Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 09:55

Upinzani Tanzania watakiwa kutafuta ufumbuzi nje ya mahakama


Mahakama Kuu nchini Tanzania imetupilia mbali Shauri la kikatiba lililo funguliwa na vyama vya upinzani kupinga Muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa wa Mwaka 2018.

Kesi hiyo imefunguliwa na muungano wa vyama 10 vya upinzani vikidai unakiuka haki za Kikatiba za kisiasa, na inazifanya shughuli mbalimbali za harakati za kisiasa kuwa ni makosa ya jinai.

Akitoa uamuzi wa kesi hiyo Jumatatu Jaji Benhajj Masoud amekubaliana na mawakili wa serikali kuwa walalamikaji hawakupaswa kuomba Mahakama itamke kifungu cha 8(3) cha Sheria ya Haki za Msingi na Wajibu kinakiuka Katiba na kuomba mahakama itamke kuwa muswada huo unakiuka katiba.

Amesema shauri hilo linakiuka kifungu cha 8 (2) cha Sheria ya Haki za Msingi na Wajibu, kwani halikufuata utaratibu unaoelekezwa katika kifungu hicho.

Kifungu hicho kinaelekeza mtu yeyote anayedai haki zake zinakiuka kwanza ni lazima atafute ufumbuzi ulioko nje ya mahakama kabla ya kufungua shauri hilo.

Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi la Tanzania jopo la mawakili wa Serikali, likiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Mark Mulwambo lilieleza kuwa walalamikaji hawakukidhi matakwa ya kifungu hicho kwani hawakutumia njia mbadala zilizopo.

Walibainisha kwamba mlalamikaji wa kwanza, Zitto ni mbunge tena mzoefu ambaye anazijua Kanuni za Bunge zikiwemo za mwaka 2016 ambazo zinampa nafasi kushiriki kujadili muswada wowote na kutoa maoni na mapendekezo yake kwa uhuru na zinampa kinga.

Walidai kuwa pia kanuni hizo zinampa mamlaka ya kumuomba Spika aisimamishe kwa muda maalum upitishwaji wa muswada huo ili kumpa nafasi kuwasilisha maoni yake. Hata hivyo waliiambia mahakama kuwa walalamikaji hawakutumia utaratibu huo kabla ya kwenda mahakamani.

Vyama hivyo vinadai kuwa muswada huo unampa mamlaka makubwa Msajili wa Vyama vya Siasa kuingilia mambo ya ndani ya vyama hivyo. Muswada huo unampa haki msajili kuingilia uchaguzi wa viongozi na kusitisha uanachama kwa wanachama wa vyama hivyo.

Pia walikuwa wanapinga kifungu cha 8 (3) cha Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi kinachozuia muswada uliowasilishwa bungeni kupingwa mahakamani.

XS
SM
MD
LG