Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 05:22

Harakati za Russia kuajiri mamluki kutoka Syria kupigana Libya zilishika kasi mwezi Mei


Rais wa Russia Vladimir Putin
Rais wa Russia Vladimir Putin

Hatua ya Russia kuajiri wananchi wa Syria kwenda kupigana nchini Libya kumuunga mkono Kiongozi wa wanamgambo Khalifa Haftar ilishika kasi mwezi Mei wakati mamia ya askari mamluki walioandikishwa, vyanzo vitano vya upinzani nchini Syria na chanzo cha kieneo ambao wanalifahamu suala hili wameeleza.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, mkandarasi binafsi wa kijeshi Wagner Group anaendelea kuajiri mamluki hao chini ya usimamizi wa jeshi la Russia, kwa mujibu wa vyanzo viwili vya upinzani vya ngazi ya juu nchini Syria na chanzo cha kieneo. Mwanachama wa zamani wa Wagner Group amesema kuwa mara ya kwanza ilipeleka Libya wapiganaji raia wa Syria ilikuwa mwaka 2019.

Waziri wa Ulinzi wa Russia na Wagner Group hawakujibu maswali ya Reuters.

Wakati huo huo Uturuki inasema inaendelea kutoa msaada wa kijeshi kwa upande wa pili wa mgogoro huo, Serikali ya Makubaliano ya Kitaifa (GNA) inayotambuliwa kimataifa ambayo makao yake makuu ni Tripoli.

Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan amesema mwezi Februari kuwa wapiganaji wa jeshi la taifa la Syria wanaoungwa mkono na Uturuki wako nchini Libya, na vile vile jeshi la Uturuki.

Russia imeendelea kuwa mshirika thabiti wa Rais wa Syria Bashar al-Assad, wakimsaidia kuzima uasi nchini humo. Kujihusisha kwa Moscow nchini Libya ni muendelezo wa utashi wake wa kujikita katika eneo la mashariki ya bahari ya Mediterranean, baadhi ya wataalam wanasema.

Misri na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) wameendelea kutoa msaada kwa Haftar kwa sababu wanadhani ya kuwa utawala wa GNA una mahusiano na Muslim Brotherhood, kundi la Kiislam ambalo wanalipinga vikali.

Uturuki, kwa upande mwengine, imefikia makubaliano na GNA juu ya mipaka ya baharini na inataka kulinda maslahi yake katika eneo hilo.

Inakumbusha mgogoro wa Syria

Kuhusika kwa Russia na Uturuki kwa pande zinazopingana katika mgogoro wa Libya unaakisi vita nchini Syria, ambako pia wamekuwa wakiunga mkono pande zenye kuhasimiana. Pia kuna hatari ya kuchochea zaidi mgogoro huo, wataalam wanatahadharisha.

“Russia na Uturuki wote wanaongeza nguvu zao za kijeshi na idadi ya vikosi vyao nchini Libya, ambapo nchi za Ulaya zimejikuta haziwezi kufanya lolote,” amesema Joshua Landis, mkuu wa kituo cha utafiti wa Mashariki ya Kati cha Chuo Kikuu cha Oklahoma.

“Russia inaendelea kujaribu kufikia juhudi ya Uturuki kwa kupeleka mamluki kutoka Syria, lakini matokeo ya hatua hiyo ni ya mchanganyiko.”

Idadi ya Mamluki

Wagner ina watu wanaofikia 1,200 waliopelekwa Libya, kwa mujibu wa ripoti ya siri ya Umoja wa Mataifa ambayo Reuters imeiona mwezi Mei. Serikali ya Russia imekanusha kuwa na vikosi vyake Libya.

Alipoulizwa mwezi Januari iwapo Wagner inapigana nchini Libya, Rais wa Russia Vladimir Putin alisema kama kuna raia wa Russia nchini Libya, hawako kuiwakilisha serikali ya Russia, na wala hawalipwi na serikali yake.

