Gazeti la “The Citizen” linalochapishwa nchini Tanzania limeandika kuwa Kenya imeipiku Tanzania.
Tanzania imeshuka daraja saba kwa mwaka mmoja uliopita , na kupata jumla ya alama 45 tofauti na utafiti wa 2018 ulioipa alama 53.
Lakini Ripoti hiyo 'Freedom in the World Report 2019' iliyotolewa siku ya Ijumaa inaonyesha kwamba Kenya ndio inayoongoza kidemokrasia miongoni mwa mataifa ya Afrika mashariki.
Kenya
Maridhiano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga ni yaliyoifanya Kenya kuwa katika sura tofauti ya kisiasa na ilichangia kujipatia alama 48.
Mwaka 2018 ripoti iliyotolewa ilikuwa inaonyesha Kenya imeshuka kidemokrasia.
Katika ripoti ya mwaka 2019 Burundi imechukuwa nafasi ya mwisho kama taifa lenye uhuru wa kisiasa kwa kupewa alama 18 ikifuatiwa na Rwanda yenye alama 23 na Uganda ilipata alama 37.
Tafiti hiyo inaeleza kuwa licha ya kuwa Tanzania na Kenya zina alama tofauti zote mbili ni katika mataifa yanayoorodheshwa kuwa na uhuru mdogo wa kidemokrasia.
Burundi, Uganda na Rwanda
Kwa mujibu wa ripoti hiyo orodha nyengine ni ya mataifa yalio 'huru' na 'yasio huru' ambapo Uganda, Burundi na Rwanda ni mataifa yasio na uhuru wa kidemokrasia.
Tanzania
Utafiti huo uliofanywa na shirika la Freedom House, umeiweka Tanzania miongoni mwa mataifa 10 yanayofuatiliwa mwenendo wake wa kidemokrasia katika mwaka 2019 .
Freedem House ni shirika huru lenye makao yake Marekani lilojikita katika kueneza uhuru na demokrasia duniani kote.
Mbali na Tanzania , mataifa mengine yanayoangazwa na shirika hilo ni Armenia, Brazil, Cambodia, Cameroon, China, Ethiopia, Iraq, Poland na Sri Lanka.
Sababu za kushuka daraja
Ripoti hiyo inaeleza sababu za kushuka daraja kwa Tanzania ni kufuatia hatua ya serikali kuwaweka ndani viongozi wa upinzani, kuzuia maandamano dhidi ya serikali na kupitisha sheria zinazokipendelea chama tawala katika siasa za ngazi za chini 2018.
Uganda ilishuka kutoka taifa lenye 'Uhuru kiasi' hadi lisilo na Uhuru kutokana na Rais Yoweri Museveni kuzuia uhuru wa kujielezea, kuvidhibiti vyombo vya mawasiliano mbali na kuidhibiti mitandao ya kijamii kwa kuweka kodi.
Rwanda imepata alama hizo kutokana na ukamataji wa viongozi wa upinzani na matishio yanayotolewa na Rais Kagame kwa vyama vya siasa.
Kadhalika ripoti inasema uongozi wa Kagame wa kidikteta umeathiri vibaya demokrasia nchini humo.
Kwa upande wa Burundi imepata alama hizo kutokana na uongozi wa Rais Pierre Nkurunziza Kuendelea kuwanyamazisha wapinzani na kukiuka katiba.