Baada ya kupita bungeni muswada huo unatarajiwa kusainiwa na Rais Magufuli.
Makundi mbalimbli vikiwemo vyama vya siasa vya upinzani na asasi za kiraia wanadai utaminya demokrasia, na ni uonevu mkubwa dhidi ya vyama hivyo.
Lusinde asema utaondoa uhuni
Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde maarufu Kibajaji amesema muswada huo unalenga kuondoa uhuni na kuvifanya vyama vya siasa kufanya kazi kwa ukomavu.
Akichangia muswada huo bungeni Jumatano, Lusinde amesema muswada huo unalenga pia kuviimarisha zaidi vyama vya siasa.
“Tukomae tufanye kazi za ukomavu, siyo kuzunguka kwenye corridor (viambaza) za mabalozi. Sheria zinatungwa ndani ya Bunge, viatu vinaisha soli,” amesema.
Amesema muswada huo unakwenda kuvitaka vyama vya siasa kutambua tunu za Taifa ikiwamo Mwenge na Mapinduzi ya Zanzibar.
“Msajili alikuwa akihudhuria kama mualikwa sasa anasimamia na kuangalia demokrasia kama inatekelezwa ndani ya chama,”amesema.
Amesema muswada haukatazwi kulindwa kwa chama chochote cha siasa na hakuna chama ambacho kimekatazwa kuwa na mlinzi wa kukilinda.
Bulaya awatahadharisha wabunge
Katika kutoa dosari za muswada huo na hatari zake Waziri kivuli na Msemaji wa kambi ya upinzani bungeni, Ester Bulaya alisisitiza kuwa wabunge wana uwezo mkubwa wa kuzuia uonevu huo ikiwa watapenda kufanya hivyo.
Bulaya ametoa mfano wa vifungu vinavyo kandamiza upinzani katika muswada huo ikiwemo kifungu kinachompa mamlaka msajili wa vyama vya siasa kuingilia mfumo wa uchaguzi ndani ya chama.
Ametahadharisha kuwa kifungu hicho kitapunguza uhuru wa vyama kufanya chaguzi bila mashinikizo kutoka ofisi ya msajili.
Kifungu kingine ni kile kinachotoa masharti ya namna ya utoaji wa elimu ya uraia, akisema kuwa masharti hayakutilia maanani kuwa vyama vya siasa vina mahusiano ya kiitikadi na vyama rafiki toka nje ya nchi.
“Ni haki yao ya msingi ya kueneza itikadi za vyama vyao bila kujali mipaka ya nchi…huu ni upungufu mkubwa kwani msajili anaweza kukataa tu kutokana na maslahi yake bila kuongozwa na sheria inayopendekezwa,” amesema mbunge huyo.
Mdee ataja kinacho vunja katiba
Kwa upande wake Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee amesema baadhi ya vipengele vya muswada wa marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 2018 vinavunja Katiba.
Mdee amesema miongoni mwa kinachovunja Katiba ni kile kinachompa mamlaka msajili wa vyama vya siasa kukifuta chama ambacho kitashindwa kuwa na kumbukumbu za wanachama wake.
“Muswada huu unataka vyama vya siasa viweke rejista kila ngazi. Kuna wanachama wanaingia na wanatoka kila siku na kununuliwa kila leo. Sasa chama kitakuwa hakina kazi nyingine zaidi ya kuweka kumbukumbu,” amesema.
Amesema muswada huo unasema kuwa chama kitakacho shindwa kufanya hivyo msajili atakifuta lakini Katiba inasema mazingira ambayo inaweza kukinyima chama usajili ama kukifuta.
Mdee alipendekeza kifungu hicho cha 8 (C) kifungu kidogo cha 3 kifutwe kwa kuwa kinakwenda kinyume na Katiba.
Akinukuu ibara ya 13 ya Katiba inasema ni marufuku kufanya ubaguzi lakini baadhi ya vifungu vya muswada huo vinakwenda kinyume.
“Uvunjwaji wa Katiba si jambo dogo. Tunataka ufanye marekebisho utakapokuja hapa (Waziri katika ofisi ya waziri mkuu sera, bunge, vijana, kazi, ajira na watu wenye ulemavu, Jenista Mhagama)” amesema.
Mdee amesema kifungu kingine wanachokitaka kifutwe ni kinachohusu zuio la vikundi vya ulinzi: “Hakuna asiyefahamu kuwa vikosi vya ulinzi wakati wa uchaguzi vimekuwa vikifanya kazi ya CCM. Polisi wanalinda maboksi ya kura. Kusingekuwa na shida kama majeshi yangesimama katikati.”
Makamba asema msajili kapewa mamlaka makubwa mno
Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Salome Makamba amesema Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa mwaka 2018 ukipitishwa kuwa sheria, itawachinja walioitunga.
“Dua la kuku halimpati mwewe. Leo mnaitazama kesi ya CUF mnaitazama Chadema. Sheria itakuja kuwachinja walioitunga kwa kumpa mamlaka makubwa msajili ya kufuta vyama vya siasa,” amesema Salome akibainisha kuwa kazi ya Msajili wa vyama ni ulezi kwa vyama.