Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 18:18

Kufungwa NGOs kwaathiri kurejea wakimbizi Burundi


Wakimbizi wa Burundi nchini DRC.
Wakimbizi wa Burundi nchini DRC.

Wakimbizi wa Burundi zaidi ya 300 waliokuwa wamerejea nyumbani kwa hiari yao kutoka Tanzania jumapili, wamelazimika tena kurudi kambini walikotoka baada ya kukosa huduma za mapokezi kutoka kwa shirika moja la hisani.

Hii inafuatia hatua ya serikali ya Burundi ya kusimamisha kazi kwa muda mashirika ya kimataifa yasiyo kuwa ya kiserikali.

Wakimbizi 320 wa Burundi kutoka kambi ya mtendeli katika mkoa wa Kigoma Jumapili walifunga mizigo yao na kuingia katika mabasi na lori wakielekea nyumbani.

Walipofika eneo la mpakani siku ya Jumatatu, waliambiwa kwamba wafanyakazi wa shirika la kimataifa liitwalo International Rescue Committee (IRC) inayo shughulikia usafiri wa wakimbizi ambao wange wasaidia usafiri hadi kwenye mikoa walikotoka, hawakuweza kufika mpakani kwa sababu shughuli za shirika hilo zilisimamishwa.

Wakimbizi warejeshwa Tanzania

Mwandishi wa Sauti ya Amerika katika eneo la mashariki mwa Burundi ambaye alifuatilia habari hiyo, amesema wakimbizi hao walirejea tena nchini Tanzania, kwa huzuni, sababu wengi walikuwa wameuza mali zao kwa matumaini ya kuanza maisha mapya nchini mwao.

Taarifa zaidi zinasema sio tu wakimbizi wa Burundi ambao wameanza kuguswa na hatari ya kusimamishwa kazi mashirika ya kihisani ya kimataifa.

Wakimbizi kutoka Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanaopiga kambi katika mikoa ya Ruyigi na Cankuzo, mashariki mwa Burundi wamejawa na wasiwasi mkubwa baada ya shirika hilo la IRC ambalo lilikuwa linawahudumia kuwapa taarifa kwamba limewasimamisha kazi wafanyakazi wake wote.

Mashirika yasiyo ya kiserikali

Pia shirika ka Kitaliano liitwalo GVC ambalo lilikuwa linawapa huduma za afya nalo lilisitisha shughuli zake tangu Jumatatu tarehe mosi oktoba. Wakimbizi kutoka DRC wapatao elfu 22 ndio walikua wanahudumiwa na mashirika ya IRC na GVC.

Katika tarafa ya Bugabira inayopatikana katika mkoa wa kaskazini wa Kirundo, kituo cha afya kilichokuwa kinatowa huduma kwa raia wenye hali duni ya maisha kinasema hakitoweza tena kuwahudumia raia hao kama ilivyokuwa awali.

Kituo hicho kilikuwa kinapata msaada wa fedha na vifaa kutoka shirika moja la Ubelgiji liitwalo Enabel. Kituo hicho kilikuwa pia kinapata msaada kutoka kwa shirika la Uingereza Concern World Wide ambalo lilikuwa linakisaidia kupambana dhidi ya utapiamlo.

Katika mkoa jirani wa Muyinga, raia wa mkoa huo waliokuwa wanasaidiwa na mashirika ya hisani kama Catholic Relief service na Care International wameanza kulalamika. Mashirika hayo yalikua yanawasaidia kwa kuwalipia bima ya afya.

Serikali ya Burundi

Serikali ya Burundi iliyasimamisha kwa kipindi cha miezi mitatu tangu oktoba mosi mashirika ya kimataifa 130 kwa madai kuwa hayaheshimu sheria ya Burundi inayohusu mashirika ya kimataifa ya kihisani.

Katika mkutano na wawakilishi wa mashirika hayo jana jumanne, waziri wa mambo ya ndani Pascal Barandangiye aliwaelezea masharti manne muhimu ambayo ni lazima mashirika hayo yaweze kutekeleza ili yaruhusiwe kufanya kazi.

Mmoja ya masharti hayo ni kwamba mashirika hayo yanatakiwa kuhakikisha usawa kati ya makabila muhimu ya Burundi unaheshimiwa wakati wa kuajiri wafanyakazi, na kuweka pesa zao zote za kigeni za matumzi kwenye Benki Kuu ya taifa, hivo zibadilishwe katika sarafu ya Burundi kwa kiwango cha benki kuu ya taifa.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Patrick Nduwimana, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG