Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Novemba 05, 2024 Local time: 16:38

VOA, BBC zalaani marufuku iliyotolewa na serikali ya Burundi kwa waandishi


Mashirika ya utangazaji ya Sauti ya Amerika, VOA na BBC yamelaani hatua ya serikali ya Burundi kuzuia waandishi wao kufanya kazi ndani ya nchi hiyo.

Mapema Ijumaa Baraza la Taifa linalosimamia utangazaji habari nchini Burundi lilitangaza hatua hiyo na kufunga leseni ya BBC na kuongeza muda kuisimamisha VOA.

“Tumeshtushwa na ripoti ya kuwa waandishi wa habari wa Burundi hivi sasa wamepigwa marufuku kuwasiliana na Sauti ya Amerika (VOA) na tunaamini vitisho hivi vinavyoendelea dhidi ya waandishi wetu vinakandamiza uhuru wa vyombo vya habari nchini humo,” amesema Mkurugenzi wa VOA Amanda Bennett.

“Tunasimama pamoja na wananchi wa Burundi dhidi ya wale wanaozuia kupata habari za kweli na za uhakika na taarifa mbalimbali.”

BBC imesema katika taarifa yake '”tunaamini kwamba ni muhimu kwa watu duniani kuweza kupata habari zisizopendelea upande wowote, ikiwemo raia milioni 1.3 wa Burundi ambao hutegemea habari za BBC'' na kusisitiza kuwa inawaunga mkono waandishi wake.

Awali Burundi ilisimamisha kwa muda matangazo ya mashirika hayo mawili kuanzia Mei mwaka 2018 kwa madai ya kukiuka kanuni za uandishi kulingana na serikali ya Burundi. Wakati huo maudhui ya VOA yalikuwa yanawafikia asilimia 57 ya wasikilizaji wake kila wiki. Tafiti za kujitegemea zilikuwa zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 90 ya wasikilizaji walitoa maoni yao kuwa wanaimani na matangazo ya VOA.

Nalo shirika la Amnesty International, kanda ya Afrika Mashariki, Maziwa Makuu na Pembe ya Afrika pia limetoa tamko kulaani hatua hiyo ya serikali ya Burundi. Naibu Mkurugenzi wa Amnesty International katika eneo hilo, Sarah Jackson, amesema katika taarifa ya “kuondolewa kwa leseni ya BBC na kuendelea kusimamisha matangazo ya VOA ni juhudi zaidi za wazi za serikali ya Burundi kunyamazisha vyombo vya habari.

Hii inafuatia hatua iliyochukuliwa na baraza hilo mwaka uliopita la kufungia matangazo ya vituo hivyo kwa kipindi cha miezi sita.

Maamuzi ya leo, yamefuta leseni ya BBC kurusha matangazo yake nchini Burundi, huku VOA ikiendelea kuzuiliwa kurusha matangazo yake kwa muda usiojulikana.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa baraza hilo Nestor Banhumukunzi, BBC na VOA, hazikutimiza kanuni ya kusaini mikataba mipya ya utendaji kazi nchini humo kama inavyoelezewa na baraza hilo.

BBC inashutumiwa kwa kurusha ripoti kuhusu vitendo vya manyanyaso na ukiukwaji wa haki za kibinadamu vilivyofanywa na afisa wa idara ya upelelelezi dhidi ya wapinzani, wakati ilikuwa imesimamishwa kwa muda, suala ambalo serikali ya Burundi inasema habari hiyo ilikuwa ya uongo. Mwenyeki wa baraza hilo ameendelea kusema kwamba, BBC na VOA zilishindwa kuwajibika kwa kusaini mkataba mpya na baraza hilo, ambao unaeleza majukuma ya vyombo hivyo vya habari katika kutangaza habari nchini Burundi.

Nestor Bankumunzi amesema, VOA upande wake imeendelea kumpa kazi mwanahabari anaetafutwa na vyombo vya sheria vya Burundi, kwa hiyo matangazo yake yataendelea kufungwa hadi itakapochukuliwa hatua nyingine.

Naye mshauri wa ngazi ya juu wa Rais wa Burundi Willy Nyamitwe, amesema kuwa kila mtu anajua kile walichofanya shirika la habari la BBC kwa Makala iliyoandaliwa juu ya Burundi. “Inaonyesha uwongo mwingi. Ni uongo wa kweli kweli. Kwa kifupi ni uongo.”

“Kwa hivyo nimejibu ujumbe wa Tweet kutoka BBC, na sio ukweli kwamba BBC kama inavyodai imefanya uchunguzi Burundi katika Makala hayo lakini ni uongo, siyo uchunguzi,” amesema.

Nyamitwe amedai kuwa watu ambao nchi za magharibi zinawaita wakimbizi wa kisiasa ni watu waliokuwa wanajaribu kufanya mapinduzi.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG