Wakimbizi hao wanadai kwamba kuna wahalifu kutoka Burundi wanaovuruga mara kwa mara usalama kambini humo na kwenye makazi ya Watanzania yalio jirani na kambi hiyo.
Madai yao ni kuwa hilo limepelekea wakimbizi katika kambi hiyo kushutumiwa kuwa wanahusika na uhalifu huo na baadae wao wanaadhibiwa kwa kurejeshwa Burundi, bila ya hiari yao.
Wakimbizi hao wa kambi ya Nduta wanasisitiza njia pekee ya kukomesha vitendo hivyo vya uhalifu katika kambi na mjini Kibondo ni kuwahamishia kwenda kambi nyingine mbali sana na mpakani, ndio muarubaini wa kukabiliana na wahalifu wanaovuka mpaka na kujipenyeza ndani ya kambi.
Wakimbizi wa Burundi karibu laki 4 walikimbilia katika nchi jirani kufwatia mgogoro wa kisiasa uliozuka mwezi April mwaka wa 2015 baada ya hatua ya rais Pierre Nkurunziza ya kuwania muhula mwengine wa tatu. Tanzania ndiyo ilipokea idadi kubwa ya wakimbizi. Kambi ya Nduta pekee inafifadhi Zaidi ya wakimbizi laki moja.
Wakimbizi hao wanasema kuna ushahidi wakutosha kwamba watu wanaohatarisha usalama katika kambi ya nduta na kwenye makazi jirani zao wanavuka mpaka wa Tanzania, wakitokea kwenye mkoa wa Ruyigi, mashariki mwa Burundi, ambao ni jirani sana na wilaya ya Kibondo.
Wakimbizi hao wanatoa mfano wa kitendo kilichotokea mwishoni mwa juma lililopita ambapo watu wenye silaha walivuruga usalama mjini Kibondo, na katika makabiliano na jeshi la polisi la Tanzania, baadhi ya waliouwawa katika makabiliano hayo walikutwa kuwa ni raia kutoka Burundi, kama anavyosema mkimbizi huyo anayeishi katika kambi ya Nduta.
Wakimbizi wanaoishi katika kambi hiyo ambao walitaka majina yao yasitajwe, wamesema kuwa: “Baadhi ya wahalifu wanaokuja kuvuruga usalama hapa kambini na kwenye makazi ya jirani zetu wa Tanzania, wanavuka mpaka kiurahisi wakitokea Burundi."
Wameeleza mfano wa hivi karibuni ni siku ya Jumamosi ambapo genge la watu wenye silaha waliendesha shambulizi kwenye mji wa Kibondo. Miongoni mwa wahalifu waliouwawa na jeshi la polisi, kuna watu 3 na watatu hao polisi ya Tanzania ilithibitisha kwamba ni raia wa Burundi sababu moja ya waliouwawa alikutwa na kitambulisho kipya cha Burundi”.
Katika mahojiano na televisheni ya Tanzania, ITV, Jumatano, kamishna wa operesheni na mafunzo katika jeshi la polisi mkoani Kigoma Liberatus Sabas, alisema jeshi la polisi liliuwa majambazi 24 katika majibizano ya kurushiana risasi ya hivi karibuni, na kupokonya silaha 14 za majambazi hao. Afisa huyo wa polisi amesema wahalifu hao ni kutoka nchi jirani ambazo hazina utulivu wa kisiasa.
Akiongea na sauti ya Amerika, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brig General Emmanuel Maganga amejizuia kuthibisha kwamba majambazi waliouwawa na jeshi la polisi mjini kibondo ni raia wa Burundi. Anasema kilicho wazi ni kuwa waliofanya shambulizi hilo la mwishoni mwa juma si raia wa Tanzania.
Maganga amesema pia kwamba usiku wa jana kuamkia leo, kuna mfanyabiashara aishio ndani ya kambi ya nduta ambae alishambuliwa na genge la majambazi, na polisi wanaolinda usalama wa kambi waliingilia kati ili kukabiliana na majambazi hao. Ima kuhusu ombi la wakimbizi kutaka kuhamishwa mbali na mpaka wa Burundi, Emmanuel Maganga anasema jukumu hilo ni la serikali ya Tanzania.
Imetayarishwa na Mwandishi wetu Patrick Nduwimana, Washington, DC.