Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 05:19

Hotuba ya Hali ya Taifa: Kenyatta awaomba Wakenya msamaha


Rais Kenyatta akiapishwa baada ya kushinda uchaguzi wa urais Novemba 2017 nchini Kenya.
Rais Kenyatta akiapishwa baada ya kushinda uchaguzi wa urais Novemba 2017 nchini Kenya.

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amewaomba msamaha wananchi wote walioathiriwa na hali ya kisiasa iliyojiri nchini humo mwaka 2017.

Hotuba ya hali ya kitaifa alioitoa Jumatano imekuja baada ya taifa la Kenya kujitosa katika uchaguzi ulioligawa na kudumaza uchumi wa nchi hiyo.

Kenyatta amekiri kuwa Kenya ilishuhudia jinsi wanasiasa walivyozomeana waziwazi na kutupiana maneno machafu machafu yaliyokuwa yanaeneza chuki huku ukabila ukijitokeza tena.

Lakini kama kiashiria cha kutaka mkondo huo usijirejee tena nchini humo, Rais Kenyatta aliwataka viongozi wa kisiasa kuwaomba Wakenya msamaha. Yeye alikuwa wa kwanza kufanya hivyo na kuwataka wengine waige mfano huo huku akimpa mbunge wa upinzani mkono wa salamu.

"Iwapo kipo chochote nilichokisema kikamuudhi au kikamwuumiza yeyote,na iwapo nilivunja umoja wa nchi kwa njia yoyote, nawaomba msamaha, nakuomba ujiunge nami tubadilishe hilo," amesema Kenyatta.

Leo ni miezi miwili baada ya Rais Uhuru Kenyatta kukutana na Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga na kuzika tofauti zao za kisiasa na kuwataka wananchi wa taifa hilo kushirikiana katika maendeleo ya taifa.

Hotuba ya Rais Kenyatta pia imesisitiza kuwa Kenya itaendelea kuimarisha juhudi za kutafuta suluhu ya kudumu katika mgogoro wa kisiasa unaolikabili taifa la Sudan Kusini na vile vile kuimarisha amani nchini Somalia.

Kando na kusisitiza kuwa serikali yake imeendelea kufanikisha utekelezaji wa katiba hususan serikali za majimbo 47, Rais Kenyatta ameeleza kuwa mgao wa rasilimali kwa asilimia 15% kwa majimbo haya umefanikishwa lakini akawaonya viongozi dhidi ya kujitosa katika ubadhirifu wa rasilimali za umma.

Kenyatta anaeleza kuwa serikali yake imesambaza kima cha shilingi bilioni 210 mwaka wa matumizi ya serikali wa 2013/14 na shilingi bilioni 327 mwaka 2017/18 kwa miaka mitano iliyopita.

Kwa mujibu wa katiba ya Kenya, Rais Uhuru Kenyatta anatakiwa kila mwaka kueleza wananchi mafanikio ya serikali yake, miradi aliyoanzisha iliyo na uwezo wa kuwanufaisha, hali ya usalama wa nchi na mahusiano ya taifa na nchi za kigeni pamoja na mwongozo wa utekelezwaji wa katiba ya Kenya.



XS
SM
MD
LG