Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 04:36

Hatua ya DPP yahofiwa itadidimiza vita dhidi ya ufisadi nchini Kenya


FILE - Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji speaks at his office in Nairobi, Kenya, July 23, 2019.
FILE - Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji speaks at his office in Nairobi, Kenya, July 23, 2019.

Mapambano dhidi ya ufisadi nchini Kenya yanaelezwa huenda yakadidimia zaidi na kupoteza mwelekeo, iwapo zipo juhudi za kisiasa kuvuruga jitihada za kurejesha mali ya umma iliyopotea kupitia ufisadi, wataalamu wa sheria na kisiasa nchini Kenya wanaonya.

Hii ni kutokana na hatua ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP)Kenya Noordin Haji Jumatano kufuta baadhi ya kesi za ufisadi zinazowakabili watu maarufu wanaotuhumiwa kwa vitendo vya ufisadi, Morara Omoke, wakili wa katiba nchini Kenya anaelezea.

Jumatano, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Kenya, chini ya kifungu cha 87 (a) cha taratibu za sheria inayohusu makosa ya jinai, ameondoa kesi ya ufisadi dhidi ya aliyekuwa Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa, ambaye sasa ni Waziri Mteule wa Utumishi wa Umma, kwa kukosa ushahidi wa kutosha.

Aisha Jumwa, alikuwa anakabiliwa na mashtaka yanayofungamana na madai ya kula njama ya kufanya ulaghai katika kashfa ya ulipaji wa shilingi milioni 19 kinyume cha sheria, kutoka mfuko wa hazina ya ustawi wa eneo bunge la Malindi, ikiwa ni zabuni kwa wakandarasi wa kampuni ya Multiserve.

Aisha Jumwa
Aisha Jumwa

Upande wa mashtaka umeondoa mashtaka dhidi ya Jumwa lakini washukiwa wengine nane walioshtakiwa wataendelea na kesi hiyo kwenye makosa yanayodaiwa kutekelezwa kati ya Mei na Oktoba, 2018 katika eneo bunge la Malindi, jimbo la Kilifi.

Jumatano, vile vile, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma imeondoa mahakamani kesi ya ufisadi dhidi ya aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa shirika la Umeme la Kenya Ben Chumo na watu wengine 10, kwa kusema kuwa hakuna ushahidi wa kutosha.

Chumo, pamoja na mrithi wake katika kampuni hiyo ya kusambaza umeme Ken Taurus, walishtakiwa mwaka 2018 kwa makosa yanayohusiana na ulipaji wa gharama ya manunuzi na usambazaji wa transforma mbovu zilizosababisha kupotea kwa umeme nchini Kenya wakati tofauti kati ya Aprili 2012 na Juni 2018 na kuifanya serikali kupoteza shilingi milioni 400.

Aidha, wakurugenzi hao wa zamani wa Kenya Power walikanusha mashtaka ya kula njama ya kutenda kosa, kusaidia kutendeka kwa uhalifu, kushindwa kimakusudi kufuata sheria za ununuzi, njama ya kutekeleza udanganyifu.

Vyombo vya habari nchini Kenya, pia vimeripoti Jumatano kuwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Kenya imewasilisha kesi ya kufuta mashtaka ya ufisadi ya shilingi milioni 80 dhidi ya aliyekuwa gavana wa jimbo la Samburu Moses Lenolkulal, lakini jaribio hilo lilisitishwa na mahakama baada ya Hakimu Thomas Nzioki kutaka uthibitisho zaidi na sababu za kufanya hivyo kuwasilishwa mbele yake.

Javas Bigambo, Mfuatiliaji wa Siasa za Kenya, anaeleza kuwa hatua ya DPP huenda ikakwamisha mapambano dhidi ya ufisadi nchini Kenya, kwani inaweza kutafsiriwa kama msukumo wa kisiasa.

Ofisi ya DPP, pia inatarajiwa kuondoa kesi zote dhidi ya watetezi wa haki za binadamu waliokamatwa kinyume cha sheria na kushtakiwa wakati wa operesheni za polisi, maandamano na matukio mengine ya aina hiyo, DPP Noordin Haji amenukuliwa na gazeti la Daily Nation, Jumatano.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Kennedy Wandera, Nairobi.

XS
SM
MD
LG