Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 04:44

Muswada wa Vyama Vya Siasa : Serikali yapewa siku 7 kuwasilisha utetezi


Viongozi wa vyama 10 vilivyo kutana Zanzibar.
Viongozi wa vyama 10 vilivyo kutana Zanzibar.

Mahakama Kuu nchini Tanzania imeipa siku saba serikali kuwasilisha utetezi wake katika kesi iliyo funguliwa na vyama 10 vya upinzani nchini Tanzania, kupinga muswada wa vyama vya siasa kujadiliwa bungeni kwani unapingana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Muda uliowekwa kisheria wa siku 14 hautatumika na hivyo serikali itatakiwa kupeleke utetezi wake ndani ya siku saba.

Kesi hiyo ambayo ilifunguliwa na Kiongozi wa Chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe na wenzake wawili, Joran Bashange na Salim Biman wa CUF kwa niaba ya vyama vya upinzani, dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Vyanzo vya habari vimeeleza kuwa uamuzi huo umetolewa Ijumaa mchana na kiongozi wa jopo la majaji watatu wanaosikiliza shauri hilo, Jaji Barke Sahel.

Ametoa uamuzi huo baada ya kukubaliana na maombi ya waliofunguwa shauri hilo la kupunguza muda wa serikali kuwasilisha utetezi wake kutoka siku 14 zinazo elekezwa kisheria.

Awali serikali kupitia kwa Mwanasheria wa Serikali, Mark Mulwambo iliomba kuongezewa muda kutoka siku 14 za kisheria mpaka siku 21 kwa madai ya kufanya mashauriano baina ya Serikali na taasisi zake nyingine.

Gazeti la Mwananchi limeripoti kuwa Jaji Sahel amesema mahakama haikushawishika na maombi ya Serikali ya kuongezewa muda kwa lengo la kushaurina.

“Kwa kuzingatia kwamba shauri hili limewasilishwa chini ya hati ya dharura na kwa kuwa lina maslahi kwa umma na kwa kuzingatia kwamba muswada huu umepangwa kusomwa bungeni kwa mara ya pili Januari 15, 2019 mahakama inatoa amri zifuatazo,” amesema.

“Mujibu maombi atawasilisha majibu yake akiambatanisha na hati ya kiapo ndani ya siku saba tangu siku ya kupewa nyaraka za shauri hili, yaani atawasilisha utetezi wake kabla au Januari 9, 2019. Usikilizwaji wa shauri hili utafanyika Januari 11 saa 3 asubuhi.

Katika shauri hilo la Kikatiba namba 31 la mwaka 2018, waombaji wanapinga kifungu cha 8 (3) cha Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi kinachoeleza kuwa muswada wowote hauwezi kupingwa mahakamani.

Zitto na wenzake wanapinga muswada huo pamoja na mambo mengine wakidai kuwa unakiuka haki za kisiasa za binadamu kwa kuwa unaharamisha shughuli za kisiasa na kumpa mamlaka makubwa Msajili wa Vyama vya Siasa kuingilia mambo ya ndani ya vyama vya siasa, yakiwemo ya uongozi.

XS
SM
MD
LG