Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 07:19

Mgogoro wa Libya : Jenerali Haftar akaidi wito wa UN kusitisha vita


Mapambano kati ya majeshi ya serikali inayotambuliwa kimataifa na majeshi ya Jenerali Haftar yakiendelea katika eneo la Ain Zara, Tripoli, Libya, Mei 5, 2019.
Mapambano kati ya majeshi ya serikali inayotambuliwa kimataifa na majeshi ya Jenerali Haftar yakiendelea katika eneo la Ain Zara, Tripoli, Libya, Mei 5, 2019.

Kamanda wa majeshi ya kusini mwa Libya Khalifa Haftar, amewahimiza wanajeshi wake kuendelea kupigana na wanajeshi wa serikali, ili kuudhibiti mji wa Tripoli na kuwapa funzo maadui zao.

Kamanda huyo amekaidi wito wa Umoja wa Mataifa (UN) uliokuwa unataka pande zote mbili kusitisha mapigano na kusema mwezi mtukufu wa Ramadhan ulioanza Jumatatu nchini Libya, ni mwezi wa vita vitakatifu.

Matamshi yake yanajiri masaa machache baada ya Umoja wa Mataifa (UN) kutoa wito wa kusitisha vita kwa muda wa wiki moja ili kuruhusu msaada wa kibinadamu kuwafikia zaidi ya watu 50,000 ambao wamekoseshwa makao kufuatia vita hivyo.

Wanajeshi wa Haftar – Libyan national Army LNA, ambao wameunda serikali yao wameshindwa kuiangusha serikali ya Tripoli inayotambuliwa kimataifa.

Haftar amesema Ramadhan haijawahi kuwa sababu ya kusitisha mapigano ya awali, yaliyomsaidia kuteka miji ya mashariki ya Benghazi na Derna, alipokuwa anapanua utawala wake na nchi kuingia katika machafuko baada ya kuangushwa kwa utawala wa Muammar Gaddafi, mwaka 2011.

Haftar, ambaye alikuwa Jenerali wa Muammar Gaddafi, anashikilia sehemu za kusini mwa Libya zenye idadi ndogo ya watu lakini yenye utajiri mkubwa wa mafuta, na sasa anajaribu kuteka mji mkuu wa Tripoli.

Mapigano mapya yanatishia juhudi za uchimbaji mafuta, kuongeza idadi ya wahamiaji kuelekea ulaya na kutatiza mipango ya UN ya kuandaa uchaguzi mkuu utakaomaliza uhasama kati ya serikali mbili za mashariki na magharibi.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG