Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 04:56

David Mwaure: Nina agano kuu 12 kwa wakenya, mafisadi mpo taabani


David Mwaure mgombea kiti cha rais Kenya 2022
David Mwaure mgombea kiti cha rais Kenya 2022

Mgombea wa Urais nchini Kenya David Mwaure Wahiga amekuwa wa nne na wa mwisho kati ya wagombea wote wa nafasi hiyo katika uchaguzi wa mwezi Agosti 9, 2022 kuzindua manifesto yake.

David, ambaye ni wakili na mhubiri kanisani, anagombea urais kupitia kwa chama cha Agano.

Ana matumaini ya kuwa rais wa 5 wa Kenya. Mwaure anaamini kwamba ufisadi ndio mzizi wa matatizo yote nchini Kenya na kwamba ufisadi umeenea kila mahali. Hivyo, shabaha yake kubwa ni kuangamiza ufisadi. Haya ndiyo makuu katika manifesto ya David Mwaure Wahiga.

Kurejesha pesa zilizoibwa na kufichwa nje ya nchi

Mwaure anasema kwamba kuna utakatishaji wa fedha mkubwa sana nchini Kenya kwa kiasi kwamba ziadi ya shilingi za Kenya trilioni 4 zinaingia nchini humo kila mwaka kwa njia ambayo sio halali. Utawala wake itahakikisha kwamba kiasi chochote cha pesa kinachoingia Kenya bila kufuata sheria, zitakamatwa na kuwa mali ya serikali. Anaaini kwamba kiasi cha shilingi bilioni mbili hupotea kila siku kutoka serikalini kutokana na ufisadi. Kwa jumla, kila mwaka Kenya hupoteza shilingi trilioni 5. Amesisitiza kwamba changamoto za uchumi zinazowakumba Kenya, zinatokana na ufisadi unaoendeshwa kwa kiasi kikubwa na wanasiasa na vioongozi serikalini.

Kufanyia mabadiliko makubwa wizara ya kilimo

Kando na kuwa rais, David Mwaure amesema kwamba atakuwa Waziri wa kilimo. Lengo kubwa la kujitwika jukumu la kusimamia wizara ya kilimo ni kutaka kupambana vikamilifu na kile ametaja kama ufisadi ambao umekithiri na kuangamiza kilimo nchini Kenya.

“Hii leo hatuwezi kuzalisha chakula cha kutosha kulisha taifa. Rais atakuwa Waziri wa kilimo. Hililitawezekana kwa kubadilisha katiba ya Kenya na kusafisha kabisa uchafu ulio katika wizara hiyo.”

Manifesto ya Mwaure inasema kwamba endapo atachaguliwa kuwa rais, kila mfanyakazi katika wizara hiyo atafanyiwa uchunguzi maalum.

Waliokuwa mawaziri na katibu wa kudumu katika wizara ya kilimo watachunguzwa wote, sawa na mashirika yote yanayosimamia kilimo nchini Kenya.

Uagizaji wa chakula kama nafaka, nyama, mayai, mafuta ya kupika na vyakula vingine ambavyo vinaweza kuzalishwa Kenya, utapigwa marufuku mara moja ili kuinua motisha na mapato ya wakulima walio ndani ya Kenya. “Tutakula chakula chetu ambacho tumezalisha wenyewe.” Amesema Mwaure.

Sehemu za Kenya ambazo hazipati mvua ya kutosha kila mwaka, zitajihusisha na kilimo cha umwagiliaji maji, shirika la huduma kwa vijana NYS litakuwa na jukumu la kuzalisha chakula kwa niaba ya serikali.

“Nitafufua mikakati ya kutafuta soko kwa wakulima hasa zao la majani chai na kahawa. Kando na hayo, tutazindua viwanda vya kutengeneza mbolea ili tuachane na uagizaji wa mbolea ambao wanasiasa wanatumia kuendeleza ufisadi na kuibia nchi.” Amesema Mwaure, akiongezea kwamba mashirika ya serikali kama ya kusimamia uhifadhi wa nafaka, la kusimamia kilimo cha majani chai miongoni mwa mashirika mengine yataongozwa na watu waliochakuliwa na wakulima.”