Marekani

Msemaji wa Jeshi la Kitaifa la Libya chini ya Haftar amekanusha kuwa iliandikisha wapiganaji kutoka Syria. Imerejea mara kadhaa kuelezea uwepo wa wapiganaji wa Syria upande wa maadui zao.

Maafisa wa Marekani walisema Mei 7 wanaamini Russia ilikuwa ikishirikiana na Assad kupeleka wapiganaji na vifaa vya kijeshi kwenda Libya.

Wizara ya habari ya serikali ya Syria haikujibu maswali yaliyotumwa kwao nji ya barua pepe.

Serikali ya GNA

Mahasimu wa Haftar, serikali ya GNA, imekuwa ikipokea ndege zisizo kuwa na rubani, mifumo ya ulinzi wa anga na washauri wa kijeshi kutoka Uturuki.

Naibu waziri wa ulinzi wa serikali ya GNA Saleh Namroush amesema hatua yao ya kuomba msaada wa kijeshi ni kutokana na kile alichokiita “ kuingilia kati kimataifa masuala ya ndani ya Libya.”

Kwa nini Uturuki?

“Uturuki ndio nchi pekee iliyokuwa tayari kutusaidia kukomesha kuenea kwa kiwango kikubwa cha mauaji ya raia na uharibifu uliofanywa na UAE, Russia na wengine,” amesema.

Taarifa za Waangalizi wa Haki za Binadamu

Kwa mujibu wa Waangalizi wa Syria wa masuala ya haki za binadamu, ambao wanaripoti mgogoro wa Syria kwa kutumia mtandao wa vyanzo mbalimbali vya habari vilivyoko nchini humo, zaidi ya raia 900 wa Syria waliandikishwa na Russia kwenda kupigana nchini Libya mwezi Mei.

Wapiganaji hao wanapewa mafunzo katika kambi ya kijeshi iliyoko mji wa Homs kabla ya kupelekwa Libya, kulingana na vyanzo vya habari ambao wameeleza kuwa malipo yao ni kati ya dola 1,000 hadi 2,000 kwa mwezi.

Harakati za wapiganaji nchini Libya zinakiuka marufuku ya silaha iliyowekwa na UN na kaimu mwakilishi wa UN kwa Libya Mei 19 alilisihi Baraza la Usalama kusitisha “mmiminiko mkubwa wa silaha, vifaa vya kijeshi na mamluki.”

Historia ya Mgogoro wa Libya

Tangu mwaka 2014, Libya imegawanyika kati ya maeneo yanayoshikiliwa na serikali ya Tripoli na eneo linaloshikiliwa na vikosi vya Haftar vilivyoko mji wa mashariki wa Benghazi.

Haftar anaungwa mkono na Russia, UAE na Misri, kwa mujibu wa wataalam wa UN na baadhi ya vyanzo vya usalama. Nchi hizo zote zinakanusha kuhusika moja kwa moja katika mgogoro wa Libya.

Pamoja na msaada huu, vikosi vinavyounga mkono GNA vilikamata ngome kuu ya mwisho ya jeshi la Haftar karibu na Tripoli Ijumaa, na kumaliza ghafla mashambulizi yake ya miezi 14 katika mji huo mkuu.

Siku ya Alhamisi, Erdogan aliahidi kuongeza msaada wa Uturuki kwa ajili ya mshirika wake nchini Libya ili kudhibiti mafanikio yaliyopatikana. Siku ya Jumamosi, Haftar alikuwa nchini Misri, ambako Rais Abdel Fattah al-Sisi alitangaza mpango mpya wa amani.

Kuondoka kwa vikosi hivyo, kumerejesha nyuma mafanikio ya Haftar aliyokuwa ameyapata mwaka 2019, na hivyo kunafanya serikali ya GNA kudhibiti sehemu kubwa ya kaskazini magharibi mwa Libya.

Hata hivyo Haftar na makundi washirika bado wanaendelea kudhibiti mashariki na eneo kubwa la kusini, na vilevile eneo kubwa lenye vinu vya mafuta nchini Libya.

XS
SM
MD
LG