Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 13:44

Wahamiaji waliokwama Libya wawasili Rwanda


Kundi la kwanza la wahamiaji wa Kiafrika waliokwama Libya, limewasili Rwanda, katika juhudi zisizo za kawaida za kuwasaidia wakimbizi na watu wanaotafuta hifadhi, walioshindwa kuingia Ulaya.

Kundi hilo la watu 66, wengi wao wakiwa akina mama na watoto, limewasili Kigali kwa kutumia usafiri wa ndege, baada ya serikali ya rais Paul Kagame kusaini mkataba na umoja wa Afrika, na shirika la umoja wa mataifa la kuwashughulikia wakimbizi UNHCR, mapema mwezi Septemba, kuwapa hifadhi wahamiaji ambao wamekwama Libya.

Serikali ya Rwanda inasema imejitayarisha kuwapokea wahamiaji 30,000 kutoka Libya inayokabiliwa na machafuko, japo mpango huo utakuwa ukiwapokea wahamiaji 500 kila baada ya mda, ili kuzuia hali ya nchi hiyo yenye watu milioni 12 kuzidiwa na mzigo wa wakimbizi.

Hata hivyo, haijabainika ni muda gani wahamiaji hao watapewa makao nchini Rwanda kabla ya kupelekwa sehemu nyingine au kurejea katika nchi zao za asili.

Katibu Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Dharura na Maswala ya Wakimbizi Olivier Kayumba, amesema kwamba wakimbizi watakaotaka kuishi nchini Rwanda muda wao wote, watapewa hifadhi, na kwamba Rwanda hailipwi kuwapokea watu hao.

Kiasi cha wahamiaji 6000 kutoka Eritrea, Ethiopia, Somalia, Sudan na mataifa mengine ya Afrika, wanazuiliwa katika vituo vinavyosimamiwa na makundi ya wapiganaji nchini Libya, yanayoshutumiwa kwa mateso na dhuluma zingine.

Baadhi ya wahamiaji hao wamekamatwa katika bahari ya Mediterania, wakiwa safarini kuelekea Ulaya.

Libya ilitumbukia katika machafuko, baada ya kuuawa kwa aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Muammar Gaddaffi mwaka 2011.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG