Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Desemba 22, 2024 Local time: 19:39

Kenya: Upinzani wamshutumu Spika "kujitwika majukumu yasiyo yake"


Moses Wetangula, Spika wa baraza la wawakilishi la kitaifa, Kenya.
Moses Wetangula, Spika wa baraza la wawakilishi la kitaifa, Kenya.

Wabunge wa upinzani nchini Kenya chini ya Muungano wa Azimio La Umoja One Kenya wametaja uamuzi wa Alhamisi wa Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula kuukabidhi Muungano wa Kenya Kwanza wa Rais William kuwa Kiongozi wa Walio Wengi katika Bunge hilo kama utekwaji nyara wa bunge.

Visa vya fujo vilishuhudiwa katika bunge hilo Alhamisi alasiri wakati wabunge kadhaa wa chama hicho kinachoongozwa na aliyekuwa mgombea urais Raila Odinga walipomfokea Spika huyo na kumlazimu kuahirisha ghafla kikao cha bunge hilo.

Kutokana na kizaazaa hicho kilichoshuhudiwa bungeni humo wakati huo baada ya Spika Moses Wetang’ula kuamuru kuwa Muungano wa Rais William Ruto wa Kenya Kwanza ndio unaostahili kuchukua Kiongozi wa Walio Wengi katika bunge hilo kutokana na makubaliano ya kisiasa na vyama tanzu vilivyogura Muungano wa Odinga baada ya ushindi wa Ruto kuidhinishwa na mahakama ya juu, wabunge hao, licha ya kupinga vikali hatua ya Bw Wetang’ula kama isiyokingika kwa misingi ya kisheria, sasa wanadai kuwa kilichotukia Alhamisi, baada ya Rais Ruto kuzuru bunge hilo Jumatano kwa ghafla, ni utekaaji nyara wa bunge la Kitaifa, ambalo linastahili kuwa huru.

Mbunge wa Suna Mashariki, Junet Mohamed, anaeleza kuwa Spika alijinyakulia na kujilimbikizia mamlaka ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa pamoja na Mahakama ya Mizozo ya Vyama vya Siasa bila kuzingatia wajibu wake kulinda uhuru wa bunge la Kenya.

Katika kikao hicho cha Alhamisi, kwa dakika kadhaa, hata baada ya Spika Wetang’ula kuamuru kuwa maamuzi yake hayawezi kupingwa au kujadiliwa kwa hoja za nidhamu ndani ya bunge hilo, wabunge wa upinzani walionekana kuondokea viti vyao na kusimama pembeni mwa bunge hilo kuliko na Mesi ya bunge ambacho ni kielelezo cha mamlaka ya Spika na Bunge la Taifa, na hivyo basi kuwalazimu wapambe wa bunge hilo kukizingira na kumlazimu spika kukatiza kikao hicho kwa ghafla na kuvuga hoja iliokuwa inafuata ya kujadili hotuba ya rais.

Hata hivyo, wabunge hao wamekataa kuondoa uwezekano wa kuelekea mahakamani kupinga uamuzi huo anavyoeleza Mbunge wa Samburu Magharibi Naisula Lesuuda.

Spika Moses Wetang’ula, kwa kujenga maamuzi yake kwa misingi ya makubaliano ya kisiasa ya baada ya uchaguzi mkuu, yaliyowafanya wabunge 14 kugura Muungano wa Bw Odinga, na kujiunga na Muungano wa Rais William Ruto wa Kenya Kwanza, ameamuru kuwa kisheria Muungano huo ndio utakaochukua wadhifa wa Kiongozi wa Walio Wengi katika bunge hilo, kwa kuwa na idadi nyingi ya wabunge 179 dhidi ya wabunge wa Azimio La Umoja One Kenya, 157.

Muungano wa Ruto hata hivyo, umeukaribisha uamuzi wa Moses Wetangula kwa mikono miwili na kuutaja kama unaostahili katika mazingira ya sasa ambapo Bw Ruto anadhibiti mabunge yote mawili, kwa nafasi za uongozi, kama anavyoeleza Sylvanus Osoro, Mbunge wa Mugirango Kusini, ambaye kutokana na uamuzi huo, atakuwa kiranja wa Walio Wengi.

Wetangula katika uamuzi wake, vile vile alieleza kuwa Azimio la Umoja One Kenya hauwezi kudai kuwa ni chama cha kisiasa kwani hakina mbunge yeyote aliyechaguliwa chini yake.

Kutokana na maamuzi ya Wetang’ula, Kamati ya Kuratibu Shughuli za Bunge inayotwikwa majukumu ya upangaji wa shughuli zitakazofanywa na Bunge na mambo yote yanayohusiana na Kanuni za Kudumu za bunge, kuwapigia msasa walioteuliwa na Ruto kuwa mawaziri na nyadhifa nyingine, itaendelea na shughuli zake kwani sitntofahamu hiyo ilikuwa inasambaratisha uwezekano wa kutekeleza shughuli hizo.

-Ripoti imetayarishwa na Kennedy Wandera, VOA, Nairobi

XS
SM
MD
LG