Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 05:47

Kauli ya Waziri Lugola Burundi ina amani yawastaajabisha wakimbizi


Waziri wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola, Tanzania
Waziri wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola, Tanzania

Baadhi ya wakimbizi wamestaajabishwa na kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania Kangi Lugola, ambayo inasema hali ni shuwari nchini Burundi ikiwa inawalazimisha kurudi Burundi.

“Ni wazi kwamba serikali ya Tanzania kwa ushirikiano na serikali ya Burundi wanataka kuturejesha nyumbani kwa nguvu. Walio wengi hatuko tayari kurejea, kwa sababu hali ya usalama bado haijaimarika,” Mmoja wa wakimbizi Renovat Nduwayo amesema.

“Tunafuatilia habari za Burundi, tunasikiliza vyombo vya habari vya ndani ya Burundi na vile vya kimataifa, ukweli ni kwamba bado kuna watu wanaendelea kuuawa, wengine wanatoweka, na wengine wanakamatwa kinyume cha sheria,” ameongeza.

Renovat Nduwayo akiongea kwa niaba ya wakimbizi wenzake amesema, iwapo serikali ya Tanzania itatekeleza tishio lake la kuwarejesha kwa nguvu wakimbizi, basi itabidi kuliomba Shirika la Umoja wa Mataifa linalowasimamia wakimbizi, UNHCR, kuwahamishia katika nchi nyingine za Afrika Mashariki kama Rwanda, Uganda na Kenya.

“Hatuna nguzu za kupingana na serikali ya Tanzania, tunaomba shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi kututetea na kututafutia hifadhi katika nchi za Afrika mashariki ambazo ziko tayari kutupa hifadhi.

Waziri Lugola alitoa matamko makali akionya mfanyakazi yeyote wa shirika lolote, liwe la kimataifa linafanya kazi kwa wakimbizi akijaribu kuwshawishi wakimbizi kwa kuwarubuni kwa kuwapotosha... kwamba Burundi haina amani atachukuliwa hatua na serikali ya Tanzania, akiongeza kama kuna wakati wa kujua nguvu ya Dkt John Pombe Magufuli ni katika suala hili.

"Baada ya kujridhisha na hali ya usalama nchini Burundi, serikali za nchi hizi mbili zimetiliana makubaliano kati yao," alisema Lugola.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola, na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Burundi, Pascal Barandagiye tayari wamesaini makubaliano yatakayo hakikisha wakimbizi wote waliopo katika Kambi ya Nduta, Wilayani Kibondo na Mtendeli iliyopo Wilayani Kakonko Mkoa wa Kigoma wanarejeshwa Burundi bila kukwamishwa na mtu au shirika lolote.

Ripoti ya UNHRC ya tarehe 31 Julai 2019, yaonyesha kuwa wakimbizi 342,867 bado wanapiga kambi Tanzania, Uganda, Rwanda na DRC, na kuwa Tanzania pekee inahifadhi wakimbizi 183,707.

Tanzania na Burundi wamesaini makubaliano ya kuwarejesha Wakimbizi 2000 kwa kila wiki nchini mwao kuanzia Oktoba 1, 2019.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG