Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 20:28

Chama kikuu cha upinzani Uganda -FDC-chagawanyika


Forum for Democratic Change party president Mugisha Muntu
Forum for Democratic Change party president Mugisha Muntu

Chama kikuu cha upinzani nchini Uganda kimegawanyika kufuatia tangazo la aliyekuwa rais wa chama hicho Mugisha Muntu kwamba ameamua kuondoka katika chama hicho baada ya mazungumzo na wafuasi wa chama na juhudi za maridhiano ndani ya chama kushindwa kufaulu.

Mugisha Muntu, ambaye alikuwa rais wa chama hicho ametangaza uamuzi huo baada ya kikao na uongozi chini ya rais wa sasa Patrick Amuriat.

Hata hivyo, Muntu hajatangaza mwelekeo wake mpya, lakini tayari kuna minong’ono kati ya raia wa Uganda kwamba anaelekea kushirikiana na mbunge Bobi Wine katika safari mpya ya kisiasa.

Uamuzi wake unafuatia miezi saba ya majadiliano na wanachama wa FDC kote nchini Uganda baada ya uchaguzi uliokumbwa na utata wa chama hicho, na kuacha nyufa chungu nzima ndani ya chama hasa baada ya Dkt Kiiza Besigye aliyekuwa mgombea urais Uganda kwa tikeyi ya chama hicho, kuonyesha hadharani kumuunga mkono Patrick Amuriat na kumpinga vikali sera za Muntu.

Kupitia ukurasa wake wa facebook, Muntu ameandika taarifa fupi kuhusu mkutano wake na uongozi wa sasa wa FDC, na kueleza nia yake ya kuondoka chamani.

Juhudi za kumfikia kwa mahojiano hazikufaulu, huku akituma ujumbe kwamba ataandaa kikao na waandishi wa habari siku ya alhamisi. Wachambuzi wa siasa kama Akol Amazima, wanasema, kuondoka kwa Muntu, kusingeweza kuepukika.

“Katika FDC kuna wale wenye msimamo mkali wa kufanya mambo kwa kudharau sera na masharti ya serikali iliyopo sasa, kama mbinu ya kuendeleza siasa za upinzani. Lakini Muntu na wafuasi wake wanaona kwamba diplomasia ndiyo njia pekee upinzani unaweza kuchukua ili kumuondoa Museveni madarakani” amesema Amazima

Mzozo ndani ya chama cha FDC ulifikia kilele chake na kufichuliwa hadharani mwezi August, baada ya rais wa chama wa sasa Patrick Amuriat, kubadilisha uongozi wa chama cha FDC bungeni, na kuwafuta kazi waakilishi wake waliokuwa wameteuliwa na Mugisha Muntu, wakati alikuwa rais wa chama.

Muntu na Bobi Wine

Wachambuzi wa siasa za Uganda wanasema kwamba huenda chama kipya atakachounda Mugisha Muntu, kikawa na uhusiano na Bobi wine, mwanamziki ambaye amepata umaarufu wa kisiasa, kushinda kiti cha bunge bila kuungwa mkono na chama chochote cha kisiasa, anayeendeleza siasa zake kwa kutumia nguvu za watu, maarufu kama “people’s power.”

“Bobi Wine anaamini kwamba vijana, kwa hali yoyote ile, watetee haki zao hata kama ni kujitoa mhanga ili kuleta mabadiliko Uganda. Mugisha Muntu kwa upande wake, anaamini kwamba maridhiano, utaratibu na kufanya mambo kwa upole ndio njia pekee ya kuleta mabadiliko. Itikadi zao kwa sasa ni tofauti. Lakini kwa sababu sasa wote hawana chama, wanaweza kuingia katika ndoa ya muda tu” ameendelea kusema Amazima.

Wanachama maarufu wa FDC wanaomwunga mkono Muntu ni pamoja na Angeline Osege, Abdu Katuntu, Reagan Okumu, Winnie Kiiza, Kassiano Wadri, Gerald Karuhanga, Anita Among miongoni mwa wengine ambao wanajulikana kuwa na ushawishi mkubwa ndani na nje ya bunge.

Baadhi ya wabunge hao, wameonekana katika misafara ya Bobi Wine kila mara na ni miongoni mwa wale wanaokabiliwa na mashtaka ya uhaini kufuatia tukio la wilaya ya Arua, ambalo rais Museeveni anadai walipiga mawe gari lake na kupasua vioo.

Lakini mchambuzi wa siasa za maziwa makuu Charles Rwomushana, anasema kwamba kwa kuzingatia historia ya Uganda na majirani wake, ndoa ya kisiasa kati ya Muntu na Bobi Wine haiwezi kuleta mabadiliko.

“Hakuna mageuzi ya kisasa wanayoweza kuleta. Museveni ana tume ya uchaguzi na mahakama ya rufaa. Hata wakipata ufuasi wa wapiga kura wote, hawawezi kuleta mageuzi” amesema Rwomushana.

Uhusiano wa Muntu na Besigye

Mnamo miaka ya 1990, kundi la wanasiasa mashuhuru kutoka jamii ya Ankole, likiongozwa na Amanya Mushega, Eriya Kategaya, Kizza Besigye na Bidandi Ssali lilianza mchakato wa kuunda vuguvugu lenye lengo la kumuondoa rais Museveni madarakani.

Kwa sababu Dkt Kiiza Besigye alikuwa amewahi kuwa waziri wa mambo ya ndani, pamoja na kuwa kamisaa katika chama cha National resistance Army chake Museveni wakati huo, kundi hilo la siasa lilihitaji msaada wake sana.

Kundi hili la wanasiasa, halikumtaka rais Museveni kuwania urais mwaka 2001 na badala yake kumtaka Bidandi Sali kuwania urais kwa sababu wakati huo Besigye alikuwa na umri mdogo ikilinganishwa na wenzake ambao tayari walikuwa wamezeeka, alipewa jukumu la kuzuru kote Uganda kuwashawishi viongozi wa NRM kutomuunga mkono Museveni, jambo ambalo alifanikiwa.

Aliporejea Kampala, Besigye alitoa ripoti yake kwa Bidandi Sali, lakini kwa siri, Bidandi akampelekea Museveni ripoti yake Besigye na kumshitaki kwamba Besigye alikuwa na njama ya kumpindua.

Besigye alichukua hatua za haraka na kustaafu kutoka jeshi katika hatua wachambuzi wanasema ilikuwa ya kuepuka kushitakiwa katika mahakama ya kijeshi.

Besigye baadaye aliwania urais mwaka 2001 na baada kutorokea uhamishoni Afrika kusini baada ya kushindwa na Museveni.

Mwaka 200, Besigye alifanya mazungumzo na Mugisha Muntu yaliyolenga

Uchaguzi mkuu wa 2006

Besigye alikamatwa aliporejea Uganda kutoka Afrika kusini na kufunguliwa mashtaka ya uhaini na unajisi. Wakati Ugand ainajitayarisha kwa uchaguzi mkuu, alikuwa anazuiliwa katika gereza la Luzira.

Wanachama wa FDC, waliokuwa wanamuunga mkono Mugisha Muntu, waliamua kumteua Muntu kuwania urais, hatua ambayo iliwakasirisha wafuasi wake Besigye, waliosaini karatasi zake Besigye na kumsajili kuwania urais wakati alikuwa gerezani.

“Tulikuwa tumepanga kumteua Besigye hata kama hakuwepo. Wanachama wa FDC kote nchini walikuwa wamekubaliana” alisema Ingrid Turinawe katika ripoti yake ya hivi karibuni.

Hatua hii ilipelekea Muntu, kukosa kuwania urais kwa mara ya pili; 2001 na 2006.

Uchaguzi wa FDC

Uhasama ndani ya FDC uliendelea baada ya uchaguzi ndani ya chama wa mwaka 2017, Besigye akimuunga mkono Patrick Amuriat dhidi ya Mugisha Muntu. Amuriat, alimshinda Muntu.

Kundi la Muntu liliripoti kutofurahishwa na jinsi uchaguzi huo ulivyoendeshwa, na kuanza mazungumzo kati ya wafuasi wake kuhusu hatma yao katika chama, ambayo matokeo yake yamepelekea Muntu kujiondoa FDC.

“Ukweli ni kwamba tangu Amuriat achaguliwe, ameshindwa kukiunganisha chama. Ameegemea sana wanasiasa ambao ni wa msimamo mkali ndani ya FDC, wnaomuunga mkono Besigye, n ahata kuwafuta kazi viongozi wa chama bungeni walioteuliwa na Muntu, ambao msimamo wao ni kufanya mambo kwa kutumia diplomasia” amesema Akol Amazima, mchambuzi wa siasa za Uganda

Japo hajatangaza iwapo ameunda chama chake, wachambuzi wanasema kwamba anayenufaika katika mgogoro kati yake na Besigye ni Rais Museveni ambaye siku zote ndoto yake ni kuona upinzani umegawanyika.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG