Sithu Aung Myint, mwandishi wa makala katika tovuti ya Frontier Myanmar na mwandishi wa radio ya Sauti ya Amerika, na Htet Htet Khine, mzalishaji vipindi wa kujitegemea wa kituo cha BBC Media Action, walikamatwa Agosti 15, Myawaddy TV imeripoti.
Sithu Aung Myint alifunguliwa mashtaka ya uchochezi na kusambaza habari za uongo ambapo Myawaddy alikuwa mkosoaji mkuu wa uongozi wa kijeshi na iliwasihi watu kuitisha migomo na kusaidia vikundi ya upinzani vilivyopigwa marufuku.
Htet Htet Khine alituhumiwa kumpa hifadhi Sithu Aung Myint, mshukiwa mhalifu, na kufanya kazi na kuiunga mkono serikali kivuli ya Umoja wa Kitaifa.
BBC Media Action imesema katika taarifa yake ina wasiwasi juu ya usalama wa Htet Htet Khine na mashtaka yaliyofunguliwa dhidi yake na wanafuatilia kwa karibu hali ya huko.
Chama cha Waandishi Wasio na Mipaka (RSF) kimesema wawili hao wanashikiliwa na hawana mawasiliano na yeyote.
“Tunalaani vikali hali ya kiholela ya kushikiliwa kwao, ambayo inaonyesha ukatili ambao utawala wa kijeshi unawafanyia waandishi wa habari,” amesema mkuu wa kitengo cha Asia Pacific Daniel Bastard.
Myanmar bado ina ukosefu mkubwa wa uthabiti na upinzani unaongezeka kwa utawala wa kijeshi, huku zaidi ya watu 1,000 wameuawa, kwa mujibu wa kikundi cha wanaharakati kinachofuatilia mauaji yanayofanywa na vikosi vya usalama.
Jeshi ambalo limefuta leseni za vituo vingi vya habari, linasema linaheshimu jukumu la vyombo vya habari lakini halitaruhusu kutolewa habari inazoziona ni za uongo au zinaweza kusababisha ghasia kwa umma.
Ripoti moja ya Kamati ya Kuwalinda Waandishi https://bit.ly/3glb0WN mwezi uliopita imesema watawala wa Myanmar walikuwa wamefanya uandishi wa kujitegemea ni uhalifu.
Kikundi kinachofuatilia haki za binadamu Human Rights Watch mwishoni mwa mwezi uliopita kilisema serikali ya kijeshi ilikuwa imewakamata waandishi wa habari 98 tangu mapinduzi na kuwataka kuacha kuwafungulia mashtaka waandishi wa vyombo vya habari. Kati ya wale waliokuwa wamekamatwa, 46 walikuwa bado wako chini ya ulinzi hadi mwisho wa Julai.
Habari hii inatokana na Shirika la Habari la Reuters