Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 07:10

Wakimbizi wadai walazimishwa kurudi Burundi


Wakimbizi wa Burundi waliokimbia vita na mvutano wa kisiasa nchini kwao wakiwa katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu magharibi ya Tanzania, Mei 28, 2015
Wakimbizi wa Burundi waliokimbia vita na mvutano wa kisiasa nchini kwao wakiwa katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu magharibi ya Tanzania, Mei 28, 2015

Serikali ya Tanzania imekana taarifa kwamba inawalazimisha wakimbizi kutoka nchini Burundi kurudi makwao licha ya kukiri kwamba jukumu la kuwahudumia wakimbizi hao limekuwa ni mzigo mkubwa.

Wakimbizi hao wanasema kwamba ujumbe wa Rais John Magufuli uliowasilishwa kwao na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania unawataka warejee makwao kwa msingi kwamba Burundi sasa ina amani na utulivu, ujumbe wanaoutafsiri kama wa kuwalazimisha kurudi makwao.

please wait

No media source currently available

0:00 0:04:28 0:00

Mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili VOA ameripoti kuwa maelfu ya wakimbizi kutoka Burundi walio nchini Tanzania, wanasema wanalazimishwa kurejea makwao, kufuatia ujumbe wa Rais John Magufuli wa Tanzania, kupitia kwa waziri wake wa mambo ya ndani, kuwataka warudi nyumbani.

Mwakilishi wa wakimbizi katika kambi ya Nduta, ambaye hakutaka jina lake litajwe ameielezea sauti ya Amerika kwamba Waziri Kange Lugola, amewahutubia wakimbizi na kuwataka warudi nyumbani kwa msingi kwamba Burundi sasa ina amani na wala hawana sababu ya kuwa na hofu ya usalama wao ndani ya nchi yao.

“Ni kweli waziri wa Tanzania wa mambo ya ndani alifanya ziara katika kambi yetu ya nduta, alifanya mkutano na waakilishi wa wakimbizi katika kambi. Aliwafahamisha kwamba amekuja na ujumbe kutoka kwa Rais wa jamuhuri ambae anauliza suali hili : Je kwanini hamrudi kwenu wakati usalama umeimarika? amesema kasi ya wakimbizi kurejea nyumbani kwa hiari imepunguka, kwa nini hamrudi nyumbani?" amedadisi.

Waakilishi wetu wamemwambia waziri : ni kweli tumekimbilia hapa, lakini kuna wakimbizi wengi wa Burundi ambao walikimbilia kwenye kambi nyingi za nchi jirani na duniani, wengine wametawanyika katika mataifa ya ulaya. Miongoni mwao kuna wanasiasa wa upinzani ambao walikua washirika wa serekali ya Burundi, lakini hawajarejea nyumbani. Siku tutasikia wanasiasa hao wa upinzani wamerejea Bujumbura, hamtolazimika kutuhimiza kurejea nyumbani, sisi wenyewe tutakuja kwenu tuwaombe gari za kutusafirisha ili turudi nyumbani.”

Lakini kupitia mahojiano na Sauti ya Amerika, Waziri wa Mambo ya Ndani amesema kwamba mwelekeo uliopo ni kuwarudisha wakimbizi wa Burundi makwao kwa hiari.

Hata hivyo Waziri Kange Lugola amefafanua: “serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kuwa imebeba mzigo wa wakimbizi wa Burundi kwa muda mrefu, na baada ya kufikia hatua ya nchi ya Burundi kutulia, na baada ya kuridhika kwamba wakimbizi walioamua kurudi makwao kwa hairi yao, sasa wanaweza kurejea.

Kwa kweli kuwa na wakimbizi ni mzigo kwa sababu kama nchi tuna lazimika kuwa na hao wakimbizi lakini ninaposema kwamba wanarudi Burundi, haimaanishi kwamba sababu ya kuwarudisha ni kuelemewa na mzigo, wanarudi kwa hiari yao”.

Lugola ameeleza kwamba tayari kuna msako wa kuwatafuta wakimbizi waliotoroka kambini kwa matayarisho ya kuwarejesha kwao.

Taarifa za wakimbizi wa Burundi kurudi makwao zinajiri mwaka mmoja baada ya rais wa Tanzania John Magufuli kukosolewa vikali na makundi ya kutetea haki za kibinadamu, baada ya kuwataka wakimbizi hao kurejea katika nchi yao.

Serikali ya Burundi imekuwa ikiwataka raia wake kurudi nyumbani, lakini juhudi zetu za kumpata katibu wa kudumu wa mambo ya ndani - Ntahiraja Rerence- hazikufaulu huku waziri wa mshikamano wa taifa Martin Nivyabandi akisita kuzungumzia swala hili.

Shirika la kuwashughulikia wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR, katika ripoti yake ya Februari 2018, inasema kwamba hali ya haki za kibinadamu nchini Burundi bado ni ya kutisha na kwamba idadi ya wakimbizi kutoka Burundi kuelekea nchi jirani, inatarajiwa kuendelea mwaka 2018 wote.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Kennes Bwire, Washington, DC

XS
SM
MD
LG