Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 04:06

Rais wa Uturuki azuru Tunisia kuimarisha ushirikiano, ajadili mzozo wa Libya


Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan akutana na Rais wa Tunisia Kais Saied mjini Tunis, Tunisia, Disemba 25, 2019. Picha kwa Hisani ya Murat Cetinmuhurdar/Turkish Presidential Press Office/Handout via REUTERS
Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan akutana na Rais wa Tunisia Kais Saied mjini Tunis, Tunisia, Disemba 25, 2019. Picha kwa Hisani ya Murat Cetinmuhurdar/Turkish Presidential Press Office/Handout via REUTERS

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amekutana na kiongozi mwenzake wa Tunisia, Kais Saied kujadili namna ya kuimrisha ushirikiano kati ya nchi zao na mzozo ulioko katika nchi jirani ya Libya.

Rais Erdoga alifanya ziara hiyo ambayo haikutazamiwa ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kuimarisha uhusiano na nchi zinazopakana na bahari ya Mediterranean, ambako Ankara imekuwa na ugomvi na Ugiriki juu ya rasilmali nje ya pwani ya kisiwa cha Cyprus.

Rais amefanya ziara hiyo ya kushitukiza katika juhudi za kutafuta njia za kusitisha mapigano nchini Libya ambayo anasema yanasababisha matatizo makubwa kwa kanda nzima.

Jeshi la Jenerali Haftar

Nchini Libya tangu mwezi April 2019, jeshi la taifa la Libya, LNA, lililoundwa na Jenerali aliyeasi Khalifa Haftar linashikilia sehemu ya mashariki ya nchi.Jeshi hilo limekuwa likijaribu kuchukua udhibiti wa mji mkuu wa Tripoli.

Lakini hadi sasa juhudi hizo zimekwama pamoja na kuungwa mkono na Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Rashia.

Hata hivyo serikali inayotambuliwa kimataifa ya Tripoli, GNA, ina ungwa mkono na Umoja wa Mataifa na kupata msaada kutoka Uturuki na Qatar.

Rais Erdogan azuru Tunis

Hivyo katika ziara yake ya Tunis hapo Jumatano, Rais Tayyip Erdogan aliwaambia waandishi habari kwamba alikuwa na mazungumzo juu ya ushirikiano kati ya nchi zao

Rais Erdogan alisema : “Tulipata nafasi ya kujadili juu ya njia za kushirikiana kuweza kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano nchini Libya kwa haraka iwezekanavyona kuanza tena utaratibu wa kisiasa.”

Kwa upande wake Rais mpya wa Tunisia Qais Saied aliyechukuwa madaraka baada ya ushindi mkubwa mwezi Oktoba, amempokea Rais Erdogan akiwa ni kiongozi wa kwanza kutembelea Tunisia tangu kiongozi huyo kuchukuwa madaraka.

Bunge la Uturuki

Bunge la Uturuki liliidhinisha siku ya Jumamosi mkataba wa ushirikiano wa usalam na kijeshi uliotiwa saini na serikali ya Tripoli na ile ya GNA mwezi uliyopita.

Erdogan ameapa kuongeza msaada wa kijeshi kwa GNA katika mapambano yake na kiongozi wa eneo la mashariki ya nchi, Haftar yanayoendelea kwa miezi kadhaa, ambaye anajaribu kuchukua udhibiti wa mji mkuu waTripoli.

Rais Recep Erdogan amesema : “Athari za maendeleo mabaya huko Libya hazibaki ndani ya nchi hiyo pekee yake bali inadhuru pia nchi jirani na Tunisia inakua ya kwanza, kwani ikio katika mstari wa mbele. Ni lazima pawepo na usitishaji mapigano Libya kwa haraka iwezekanavyo.”

Libya ina mpaka mrefu na Tunisia na maelfu ya Walibya wamevuka mpaka na kuomba hifadhi tangu uasi wa 2011 uliosaidiwa Umoja wa majeshi ya kujihami ya Ulaya ( NATO) na kusababisha kupinduliwa kwa kiongozi wa muda mrefu Muammar Ghadafi.

Serikali ya Moscow yakanusha

Serikali ya Moscow mwezi uliyopita imekanusha ripoti ya gazeti la Marekani la New York Times kwamba imewapeleka mamluki kuungana na Haftar katika vita vyao, na Umoja wa Mataifa umemtuhumu kiongozi huyo mwenye ushawishi mkubwa kwa kuwaandikisha wapiganaji kutoka Sudan.

Aidha Rais Erdogan amesema hafahamu watu hao wanafanya nini nchini Libya.

Rais Erdogan ameeleza kuwa iwapo Uturuki itaalikwa kupeleka wanajeshi tutakubalikwa sababu angalau tuna mkataba wa kijeshi na GNA.

Uturuki imekosolewa na Jumuia ya Kimataifa kwa mkataba huo na GNA na mkataba tofauti wa mipaka ya bahari iliyotiwa saini mwezi Novemba 2019.

Nayo Ugiriki imekasirishwa na mkataba huo ikieleza ina kiuka sheria za kimataifa, lakini Ankara inadai inalengo la kulinda haki zake katika kanda hiyo na inaambatana kabisa na sheria za safari za baharini.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Abdushakur Aboud, Washington, DC

XS
SM
MD
LG