Katika ujumbe wake maalum kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, Rais Magufuli ameeleza kuwa kukosekana kwa utulivu katika kipindi cha karibuni katika nchi hizo mbili kumesababisha wakimbizi kukimbilia Tanzania na katika nchi nyingine za jirani, hivyo Afrika Mashariki ina nia ya dhati kuhakikisha utulivu wa kisiasa unarejea katika nchi hizo.
Wakati anakabidhi ujumbe wa rais kwa Katibu Mkuu, Waziri wa Mambo ya Nje Augustine Mahiga amesema Jumatano kuwa, Tanzania ikiwa mwenyikiti wa Afrika Mashariki, imepata matuamini na hatua iliyofikiwa katika mchakato wa kutafuta suluhu Burundi, chini ya uongozi wa Rais Yoweri Museveni wa Uganda na usimamizi wa Rais Mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa.
Taarifa iliotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje Alhamisi imesema kuwa Mahiga alimfahamisha Katibu Mkuu kuwa Mkutano wa marais wa Afrika Mashariki utaofanyika hivi karibuni unategemewa kupokea ripoti ya maendeleo juu ya mchakato huo.
Waziri Mahiga amewaambia waandishi kuwa Rais Magufuli alikutana na Guterres wakati wa Mkutano wa Marais wa Umoja wa Afrika, huko Addis Ababa, mapema mwaka huu, ambapo viongozi hao wawili walizungumzia vizuri masuala mbali mbali yanayohusu eneo la Afrika Mashariki.
“Rais amenituma nifikishe ujumbe huu kwa Katibu Mkuu Guterres, na pia amemwalika kufanya ziara ya kikazi nchini Tanzania wakati atapoona ni sawa kwake kufanya hivyo,” amesema Mahiga.
Katibu Mkuu alilakiwa na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje Mahiga kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akiwa njiani kutoka Somalia na Kenya ambako alikuwa katika ziara ya kikazi.