Ufisadi katika sekta ya afya

Mara tu baada ya kuapishwa, endapo atashinda kiti cha urais, mgombea David Mwaure ameahidi kufutilia mbali zabuni zote ambazo serikali ya sasa imefanya na serikali zingine au kampuni mbalimbali kuhusiana na uagizaji wa vifaa vya matibabu au dawa. Marufuku hiyo itazingatia Zaidi zabuni ambazo ziemtajwa kufanyika katika mazingira ya ufisadi.

Wizara ya afya itafanyiwa ukaguzi wa kina, wafanyakazi wake kuchunguzwa na kutambua namna walivuopata mali walizo nazo hasa wafanyakazi wanaosimamia bima ya afya ya kitaifa NHIF.

“Serikali yangu itaanzisha tume ya kitaifa kusimamia sekta ya afya na kuhakikisha kwamba gharama ya matibabu inashuka katika hospitali zote hata za kibinafsi.”

Wataalam pekee kusimamia sekta ya elimu

Manifesto ya David Mwaure inasema kwamba serikali yake itapiga marufuku hatua zote za kubadilisha mfumo wa elimu zinazofanywa kiholela bila kupata ushauri wa kina na unaofaa kabisa kutoka kwa wataalam wa elimu na kwamba wizara yote ya elimu itasimamiwa na watu waliosomea namna ya kusimamia sekta ya elimu pekee.

“Serikali yangu itahakikisha kwamba kila mwanafuzi anasoma bila kulipa karo yoyote katika ngazi zote kutoka shule ya msingi hadi chuo kikuu. Kampuni au mashirika yanayotoa mafunzo kwa wanafunzi wanaomaliza masomo au wanaokaribia kumaliza masomo, na baadaye kuwaajiri, yatapunguziwa kodi au kupata msamaha wa kodi kwa mda Fulani.”

Mkaguzi mkuu wa serikali kupata mamlaka ya kufungua kesi

Ili kupamabana vilivyo na kesi za uhalifu na ufisadi, Mwaure ameweka agano na wakenya kwamba atatenga kiasi cha kutosha cha pesa kwa idhara ya mahakama ili kuhakikisha kwamba majaji wa kutosha wanaajiriwa, kesi zote za uhalifu na ufisadi zinasikilizwa katika mda usizidi miezi mitatu.

Mkaguzi mkuu wa serikali atakuwa na mamlaka ya kufungua kesi mahakamani endapo anagundua ubadhirifiu wa aina yoyote na tume ya kupambana na ufisadi itakuwa na mamlaka ya kuendesha kesi mahakamani.

Sheria kulazimisha mashirika kuwaajiri vijana na kupewa nafasi ya juu katika utoaji wa zabuni

Kwa kuzingatia kwamba Zaidi ya robo tatu ya idadi ya watu nchini Kenya ni vijana, ambao wamekuwa wakilalamika kwamba hawapati nafasi za kazi serikalini, Mwaure ameahidi kwamba endapo atakuwa rais wa tano wa Kenya, atahakikisha kwamba sehria imetungwa kulazimisha mashirika yote na viwanda nchini humo, yanaajiri vijana. Wanawake wanaojihusisha na biashara watapata msahama wa kodi inavyostahili na kupewa nafasi ya mbele katika utoaji wa zabuni za serikali.

“Tabia ya sasa ambapo walio serikali wanatoa zabuni kw awatu wa jamii zao na marafiki, itakoma mara moja. Haitawahi kutokea tena.” Ameahidi Mwaure.

Ukaguzi wa mapato ya wakusanyaji ushuru, kukuza viwanda

Maafisa wanaofanya kazi katika mamlaka ya kukusanya ushuru nchini Kenya, wametuhumiwa mda mrefu kwa ufisadi na kupelekea Kenya kupoteza mabilioni ya pesa kila mwaka. Manifesto ya Mwaure inasema kwamba hakuna mfanyakazi wa mamlaka hiyo ataruhusiwa kufanya kazi bila kuchunguzwa na kufanyiwa ukaguzi mkubwa namna alivyopata mali zake.

