“Jana tulikuwa tumepata hisabu ya kuwa watu 15,000 bado wanahitaji kuokolewa Alhamisi – watu hao 15,000 wako katika hali mbaya. Bado wako hai, tunawasiliana nao, tunawapelekea chakula, lakini inatulazimu kuwaokoa na kuwaondoa katika maeneo hayo ya mafuriko,” aliwaambia waandishi wa habari.
Hadi Allhamisi asubuhi vifo 200 vimethibitishwa kutokea Msumbiji, zaidi ya 100 Zimbabwe na karibu 60 nchini Malawi. Mamia wamejeruhiwa na wengine wengi hawajulikani waliko. Zaidi ya watu milioni mbili na nusu wameathirika kutokana na upepo mkali na mvua zilizoletwa na kimbunga Idai katika eneo la Kusini mwa Afrika.
Marekani yajiandaa kuanza shughuli za uokozi
Idara ya maendeleo ya kimataifa ya Marekani, USAID, imetangaza Alhamisi inasubiri kibali kutoka serikalini kuzindua mpango wa kupeleka timu ya kutoa misaada ya dharura ambapo itatumia ndege za kijeshi katika operesheni hiyo kufuatia janga la mafuriko yaliotokana na kimbunga Idai.
Tayari kuna ndege ya kijeshi ya Marekani Jijini Maputo ikisubiri amri ya Washington kuanza kusaidia kutoa huduma za dharura katika maeneo ambayo watu wamekwama kutokana na mafuriko hayo, ameleza afisa muandamizi wa USAID.
UN yatoa dola milioni 20
Nayo idara ya huduma za dharura ya Umoja wa Mataifa imetangaza Jumatano kwamba imetenga dola za Marekani milioni 20 kutoka mfuko wa kukabiliana na dharura CERF ili kuhakikisha msaada unawasili katika maeneo yaliyoathirika zaidi.
Kwa upande wake Uingereza imetangaza msaada wa dola milioni 6 , huku Tanzania ikiwa imepeleka tani 238 za chakula na dawa kwa nchi tatu zilizoathirwa za Msumbiji, Malawi na Zimbabwe.
Shirika la Msalaba Mwekundu
Shirika la Msalaba Mwekundu linasema wasiwasi uliyopo hivi sasa ni njia gani itumike kuwaondoa aelfu ya watu amabo wako katika vijiji vya mbali na hofu ni huenda mvua hizo zikaendelea na pia uwezekano wa kuzuka kwa magonjwa ya kuambukiza yanayotokana na maji yasiyo salama.
Shirika hilo imeeleza Jumatano kwamba watu 910 waliokolewa huko Beira, 210 kwa helikopta tano na wengine 700 kwa boti.
Msumbiji yaanza kampeni maalum
Wakati huohuo kazi za kusafisha, kuondoa vifusi na kutathmini uharibifu uliotokana na kimbunga cha hatari cha Idai zimeanza Msumbiji, huku shughuli za uokozi zikiendelea, na tayari juhudi hizo zimeweza kugundua miili zaidi wakati walipowasili maeneo ambayo hayakuweza kufikiwa wakati mafuriko yanatokea.
Wakati operesheni hiyo ikiendelea, misaada zaidi kutoka mataifa mbali mbali imeanza kuwasili Msumbiji na Zimbabwe ambapo watu wapatao miloni 1.7 wameathirika.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa wakazi wa mji wa bandari ya Beira kati kati ya Msumbiji wameanza kazi ya usafishaji na kurudi nyumbani kutathmini uharibifu ulosababishwa na kimbunga Idai kilichopiga kwanza katika mji huo siku ya Alhamisi na kusababisha vifo vya mia ya watu.
Asilimia 90 ya miundombinu imeharibika
Asilimia 90 ya miundo mbinu ya mji huo imeharibika hakuna maji wala umeme na Matilde Cunhaque, mtaalamu wa afya katika chuo kikuu cha John Hopkins ametembelea mji huo na kueleza kwamba hali ni mbaya sana.
Matilde Cunhaque anasema :Hatuna nishati, asili mia 99 ya nguzo za umeme zimeanguka hakuna umeme. Kituo cha mtambo wa umeme kimepoteza paa lake lote na hata makao makuu ya shirioka la umeme limeharibika. Kila kitu kimeharibika hospitali zinakabiliwa na hali ngumu , hakuna mawasiliano wala maji ya kunywa.
Kufikia Jumatano watu 300 wametangazwa rasmi wamefariki Msumbiji, wakati wafanyakazi wa uokozi wakisema wanashindwa kuwafikia wale waliokwama juu ya paa za nyumba.
Rais wa Zimbabwe
Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe alitembelea wilaya ya Chimanimani kilichoathirika zaidi na mafuriko na kusema amekwenda kutathmini binafsi hasara iliyopitikana na kiwango cha msaada unaohitajika.
Emmerson Mnangwagwa ameeleza : “Mataifa kama Afrika Kusini, Botswana, Namibia, na Angola zimeeleza kwamba zinataka kujua mahitaji yetu na tunajishughulisha kukusanya bidhaa tunazodhani ni muhimu zinazohitajikaili tuweza kuwasaidia wamnaoathirika.”
Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji aliyetembelea kwa helikopta mji wa Beira siku ya Jumatatu amesema ana hofia idadi ya waliofariki huenda ikafikia elfu moja na kutangaza hali ya dharura katika maeneo yaliyoathirika.
Changamoto za uokozi
Msemaji wa shirika la kimataifa la msalaba mwekundu Caroline Haga ameliambia shirika la habari la AFP kwamba wafanyakazi wa uokozi wanakabiliwa na changamoto kubwa kuwafikia wanaohitaji msaada na wana wasiwasi na huzuni, kwani siku ya Jumanne walifanikiwa kuwaokoa watu 167 na kwamba muda unakimbia haraka sana na watu bado wamekwama na wako hatarini.
Papa Francis aeleza masikitiko yake
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis alieleza masikitiko yake na kutoa rambirambi zake kwa walioathiriwa na maafa hayo.
Papa ameeleza : “Mnamo siku chache zilizopita mafuriko makubwa yamesababisha maafa na uharibifu katika maeneo mbali mbali ya Msumbiji, Zimbabwe na Malawi. Ninaeleza machungu yangu na kuwaombea waathiriwa na familia zao Mwenyezimungu awabariki na nina watakia afweni wanaokumbwa na janga hilo.”
Hata hivyo Umoja wa Mataifa umeeleza kuwa msaada wa dharura umeshaanza kuwasili katika baadhi ya maeneo huku wananchi wakilia hawana kitu cha kula kwa muda wa siku 6 baada ya kimbunga kupiga eneo hilo.
Mkazi wa Beira
Julia Luis, mkazi wa Beira, amesema kuwa : “Hatuna kitu chochote kilichobaki, hatuna chakula, hatuna kitu ni tatizo kubwa. Usiku hatupati chakula, hatuna blanketi la kujifunika, tunataabika sana hadi hii leo.”
Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Abdushakur Aboud, Washington, DC.