Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Novemba 05, 2024 Local time: 15:33

Chadema yasusia uchaguzi mdogo Tanzania


Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Semistocles Kaijage
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Semistocles Kaijage

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nchini Tanzania, Jumatano kimetangaza kususia uchaguzi wote mdogo wa Ubunge na udiwani unaotarajiwa kutangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe amesema kuwa kumekuwepo na ukiukwaji mkubwa wa sheria za uchaguzi katika chaguzi ndogo zilizo itishwa hivi karibuni katika majimbo ya Ukonga na Monduli, jambo ambalo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imelipinga.

"Hatuwezi kushiriki katika uchaguzi ulioitishwa Liwale na kata 37 nchi nzima kwani tumeona ni kwenda kuhalalisha uvunjaji wa sheria, unaofanywa na serikali," amesema Mbowe.

Mbowe ameeleza kuwa Tume ya uchaguzi imekuwa ni sehemu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwanza ina makada wa CCM ambao wanapokea mamlaka na amri kutoka serikali ya CCM, na hivyo uhuru wa Tume kusimamia uchaguzi ambao ni huru na haki kwa kweli umepotea.

Amesema kuwa katika hatua ya kuwatishia wananchi jeshi la polisi nchini limetenga kikosi kizima kwa ajili ya operesheni hiyo.

"Huu ni ubatili mkubwa na ukatili dhidi ya demokrasia, na matokeo yake asilimia 10 -15 tu ndiyo wanajitokeza kupiga kura," Mwenyekiti huyo amefafanua.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi

Hata hivyo Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Semistocles Kaijage alikiri kuwa wapiga kura hawakuonyesha kushawishika kujitokeza kupiga kura katika majimbo ya Ukonga na Monduli na kuahidi kufanya mabadiliko makubwa kabla ya uchaguzi wa mwaka 2020.

Mwenyekiti huyo alitoa kauli ya kuwa uchaguzi huo wa marudio ulikuwa umefanyika kwa mujibu wa sheria.

Ametupilia mbali ripoti za madai ya mawakala wa Chadema katika majimbo ya Ukonga na Monduli zinazodai kuwa walizuiliwa kuingia katika vituo vya kupiga kura na kusema umma uyapuuze madai yao.

“Ni wakala wanne tu walio kuwa wamezuiliwa kuingia katika vituo vya kupiga kura jimbo la Ukonga kwa sababu halisi, ikiwemo kutokuwa na barua za kuwatambulisha na shahada za viapo. Baadhi ya mawakala walikuja kuwawakilisha wenzao, jambo ambalo ni kinyume cha sheria,” amesema.

XS
SM
MD
LG