Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 13:30

Mwandishi wa habari za uchunguzi akamatwa Tanzania


Joseph Gandye
Joseph Gandye

Mwandishi wa habari Tanzania amekamatwa kwa madai ya kuchapisha habari za uongo baada ya kutangaza habari ya ukatili unaofanywa na jeshi la polisi, wakili wake amesema Ijumaa.

Joseph Gandye ambaye anafanya kazi katika kituo cha Televisheni cha Watetezi, alikamatwa Alhamisi mjini Dar es Salaam na kuzuiliwa usiku kucha rumande.

Kwa mujibu wa wakili wake Jones Sendodo, mteja wake alihamishwa kwenda kituo cha polisi mkoa wa Iringa ulioko kusini mwa Tanzania siku ya Ijumaa.

Mkuu wa Polisi wa Iringa alipinga vikali taarifa hiyo Agosti 14 na kutoa onyo kali dhidi ya kupakwa matope kwa jeshi la polisi na maafisa wake. Hivi leo polisi imesema kuwa bado yuko mikononi mwao mjini Iringa na hajafikishwa mahakamani.

Wakati huohuo taarifa juu uminyanji wa uhuru wa habari unaoendelea hivi sasa nchini humo zimeendelea kuripotiwa katika vyombo vya habari ndani na nje ya Tanzania.

Watetezi TV inamilikiwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binaadamu Tanzania (THRDC) na imejikita zaidi kwenye taarifa za ukiukwaji wa haki za binaadamu nchini humo.

Kwa mujibu wa Mratibu wa Kitaifa wa THRDC, taarifa iliyomtia matatani Gondye inahusu tuhuma za polisi mkoani Iringa kuwalazimisha mahabusu kulawitiana katika kituo cha Mafinga.

Mahabusu hao sita walikuwa wanakabiliwa na tuhuma za kumuibia mwajiri wao na wanadaiwa kupigwa pia na polisi.

"Juni 17, waandishi wa Watetezi TV walipokea ripoti za matendo hayo ya kudhalilisha katika kituo cha polisi Mafinga, mkoani Iringa. Baada ya kupokea taarifa, Joseph Gandye alisafiri kwenda Iringa na kufanya uchunguzi wa kina kisha kuchapisha taarifa hiyo kwenye mitandao (ya Watetezi TV) ya Facebook, Twitter na You Tube," inaeleza taarifa kutoka THRDC.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG