Wawili hao wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mwenyekiti Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko wataendelea kushikiliwa rumande baada ya dhamana zao kufutwa.
Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwamo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari mosi na 16, mwaka 2018 maeneo ya Dar es Salaam.
Baada ya kesi hiyo kuahirishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam Ijumaa, viongozi hao waliwatakia wanachama wao heri ya Krismasi na mwaka mpya.
Katika kesi hiyo, Wakili wa Serikali, Wankyo Simon, alidai mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, kuwa kesi imekuja kwa ajili ya kutajwa na kuiomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine kwa madai kuwa hawana taarifa ya kinachoendelea mahakama ya juu.
Hata hivyo, Wakili wa utetezi wa kesi hiyo, Faraja Mangula, alidai kuwa mawakili, Peter Kibatala na Sheck Mfinanga, wamepata dharura na kushindwa kufika mahakamani hapo na waliomba mahakama hiyo kuahirisha kesi hiyo hadi Januari 4, mwakani.
Akijibu hoja hiyo, Wakili Wankyo, alidai suala la kupanga tarehe wanaiachia mahakama hiyo kwa watakavyoona inafaa.
Hakimu Mashauri alisema Januari 4, mwakani atakuwa na kazi nyingine hivyo aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 3, mwakani.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Katibu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji, Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya na Katibu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu.