Kimunya, na wenzake wawili wamefikishwa katika mahakama ya kusikiliza kesi za ufisadi ya Milimani kuhusiana na kesi ambayo mahakama kuu ilikuwa imewaondolea mwaka 2020, ya ulaghai wa kiasi cha shilingi milioni 60 kuhusu ununuzi wa ardhi.
Vyombo vya habari vya Kenya vinaripoti kwamba jaji Lawrence Mugambi amemwachilia Kimunya kwa dhamana ya shilingi 700,000 pesa taslimu, wakati anajitayarisha kujitetea.
Kimunya anakabiliwa na mashtaka 7 ya uhalifu.
Kesi yake inaanza kusikilizwa upya baada ya jaji wa mahakama kuu Esther Maina kuamuru kwamba mahakama ya chini ilikosea katika uamuzi wake wa awali, na kwamba wasimamizi wa mashtaka wamebaini kwamba Kimunya ana kesi nzito ya kujibu.
Mahakama ya chini ‘ilikosea’
Ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu ilikata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama ya chini kufutilia mbali kesi ya ulaghai na ufisadi dhidi ya Kimunya, na anakuwa afisa wa kwanza wa ngazi ya juu katika serikali ya rais mstaafu Uhuru Kenyatta, kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya ufisadi.
Kesi imepangiwa kuanza kusikilizwa Oktoba 31.
Kesi dhidi ya Amos Kimunya, ilianza mwezi March 2014 kutokana na madai ya kutenga kiasi cha ekari 24 za ardhi katika kaunti ya Nyandarua, kwa kampuni ya Midlands Ltd, mwaka 2005. Ana uhusiano na kampuni hiyo.
Ardhi aliyojitengea ilikuwa mali ya wizara ya kilimo na kwamba hakushauriana na wizara hiyo kabla ya kujitengea ardhi ya serikali.
Wakati huo, Kimunya alikuwa waziri wa ardhi.
Kesi ilifunguliwa baada ya tume ya kupambana na ufisadi kubaini kwamba likuwa amejitengea ardhi hiyo kinyume cha sheria.
“Heri nife kuliko kujiuzulu”
Hii si mara ya kwanza Amos Kimunya amejikuta katika kashfa ya ufisadi.
Mnamo mwaka 2008, akiwa waziri wa fedha, Amos Kimunya alisema kwamba “heri afe kuliko kujiuzulu,” alipokumbana na shinkizo la kutakiwa kujiuzulu kuhusiana na Sakata ya uuzaji wa hoteli ya serikali.
Alikumbana na mzozo wa ‘kuuza hoteli ya Grand Regency, Nairobi kwa gharama ya chini kabisa ya thamani ya hoteli hiyo.’
Bunge lilipiga kura ya kutokuwa na imani naye kuhusina na madai ya ufisadi. Kimunya alikana madai yote dhidi yake.
"Kitu ambacho sipo tayari kufanya, na ambacho sitafanya, ni kujiuzulu. Heri nife kuliko kujiuzulu,” Kimunya aliwaambia wafuasi wake katika mkutano wa kisiasa wakati alipokuwa anakumbana na shinkizo kutoka bungeni na kutoka kwa wanaharakati.
Kesi hiyo pia iliwahusisha aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga, waziri wa ardhi James Orengo na mkuu wa tume ya kupambana na ufisadi wakati huo Aaron Ringera. Hata hivyo, walikana madai kwamba walijua kuhusu uuzaji wa hoteli hiyo, Odinga akisisitiza kwamba alijua habari hizo kama hoteli tayari ilikuwa imeuzwa.
Iliripotiwa kwamba hoteli ilikuwa imeuzwa kwa kiasi cha shilingi bilioni 1.8, japo Kimunya alidai kwamba ilikuwa imeuzwa kiasi cha shilingi bilioni 2.95.
Mbunge wa chama cha Jubilee ahukumiwa miaka 67 gerezani
Wiki iliyopita, mahakama kuu nchini Kenya ilimhukumu mbunge wa chama cha Jubilee, chake rais mstaafu Uhuru Kenyatta, miaka 67 gerezani baada ya kupatikana na makosa ya ufisadi.
John Waluke (57), mbunge wa Sirisia, Kaunti ya Bungoma, magharibi mwa Kenya, alipatikana na makosa ya kuilaghai bodi ya taifa ya nafaka, kiasi cha shilingi milioni 313.
Alikuwa ameachiliwa kwa dhamana baada ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama ya chini.
Akitoa uamuzi wake, jaji wa mahakama kuu Esther Maina, amesema kwamba “mashtaka dhidi ya Waluke na mwenzake Grace Wakhungu, yaliyokuwa yakisikilizwa na jaji Elizabeth Juma, yana ushahidi wa kutosha dhidi ya washtakiwa. Hukumu waliyopewa sio kali sana inavyostahili. Ni hukumu iliyo katika sheria na hivyo kuhumu hiyo imekubaliwa na Mahakama hii.”
Mbunge Waluke alihukumiwa miaka 67 gerezani, huku mwenzake Grace Wakhungu akihukumiwa miaka 69.
Baadhi ya Sakata za ufisadi ambazo ziliripotiwa wakati wa utawala wa Uhuru Kenyatta
- Huduma ya vijana kwa taifa (NYS): Shilingi bilioni 1.9 zilipotea katika zabuni za huduma hiyo na washukiwa kadhaa waliachiliwa huru.
- Ununuzi wa vifaa vya tiba: Sakata la Afya House la shilingi bilioni 5 ambalo halijatatuliwa kufikia sasa
- Mfuko wa Pensheni: Serikali inadaiwa kupoteza shilingi bilioni 6.8 kutokana na sakata ya ujenzi wa makao makuu ya pesa za penshini, Hazina Towers.
- Ujenzi wa uwanja wa Ndege: Utoaji wa zabuni ya kujenga sehemu ya uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta kwa kiasi cha shilingi bilioni 55.6
- Unyakuzi wa ardhi ya Karen: Serikali iliripoti kupoteza kiasi cha shilingi bilioni 8. Ripoti zilisema kwamba maafisa katika wizara ya ardhi na baadhi ya wabunge walihusishwa na jaribio la kunyakua ardhi ya ukubwa wa ekari 134.4.
- Ununuzi wa kamera za CCTV: Shilingi bilioni 15 zilitumika kununua kamera za CCTV kuisaidia polisi kuimarisha usalama.
- Sakata ya Eurobond: Mkaguzi mkuu wa serikali Edward Ouko alidai kwamba kiasi cha shilingi bilioni 250 zilipotea mwaka 2014.
- Unyakuzi wa ardhi ya shule ya msingi ya Lang’ata
- Mradi wa NSSF Tassia wa kiasi cha shilingi bilioni 5
- Ununuzi wa makontena kwa ajili ya kutumiwa kama kliniki, sakata ambayo ilipewa jina “chickengate’ ambapo shilingi milioni 50 zililipwa kama hongo.
- Sakata ya wizi wa pesa kwa vijana ambapo shilingi milioni 80 zilipotea mwaka 2015
- Ujenzi wa reli ya mwendo wa wastani SGR iliyogharimu shilingi bilioni 314.2
- Sakata la upandaji wa miti katika shule za msingi ambapo kiasi cha shilingi bilioni 2 zilitumika vibaya.
- Wizi wa shilingi bilioni 7.8 kutokana na zabuni za ununuzi wa vifaa katika mamlaka ya kusambaza dawa (Kemsa) wakati wa janga la virusi vya Corona.