Rais Mkapa ambaye ni msimamizi wa mazungumzo ya kutafuta amani nchini Burundi amesema alivialika vyama vya siasa na kuwa kutofika kwa upande wa Serikali kunamaanisha “mkutano mwingine nimeuahirisha.”
“Nilikuwa na matumaini kwamba kuja kwao kungerahisisha kuwasiliana nao wakati wakiwa hapa. Lakini sasa itabidi nifanye utaratibu maalum kukutana na upande wa serikali peke yao,” amefafanua Mkapa.
Aliwaambia waandishi wa habari kuwa “mnafahamu ni vyama vya siasa ndivyo hushawishi wananchi kuishi kwa amani,” na ndio sababu nimewaalika.
“Ni matarajio yangu kwamba tutaweza kufikia muafaka katika suala la kurejesha utulivu wa kisiasa na kuanza upia mazungumzo juu ya mahusiano ya kibiashara katika maeneo ambayo Burundi imewekewa vikwazo na jumuiya ya kimataifa,” ameeleza Mkapa.
Mazungumzo haya ambayo yatafanyika kwa siku tatu ni hatua ya kuanza ya mchakato wa kuwarudisha wakimbizi nchini kwao ambao wako katika makambi. Bila shaka hatua hii itasaidia kuweka msingi wa kukubaliana wakimbizi wa kisiasa waruhusiwe kurudi Burundi.
Nafikiri hilo linawezekana na ni matumaini yangu linaweza kuharakishwa kupitia mazungumzo haya.
Serikali ya Burundi ilitoa tamko Jumatano kwamba haitapeleka ujumbe wake katika mazungumzo ya Burundi huko Arusha, Tanzania.
Hii ni awamu nyingine ya mazungumzo, Katika awamu ya kwanza mkataba wa amani ulitiwa saini mwaka 2000 na kuiwezesha Burundi kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyo dumu kwa muongo mmoja.
Wachambuzi wa kisiasa wamesema kuwa washiriki katika mazungumzo haya wataangalia kwa undani kipi kifanyike ili kumaliza mzozo wa kisiasa unaoikabili Burundi tangu Aprili mwaka wa 2015, alipotangazwa rais wa Burundi Pierre Nkurunziza kuwa atagombea urais katika awamu ya tatu.
Wajumbe zaidi ya 30 kutoka tabaka zote wamealikwa lakini hatua ya msimamizi wa mazungumzo haya ya kualika wanasiasa wanaofuatiliwa na vyombo vya sheria Burundi imeanza kulaaniwa na mashirika ya kiraia yaliokaribu na chama tawala.