Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 15:35

Chadema yadai uonevu katika uchaguzi mdogo


Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Semistocles Kaijage
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Semistocles Kaijage

Chama cha upinzani cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nchini Tanzania, kimepinga matokeo ya uchaguzi mdogo katika jimbo la Monduli kwa madai ya kuwa uchaguzi huo ulitawaliwa na uvunjifu wa sheria.

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa mgombea wa uchaguzi huo kupitia tiketi ya Chadema, Yonas Laizer, alieleza masikitiko yake muda mchache baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa, Jumapili.

Tanzania, kwa mara nyengine tena imefanya uchaguzi wa marudio unaotokana na wabunge wa upinzani kuhama vyama vyao na kugombea kupitia chama tawala, CCM.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi

Hata hivyo Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Semistocles Kaijage amekiri kuwa wapiga kura hawakuonyesha kushawishika kujitokeza kupiga kura katika majimbo ya Ukonga na Monduli na kuahidi kufanya mabadiliko makubwa kabla ya uchaguzi wa mwaka 2020.

Lakini Mwenyekiti huyo alitoa kauli ya kuwa uchaguzi huo wa marudio ulikuwa sawa. Ametupilia mbali ripoti za madai ya mawakala wa Chadema katika majimbo ya Ukonga na Monduli zinazodai kuwa walizuiliwa kuingia katika vituo vya kupiga kura na kusema umma uyapuuze madai yao.

“Ni wakala wanne tu walio kuwa wamezuiliwa kuingia katika vituo vya kupiga kura jimbo la Ukonga kwa sababu halisi, ikiwemo kutokuwa na barua za kuwatambulisha na shahada za viapo. Baadhi ya mawakala walikuja kuwawakilisha wenzao, jambo ambalo ni kinyume cha sheria,” amesema.

Chadema yakataa matokeo ya uchaguzi mdogo

Kufuatia uchaguzi huo, kwa mara nyengine tena, Chadema imekataa matokeo ya uchaguzi mdogo katika jimbo la Monduli kikidai kuwa uchaguzi huo ni haramu kwa kuwa ulitawaliwa na uvunjaji wa sheria kanuni za tume ya uchaguzi na hujuma kwa chama hicho.

Kwa mujibu wa Matokeo ya uchaguzi mgombea wa CCM, Julius Kalanga, alishinda uchaguzi huo kwa kupata asilimia 95 ya kura zote zilizopigwa na Chadema kuambualia asilimia 5 tu.

Hujuma za uchaguzi

Lakini Laizer anadai kuwa uchaguzi huo ulihujumiwa kwa vitendo vya baadhi ya mawaziri wa serikali walioshiriki katika kampeni za uchaguzi huo na kuahidi kuwa endapo CCM itashinda, serikali ingeliwapelekea maendeleo na kutatua kero zinazo wakabili wananchi.

Mgombea huyo amesema kuwa anakusanya ushahidi wa matukio yote ya uvunjifu wa kanuni na taratibu zilizovunjwa na wapinzani wao ili kuweza kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kulifikisha suala hilo mahakamani.

Mwenyekiti wa Chadema- vijana

Naye mwenyekiti wa baraza la vijana la taifa la Chadema, Patrick Ole Sosopi, ameunga mkono madai hayo na kueleza kuwa mawakala wa chama chake walitekwa na wengine kupigwa huku gari la mbunge wa chama hicho likishambuliwa na watu wasiojulikana wakati wakisambaza mawakala kwenye vituo.

Chama tawala cha CCM

Hata hivyo, chama tawala CCM kupitia meneja wa mgombea wake na aliye tangazwa mshindi, Wiliam Nasha, kimetupilia mbali madai ya Chadema na kusema kuwa ushindi wao umetokana na wananchi kukikubali chama hicho.

Jeshi la polisi

Kwa upande wake Jeshi la polisi limesema kuwa uchaguzi huo umefanyika kwa amani na kutupilia mbali madai ya mawakala wa Chadema kutekwa kwa kuwa hakuna matukio zaidi yaliyo ripotiwa polisi.

Tukio pekee ni la mbunge wa viti maalum wa Chadema ambaye gari lake lilishambuliwa na magurudumu yote manne kutobolewa na watu wasio julikana.

XS
SM
MD
LG