Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 10:04

Mahakama yaamuru Tanzania kurekebisha Sheria ya huduma ya habari 2016, yasema inakiuka mikataba ya kimataifa


Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo nchini Tanzania, Waziri Harrison Mwakyembe
Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo nchini Tanzania, Waziri Harrison Mwakyembe

Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Alhamisi imeiamuru Tanzania kurekebisha sheria yake ya huduma ya habari ya mwaka 2016.

Mahakama hiyo imesema uamuzi huo umefikiwa baada ya sheria hiyo kuonekana inakiuka mkataba wa uanzishwaji wa Jumuiya hiyo na mikataba mingine ya kimataifa ambayo nchi hiyo imeridhia.

Maelekezo hayo yametolewa katika hukumu ya kesi ya kupinga ukandamizaji wa uhuru wa vyombo vya habari iliyokuwa imewasilishwa na Baraza la habari Tanzania, MCT, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, LHRC, na mtandao wa watetezi wa haki za binadamu.

Asasi hizo tatu ambazo kwa pamoja zilifunguwa kesi katika Mahakama ya Afrika Mashariki, dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupinga baadhi ya vifungu katika sheria hiyo.

Hukumu hiyo imetolewa mbele ya Jopo la majaji watatu Jaji Charles Nyachae, Monica Mugenyi na Jaji Justice Ngie.

Mwanasheria wa asasi hizi tatu anasema kuwa maamuzi ya mahakama hii yanatekelezeka na wameahidi kurudi mahakamani kuomba amri ya kutekeleza maamuzi hayo iwapo serikali ya Tanzania haitatekeleza uamuzi wa mahakama.

"Kwa hiyo kwa kusema hayo maamuzi sasa nini kitafanyika, Tanzania ni sehemu ya mkataba wa Afrika Mashariki, inatakiwa itekeleze maamuzi ya mahakama hiyo," wakili huyo amesisitiza.

Akisoma hukumu hiyo Jaji Nyachae amesema vifungu vilivyo kwenye sheria hiyo ni vibovu na vinakiuka mkataba wa uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Hivyo Jaji ameitaka Serikali ya Tanzania kurekebisha vifungu vya Sheria ya Uhuru wa Habari kutokana na kukiuka Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Sheria hii inapaswa kufanyiwa marekebisho ili iendane na mkataba wa uanzishwaji wa Jumuiya,” amesema Jaji Nyachae.

Akizungumza baada ya hukumu hiyo kutolewa, Katibu wa MCT, Kajubi Mukajanga amesema leo ni siku ya kihistoria na ushindi kwa wanahabari na ushindi kwa Serikali kwani imepewa wasaa wa kwenda kurekebisha sheria hiyo.

“Demokrasia leo imeshinda haki ya wanahabari kufanya kazi bila kuingiliwa imethibitishwa leo na Mahakama ya Afrika Mashariki,” amesema Mukajanga.

Katibu mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga na baadhi ya wanasheria wamezungumzia hatua hiyo huku wakieleza kuwa haki imetendeka na sasa wanasubiri utekelezaji wa amri hiyo kwa upande wa serikali ya Tanzania.

Mwaka 2016 Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha
sheria yahuduma ya vyombo vya habari ambayo ililalamikiwa na
wadau wote kuwa inakandamiza uhuru wa habari hatua iliyopelekea
wadau haokwenda mahakamani.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Washington DC

XS
SM
MD
LG