Wizara inayohusika na kupambana na majanga imesema inaendelea kuwaasa raia wanaoendelea kuishi kwenye maeneo hatarishi kuhama.
Lakini Mamlaka ya hali ya hewa imelaumiwa kushindwa kutoa taarifa muhimu kuhusu hali inavyoendelea kubadilika.
Ripoti kuhusu maafa yanayotokana na mafuriko ya mvua zimekuwa zikitolewa miaka ya hivi karibuni na mara nyingi serikali imekuwa ikiahidi kuchukua hatua za kukabiliana na tatizo hilo. Lakini mpaka sasa hatua hizo hazijaweza kulipatia tatizo hilo suluhu ya kudumu.
Kumekuwa na vilio vya hapa na pale kutoka kwa wananchi wakiomba msaada kwa serikali.
Baadhi ya raia wamesema kuwa mvua imesababishia matatizo makubwa na kuharibu mashamba yao.
Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili anaripoti kuwa mashamba hayo yamefunikwa na udongo, na mazao kama vile miwa, nyanya, viazi na takriban kila kitu kilichokuwa shambani kimetoweka.
Kadhalika raia hao wamesema kuwa nyumba zao zimeanguka. Pia kutokana na maafa hayo wanaiomba serikali iwapatie chakula.
Lakini baadhi ya wananchi wamelaumu kuwa janga la mafuriko linalosababisha maafa na hasara kwa wananchi kwa kiasi kikubwa limekuwa likichangiwa na ukosefu wa sera bora ya mpango mji, hali inayosababisha kila mvua ikinyesha maji kuwasomba watu na mali zao.
Baadhi ya wananchi wamesema kuwa hata mifereji iliyoelekezwa katika maeneo yao, ielekezwe maeneo mengine kwa maana ndiyo inayosababisha matatizo au "basi watuwezeshe kuhamia maeneo mengine yaliyo salama."
Hata hivyo wizara inayohusiana na masuala ya kupambana na majanga imekuwa ikijitahidi kutoa misaada kwa wananchi walioathirika lakini bila kupata muafaka wa matatizo hayo.
Hii ni kwa sababu kila mwaka zinaponyesha mvua za aina hii, watu wengi hupoteza maisha huku tatizo hili pia likichangiwa na radi zinazopiga wananchi kwa wingi.
Mwezi uliopita watu 16 walifariki dunia kwa mpigo baada ya kupigwa na radi walipokuwa kanisani jimbo la magharibi mwa nchi.
Lakini wizara inayopambana na majanga inasema licha ya kutoa misaada bado wananchi wana jukumu la kuwa na tahadhari na kinga.
Phillipe Habinshuti ambaye ni mfanyakazi wa wizara hiyo anasema kuwa wizara itaendelea kuwasaidia kama ambavyo tunafanya lakini tunaendelea kusema kuwa ni vema kila mwananchi akawa na tahadhari, tunakiri kuwa wakati mwingine zinanyesha mvua zenye nguvu kupita kiasi kutokana na maumbile ya nchi yetu.
Lakini tunasema hata kama zikinyesha mvua za aina hiyo angalau zikute kuna mikakati iliyochukuliwa ili kupunguza athari kama ambavyo tunashuhudia.
Serikali inasema licha ya vifo hivyo 41 wengine 162 walijeruhiwa na mvua hizo, huku makazi elfu tatu na thelathini na mbili yamesombwa na maji sambamba na ekari 1751 zilizoharibiwa kabisa na mvua hizo.
Kwa upande mwingine mamlaka ya hali ya hewa imekuwa ikilaumiwa na wananchi kama isiyotoa taariha sahihi kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa na hivyo kuchangia tatizo hilo.