ni Iran, ubabe wake, na utashi wake wa kuwa na nyuklia na vitendo vya uchokozi, ikiwemo maeneo ya mipaka yetu.”

Kuendelea kuwepo kwa majeshi ya Iran katika ardhi ya Syria yakimuunga mkono Rais Bashar al-Assad ndio hasa linalomtia wasiwasi Netanyahu. Ameishutumu Tehran kwa kutaka kuweka kituo cha kudumu cha kijeshi nchini Syria.

“Tunataka kujua na lazima tujue, msimamo wa Marekani ukoje iwapo tutaingia katika mapambano zaidi na Iran,” Michael Oren, Naibu Waziri wa Israeli na balozi wa zamani Marekani, amsema Jumapili kupitia televisheni ya Israeli.

Ziara ya Netanyahu huko Washington ni njia fulani ya kukimbia matatizo nyumbani, ambako anakabiliwa na mlolongo wa uchunguzi unaohusu ufisadi. Wapelelezi nchini Israeli wamemhoji Netanyahu na mkewe Sara kwa masaa kadhaa Ijumaa katika mojawapo ya mambo anayochunguzwa, na kuwa msemaji wa zamani wa Netanyahu akikubali kuwa shahidi wa upande wa serikali.

Hata hivyo Netanyahu amekanusha kutenda kosa lolote, akisema kuwa tuhuma hizo ni “habari feki,” tamko ambalo Trump mara nyingi amelitumia katika kuelezea uchunguzi wa kipindi cha miezi kadhaa juu ya tuhuma kuwa kampeni yake ilishirikiana na Urusi kumwezesha kushinda uchaguzi wa urais wa Marekani wa mwaka 2016.

XS
SM
MD
LG