Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 17:44

Wakimbizi wa Burundi nchini Tanzania waomba kurudi makwao


Maelfu ya watoto wa Burundi wakimsikiliza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipotembelea katika kambi ya wakimbizi huko Kigoma
Maelfu ya watoto wa Burundi wakimsikiliza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipotembelea katika kambi ya wakimbizi huko Kigoma

WAKATI serikali za Tanzania na Burundi zikianza utaratibu wa kuwarudisha wakimbizi wa Burundi nchini kwao zaidi ya wakimbizi 6,000 wamejiorodhesha na kuomba kurudishwa nchini mwao.

Uamuzi wa wakimbizi hao umekuja wakati utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli wa Tanzania na Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi uliofikiwa hivi karibuni ukichukua mkondo wake.

Agizo hilo linahusisha wakimbizi wanaohifadhiwa kwenye kambi mbalimbali mkoani Kigoma.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Emmanuel Maganga alitoa taarifa hizo katika kikao cha pamoja cha siku tatu cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Kigoma na Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa mitano ya Burundi kilichofanyika Mkoa wa Makamba nchini Burundi kuanzia Julai 29, mwaka huu.

Maganga alisema katika kikao hicho aliouongoza ujumbe wa mkoa wake na kilizungumzia mambo mbalimbali ya ulinzi na usalama, ikiwemo maandalizi ya kuwarudisha wakimbizi wa Burundi wanaohifadhi nchini kutokana na kujiridhisha kwamba kwa sasa hali ya ulinzi na usalama nchini Burundi ni shwari.

Alisema pia walipata nafasi ya kuzunguka mikoa mbalimbali ya Burundi ambako pamoja na taarifa zilizotolewa kwenye kikao hicho, pia wamejiridhisha kwamba kwa sasa Burundi inayo amani na hivyo wakimbizi wanaohifadhiwa nchini hawana sababu zinazowafanya kukimbia hali mbaya ya usalama iliyokuwepo awali.

Pamoja na hilo, alisema pia Agosti 31, mwaka huu kitafanyika kikao cha pamoja cha pande tatu kinachohusisha Serikali ya Tanzania, Burundi na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) kitakachozungumzia kurudishwa nchini kwao kwa wakimbizi wa Burundi wanaohifadhiwa Tanzania.

“Kwa sasa hakuna wakimbizi wanaopokewa hapa nchini hasa Mkoa wa Kigoma kutokana na kuomba hifadhi kutokana na hali mbaya ya usalama nchini mwao, tumethibitisha kwamba kigezo cha kuomba hifadhi kutokana na hali mbaya ya usalama hakipo lakini hilo la baadhi ya raia wa Burundi kuomba hifadhi nchini kwa kigezo cha hali mbaya ya uchumi (njaa) nchini mwao hatuna uhakika nalo lakini vyombo vyetu vinalifanyia kazi,” alisema Maganga.

Kwa mujibu wa gazeti la habari leo nchini Tanzania Kikao hicho mbali ya kuhudhuriwa na mkuu wa Mkoa wa Kigoma, pia kilihudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Burundi na Mwambata wa Kijeshi katika Ubalozi wa Tanzania nchini Burundi huku Burundi ikiwakilishwa na mikoa ya Makamba, Ruyigi, Rutana, Cyankuzu na Rumonge.

Vyanzo vya habari zimeelelza kuwa Mratibu wa Wakimbizi Kanda ya Magharibi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Thoony Laiser alisema wakati mkimbizi anatakiwa kurudi nchini mwake kwa mujibu wa taratibu za kimataifa, anazo haki mbalimbali atapewa ikiwemo kuanza mtaji wa kuanzia maisha ambapo kikao cha Agosti 31, mwaka huu kitazungumzia maandalizi hayo.

Laiser alisema hadi sasa wakimbizi zaidi ya 6,000 kutoka kambi ya Nyarugusu wilayani Kasulu, Nduta na Mtendeli za wilayani Kibondo wamejiorodhesha na kuomba kurudishwa nchini mwao hadi kufikia jana huku idadi ya wakimbizi wanaotaka kurudishwa nchini mwao baada ya kauli za marais hao ikizidi kuongezeka. Pamoja na hilo, Laiser alisema yapo mawasiliano baina ya idara ya wakimbizi na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Kibondo ambayo yanayoangalia namna wakimbizi hao watakavyorudi nchini mwao.

XS
SM
MD
LG