Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Novemba 05, 2024 Local time: 11:03

Mkurugenzi wa VOA asema bila ya vyombo vya habari huru hakuna demokrasia


Mkurugenzi wa VOA Amanda Bennett alipozuru Kitu cha Ufanisi wa Vyombo vya Habari Afrika (ACME) Kampala, Uganda.
Mkurugenzi wa VOA Amanda Bennett alipozuru Kitu cha Ufanisi wa Vyombo vya Habari Afrika (ACME) Kampala, Uganda.

Nchini Marekani Marekebisho ya Kwanza ya Katiba juu uhuru wa vyombo vya habari siyo kwa kubahatisha kwa sababu ni pale tu unapokuwa na vyombo vya habari huru vinavyoweza kuwafikishia wananchi habari zisizominywa, vinginevyo huwezi kuwa na jamii yenye demokrasia.

Mkurugenzi wa Sauti ya Amerika Amanda Bennett ameeleza hayo ikiwa ni sehemu ya ujumbe wake kwa dunia katika kuadhimisha Siku ya uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani leo Ijumaa.

Kwa nini serikali zinataka kuhodhi habari

Amefafanua kuwa “ unaweza kuona pande mbalimbali za dunia wakati serikali zikikabiliwa na matatizo au wakifanya kitu ambacho wananchi hakiwapendezi kama vile mapinduzi, kupinga matokeo ya uchaguzi, ndio wakati ambao huvifungia vyombo hivyo vya habari.”

Mkurugenzi huyo anasema sababu ya serikali hizo kukandamiza vyombo hivyo ni wanajua habari inawapa wananchi nguvu. “Na iwapo watu watapata habari za kutosheleza, wataweza kupima uwezo wa viongozi wao, na ndio sababu wanavifungia vyombo vya habari ili kuhodhi habari zote wao wenyewe.

Miaka 75 ya VOA kutekeleza majukumu

“Bila ya shaka kwa muda wa miaka 75, VOA imeendelea kutekeleza jukumu lake la kutoa habari na taarifa za kuaminika, zinazoweza kuthibitishwa, zisizo kandamiza upande wowote kwa nchi ambazo hazina njia nyingine ya kupata habari hizo. Hivyo tunapeperusha matangazo yetu katika nchi ambazo hazina ushirikiano mzuri kabisa na mataifa mengine ulimwenguni.,” amesema Mkurugenzi.

Amanda amesema inashtusha kufahamu kuwa ni asilimia 13 tu ya nchi zote duniani wanaweza kupata habari kutoka vyombo huru. “Na hao ndio wasikilizaji wetu tunaowatangazia na tunafikiria kuwa ni muhimu watu waweze kupata habari ambazo wataziamini.

Hatari zinazowakabili waandishi

"Katika nchi ambazo vyombo vya habari haviko huru waandishi wetu wanakabiliwa na uhalisia wa jaribio la kuzuiliwa wasikusanye habari, watu wanajaribu kuwanyang’anya vifaa vyao, wanapigwa, lakini tunashukuru kwamba hakuna yoyote aliyefungwa jela. Lakini wanakabiliwa na uwezekano wa kuwekwa kizuizini. Kwa hivyo wanakabiliwa na vitisho vilevile vinavyowakabili waandishi wazawa katika nchi hizo. Na tunawategemea hawa waandishi shujaa kutupatia habari kutoka katika nchi wanazofanya kazi," amesema Amanda.

Akieleza kuhusu ziara zake alizofanya Afrika, amesema aliweza kukutana na waandishi wa habari nchini Uganda, ambapo wengi wao walikuwa wamepigwa katika harakati zao za kutekekeza majukumu ya kazi zao. “Pia niliweza kukutana na waandishi wa habari kutoka maeneo mbalimbali ya Afrika, makundi mbalimbali tuliyoyaleta pamoja.

Ila ya baadhi ya wamiliki wa vyombo vya habari

“Pia walinieleza kuhusu matatizo ya kufanya kazi katika mfumo wa chombo cha habari, ambacho maamuzi ya kutangaza habari yanamilikiwa na mtu mwenye ajenda yake binafsi. Kwa hivyo waliniambia , unajua, tunaweza kuwa waandishi mahiri sana duniani, tunaweza kuripoti habari bora zaidi duniani, lakini hatupati mtu kuzitoa habari hizo kwa sababu baadhi ya wamiliki wa vituo vya habari hawaruhusu zitolewe. Kwa hivyo hilo ni tatizo kubwa,” amesema Mkurugenzi Amanda.

Pia Mkurugenzi ameeleza matatizo yanayowakabili waandishi kutokana na malipo duni katika bara la Afrika, tunajaribu kujiepusha na utamaduni wa bahasha zinazotolewa na vyanzo vya habari kwani huko ni kuvuka mipaka ya uandishi. “Lakini wanasema kuwa hawalipwi mishahara ya kuwawezesha kujikimu kwa hiyo ni changamoto kwao.”

Aliyojifunza Mkurugenzi ziara yake Afrika

Amesema katika mahojiano haya na mwandishi wa VOA kwamba wakati akizungumza na waandishi katika safari yake hiyo Afrika ilimkumbusha hali iliyokuwa inawakabili “marafiki zangu na mimi mwenye takriban miaka 40 iliyopita, kulikuwa na wanawake wachache, matarajio ni kuwa hutaweza kufanya kazi hiyo ya uandishi, kulikuwa na kipingamizi kikubwa kukuruhusu ushiriki katika kazi hii.”

Amanda amesema kuwa unapozungumzia viwango vya uandishi, moja ya vipimo vya uandishi ni kujaribu kutafuta njia ya kuthibitisha vitu vinavyotokea, na kuzungumza na pande zote zenye mvutano.

Hivyo ikiwa upande moja hautaki kuongea na wewe, aghlabu unaweza kutafuta ukweli kutoka upande mwengine, na unaweza kuleta uwiano wa hiyo habari kwa njia hiyo.

“Na jambo jingine ni kuweza kuthibitisha matukio, kwa kutafuta ukweli, hilo kwa kweli ni muhimu tujitahidi na tutekeleze," alisisitiza.

Aliongeza kuwa : "Na nafikiri hiyo ni nguvu tuliokuwa nayo ya kuwa na operesheni kubwa hapa Marekani, kwani waandishi wetu wanaweza kuwasaidia waandishi walioko katika maeneo ya matukio kupata habari zaidi na kuthibitisha ukweli wa habari hizo."

Tuhuma za Burundi dhaifu

Mkurugenzi wa VOA amesema kuwa serikali ya Burundi kusema kuwa imeifungia VOA na shirika la habari la Uingereza, BBC, kwa sababu ya kusambaza habari feki ni jambo la kusikitisha, kwa sababu tunajua kitu chochote potofu siyo habari. Na kutumia maneno kama hayo ni maneno yasiyokuwa na maana, kufunga operesheni halali za kukusanya habari wakati wowote zinapotokea duniani. Huo ni msiba kweli kweli. Na hilo limetokea Burundi, VOA imefungiwa, alisema.

Amanda amesema : Na hivyo nafikiri inawapa njia fulani wasikilizaji angalau kufahamu kuwa wakipata habari kutoka chanzo cha kuaminika, watapata fikra kuwa kile ambacho tunatangaza ni karibu na ukweli ambao wanaweza kwa juhudi zao zote kuufikia. Nafikiri sisi nahisi ni kama nanga katika mawimbi makali, na vyombo vya habari vya kuaminika vinaongezeka kuwa ni nanga ya aina hiyo wakati habari nyingine zikiwa zinaelea pembezoni.”

XS
SM
MD
LG