“mafisadi katika mamalaka ya kukusanya ushuru husababishia Kenya hasara ya shilingi bilioni 200 kila mwaka. Tutawachunguza namna walivyoapata mali zao.”

Bidhaa zote zinazoagizwa kutoka nje ya Kenya zitawekewa kiwango cha juu Zaidi cha ushuru ili kukuza viwanda na bidhaa zinazoliswa ndani ya Kenya. Hilo pia, Mwaure anaamini kwamba litaziba mwanya zote za ufisadi.

Mali iliyoibwa kurejeshwa kwa lazima

Mgombea huyo wa chama cha Agano, ameahidi kuunda tume maalum ya kurudisha mali yote ya serikali iliyoibwa. Tume hiyo itafanya kazi na tume ya ufisadi ili kuwanasa watu walioiba mali ya serikali.

“Mda wa miei sita utatolewa kwa watu walioiba mali ya serikali kurudisha ili waepuke kukamatwa na kushitakiwa. Wasipofanya hivyo mahakama maalum ya uhalifu wa kiuchumi, ambayo tutaunda, itawahukumu katika kikao kitakachofanyika ndani ya mda wa miezi 3.” Inasema manifesto ya Mwaure.

Ushoja, Usagaji na utoaji mimba

Manifesto ya chama cha Agano inasema kwamba endapo kitaunda serikali, kitahakikisha kwa vyovyote vile kwamba Maisha yanalindwa kutoka wakati mama anapata uja uzito.

Pia chama hicho kitahakikisha kwamba hakuna ndoa kati ya mwanamme na mwanamme au mwanamke na mwanamke inafanyika nchini Kenya. Ndoa au uhusiano wa kimapenzi utakuwa kati ya mwanamme na mwanamke.

Vijiji kuamua miradi serikali inastahili kutekeleza

Mwaure anaahidi wakenya kwamba kila familia itakuwa na angalau mtu mmoja ambaye ameajiriwa na kupata mshahara mzuri, kodi ya mishahara kupunguzwa kwa silimia 40, kiasi cha pesa kwa serikali za kaunti kuongezwa kwa asilimia 40, gavana wa jiji kuu la Nairobi kuteuliwa na rais na kujumulisha katika baraza la mawaziri, kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Kenya na jumuiya ya Afrika mashariki, umoja wa Afrika na jumuiya ya kimataifa, vijiji kuamua aina ya miradi inayostahili kutekelezwa na wala sio serikali kuu au za kaunti kufanya uamuzi huo, mikataba yote kati ya serikali nan chi zingine au mashirika hasa ujenzi wa reli SGR, barabara kuu na bandari kuwekwa wazi kwa wakenya.

Nguzo 12 za chama cha Agano

  • Agano kulinda katiba
  • Agano kulinda familia
  • Agano kuboresha Maisha ya vijana
  • Agano kutoa ajira na zabuni za serikali kwa vijana
  • Agano kuboresha na kulinda haki za walemavu
  • Agano kuimarisha ukuaji wa kila kaunti kwa kuongeza pesa kwa kaunti hizo kutoka serikali kuu
  • Agano kuboresha maslahi na mazingira kwa wafanyakazi
  • Agano la kuboresha mazingira ya kufanya biashara
  • Agano kuhakikisha kwamba uchumi wa Kenya unakua kwa haraka
  • Agano kwa taasisi za kidini
  • Agano la kulinda mazingira
  • Agano la kushirikiana na jamii ya kimataifa

“Tuhakikishe kwamba tubadilisha kabisa namna nchi inavyoendeshwa. Tubadilsihe uongozi. Tubadilishe namna serikaliinavyoendeshwa. Tubadilishe sheria na siasa za sasa. Agano letu ni kuleta mabadiliko.” Inasema manifesto ya mgombea urais David Mwaure.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG