Tamko la serikali
Katika taarifa aliyo itowa Alhamisi Katibu Mkuu wa Baraza la Usalama la kitaifa, Jenerali Silas Ntingurigwa, mashirika hayo yamesitishwa kutoa huduma kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia tarehe mosi Oktoba.
Lakini hakutoa idadi au utambulisho wa mashirika yanayo kabiliwa na hatua hiyo. Nchini Burundi, kuna mashirika yasio kuwa ya kiserikali yapatao 130.
Sababu yakusimamishwa mashirika hayo
Katika mkutano na waandishi wa habari Ijumaa, msemaji wa Rais Pierre Nkurunziza amesema hatua ya kuyasimamisha baadhi ya mashirika yasio kuwa ya kiserikali ya kimataifa imechukuliwa kwa sababu mashirika hayo yanaingiza nchini tabia ambazo ni kinyume na mila ya Burundi kama ushoga, mengine yanachochea vita.
Tuhuma za ushoga
“Tumegunduwa kwamba baadhi ya mashirika hayo yanaunga mkono harusi kati ya watu wa jinsia moja, hata watu wa jinsia moja kutenda ngono,” amesema Jean Claude Karerwa, msemaji wa Rais wa Burundi.
“Mashirika mengine yanachochea vurugu ili makampuni yanayo tengeneza silaha yaweze kupata soko. Hatuwezi kamwe kukubali jambo hili,” amesisitiza Karerwa.