Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 19:59

Samia na Ruto waamrisha kuondolewa vikwazo 14 vya biashara


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan (Kulia) akiwa kwenye mazungumzo na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Kenya Dkt. William Samoei Ruto, mara baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan (Kulia) akiwa kwenye mazungumzo na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Kenya Dkt. William Samoei Ruto, mara baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Rais wa Kenya William Ruto ambaye yuko katika ziara ya siku mbili nchini Tanzania  katika mazungumzo yake na Rais Samia Suluhu Hassan Ikulu jijini Dar es Salaam, Jumatatu, walijadili kuhusu uhusiano wa kibiashra baina ya mataifa hayo mawili.

Pia marais hao wamewataka mawaziri wao wanaohusika na biashara kuhakikisha wanatatua changamoto za kibiashara, ikiwemo kuondoa vikwazo 14 vya biashara baina ya nchi hizo mbili.

Huku wachambuzi wakisema ujio wa Rais huyo utaleta manufaa kwa nchi zote.

Ni miaka miwili tu iliyopita Kenya na Tanzania zilikuwa na mahusiano yenye mikwaruzano ya mara kwa mara, huku kila taifa likimtuhumu mwenzake kwa mbinu chafu za kibiashara.

Hata hivyo katika siku za karibuni uhusiano wa Tanzania na Kenya uliodumu kwa miaka mingi, umeanza kuimaraika.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,. Samia Suluhu Hassan akiongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mazungumzo Rasmi na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Kenya Dkt. William Samoei Ruto pamoja na ujumbe wake Ikulu Jijini Dar es Salaam. Picha kwa Hisani ya Ikulu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,. Samia Suluhu Hassan akiongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mazungumzo Rasmi na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Kenya Dkt. William Samoei Ruto pamoja na ujumbe wake Ikulu Jijini Dar es Salaam. Picha kwa Hisani ya Ikulu

Mazungumzo baina ya Rais Samia Suluhu Hassan na Mgeni wake Rais William Ruto yanaashiria kuzidi kuifungua milango ya kibiashara kati ya mataifa haya mawili na kujadili kwa kina kuhusu kutafutiwa ufumbuzi wa haraka wa changamoto za kibiashara yenye lengo la kuzipeleka nchi hizo katika hatua nyingine.

Hii ni Mara ya kwanza kwa Rais wa Kenya William Ruto kuzuru Taifa hili la Tanzania tangu alipochukua uongozi kutoka kwa mtangulizi wake Uhuru Kenyatta.

Aidha Rais Ruto amesema uhusiano uliokuwepo kati ya Tanzania na Kenya umezisaidia sana familia hizi mbili ambapo ameongeza kuwa kupitia uhusiano huu Taifa la Kenya limefanikiwa kununua bidhaa nyingi kutoka Tanzania.

Ziara ya Rais Ruto nchini Tanzania inatazamiwa kuleta matumaini mapya kwa Nchi hizi hasa katika fursa za kibiashara na katika Nyanja za kisiasa na kijamii

Walter Nguma mchambuzi wa masuala ya kiuchumi kutoka Dar es Salaam amesema ziara ya Rais William Ruto itasaidia sana kuzimaliza changamoto za vikwazo vya kibiashara vilivyobaki na kuboresha dosari zilizopo hasa katika mipaka ya Nchi hizo.

Uhusiano baina ya Tanzania na Kenya ni wa kihistoria ni Msingi imara ulioasisiwa na Marais wa mwanzo wa mataifa haya Julius Nyerere na mwenzake Jomo Kenyata. bila shaka baada ya makutano hayo mahusiano ya kibiashara ya mataifa haya yataimarishwa mara mbili zaidi.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Amri Ramadhani, Dar es Salaam, Tanzania

XS
SM
MD
LG