Jumatano, Ofisi ya Mkurugenzi ya Mashtaka ya Umma (DPP) ilizua wasiwasi ilipofuta kesi za ufisadi dhidi ya aliyekuwa Mbunge wa Malindi na sasa Waziri Mteule wa Utumishi wa Umma Aisha Jumwa pamoja na kesi dhidi ya aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa shirika la Umeme la Kenya, Ben Chumo na wengine 10, kwa madai ya kukosekana kwa ushahidi wa kutosha kuendelea na kesi hizo.
Hatua hiyo ya DPP Noordin Haji ya kuondoa kesi hizo za ufisadi dhidi ya watu hao, inatajwa na chama hicho cha mawakili nchini Kenya, LSK kuwa hatari kubwa kwa misingi na utawala wa kisheria na inatia doa taswira, uaminifu na uwezo wa taasisi za uchunguzi kufuatilia kesi za ufisadi zinazowahusu wakuu serikalini na hata mashirika na taasisi za umma, kama anavyoeleza Mwaura Kabata ambaye ni mwanachama wa LSK.
Wakati akizungumza na vyombo vya habari jijini Nairobi, chama hicho kinaeleza kuwa wakati anapotekeleza mamlaka ya ofisi yake ya kikatiba, DPP Noordin Haji, anastahili kuzingatia ibara ya 157 inayomwezesha kufanya hivyo kwa kuzingatia maslahi ya umma, kutenda haki, na kuepukana na matumizi mabaya ya mfumo wa kisheria.
LSK kinasema kuwa kimesikitishwa na hatua ya DPP kwa sababu inazua kiwewe miongoni mwa raia wa Kenya kwa misingi kuwa huenda ofisi yake ilifuatilia kesi hizo kufikia madhumuni fulani au kuondolewa kwa mashtaka hayo kunatokana na shinikizo fulani.
DPP anatakiwa kuwajibika, kwa kuuelezea umma jinsi uamuzi wa mashtaka ulivyofikiwa mara ya kwanza, na kinachomfanya sasa kuyaondoa kimyakimya, na iwapo amefahamu kulikuwa na ubatili wa kiasi fulani, hakuufahamisha umma.
Chama hicho cha mawakili nchini Kenya, kinaitaka idara ya mahakama kumsisitiza DPP kueleza sababu za kuaminika za kuondoa mashtaka yanayowakabili baadhi ya washukiwa, kabla ya kuridhia ombi hilo, kwani kufanya hivyo kimyakimya ni kutumia idara ya mahakama kwa misingi isiyofaa, na matumizi mabovu ya muda na rasilimali za umma.
Bobby Mkangi, mtaalam wa katiba ya Kenya, ameiambia Sauti ya Amerika kuwa kuondoa kimyakimya kwa mashtaka kunaweza kutafsiriwa visivyo, bila maelezo ya kutosha.
Jumatano, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, chini ya kifungu cha 87 (a) cha taratibu za sheria inayohusu makosa ya jinai, amezua kiwewe kwa kuondoa kesi ya ufisadi dhidi ya aliyekuwa Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa, ambaye sasa ni Waziri Mteule wa Utumishi wa Umma, kwa kukosa ushahidi wa kutosha.
Aisha Jumwa, alikuwa anakabiliwa na mashtaka yanayofungamana na madai ya kula njama ya kufanya ulaghai katika kashfa ya ulipaji wa shilingi milioni 19 kinyume cha sheria, kutoka mfuko wa hazina ya ustawi wa eneo bunge la Malindi, ikiwa ni zabuni kwa wakandarasi wa kampuni ya Multiserve.
Pia, Bw Haji ameondoa mahakamani kesi ya ufisadi dhidi ya aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa shirika la Umeme la Kenya Ben Chumo, kwa kueleza kuwa hakuna ushahidi wa kutosha.
Chumo, pamoja na mrithi wake katika kampuni hiyo ya kusambaza umeme Ken Taurus, walishtakiwa mwaka 2018 kwa makosa yanayohusiana na ulipaji wa gharama ya ununuzi na usambazaji wa transforma mbovu zilizosababisha kupotea kwa umeme nchini Kenya wakati tofauti kati ya Aprili 2012 na Juni 2018 na kuifanya serikali kupoteza shilingi milioni 400.
Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma pia imeripotiwa kuwasilisha ombi la kufuta mashtaka ya ufisadi ya shilingi milioni 80 dhidi ya aliyekuwa gavana wa jimbo la Samburu Moses Lenolkulal lakini jaribio hilo lilisitishwa na mahakama hiyo ikitaka uthibitisho zaidi wa sababu za kufanya hivyo.
Wanasheria ncini Kenya wanaeleza kuwa mapambano dhidi ya ufisadi nchini Kenya huenda yakadidimia zaidi na kupoteza mwelekeo, kama zipo juhudi za kisiasa kuvuruga jitihada za kurejesha mali ya umma iliyopotea kupitia ufisadi.
Imetayarishwa na mwandishi wetu Kennedy Wandera, Nairobi, Kenya