Washtakiwa Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko, walifutiwa dhamana yao na wanaendelea kukaa rumande.
Akiwasilisha hoja yake Ijumaa, Wakili wa Serikali, Paul Kadushi, aliieleza mahakama kuwa kwa vile shauri limesitishwa mpaka rufani iliyokatwa itakaposikilizwa, aliiomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya kutajwa, limeripoti gazeti la Nipashe nchini Tanzania.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu Bara na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Katibu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji, Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche.
Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, yakiwamo ya kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari 1 na 16, 2018, Dar es Salaam.
Mara baada ya hoja hiyo kuwasilishwa, Profesa Safari alihoji rufani iliyo wasilishwa na upande wa mashtaka katika Mahakama ya Rufani kama ina hati ya dharura na kama hakuna itolewe sababu.
Kadushi alidai kuwa rufani iliyopo ni dhidi ya Mahakama Kuu na si Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na upande wa utetezi hauna uhalali wa kuhoji na endapo Mahakama Kuu itatoa amri, wataeleza.
Baada ya maelezo hayo, Prof. Safari alitaka kujua kama rufani hiyo iliwasilishwa chini ya hati ya dharura na kama upande wa serikali hawajui wawe wawazi kusema na kama wanajua pia wanapaswa kueleza.
Wakili Kadushi akijibu hoja hiyo, alidai kilichowasilishwa na upande wa utetezi wa kutaka waeleze waliwasilisha rufani hiyo chini ya hati ya dharura, si halali kisheria kwa kuwa hakuna kifungu cha sheria kinachowapa uhalali wa kuhoji hayo.
Baada ya maelezo hayo, Hakimu Mashauri, aliwataka mawakili wa utetezi kwenda kuhoji jambo hilo katika Mahakama ya Rufani kwa kuwa ndipo rufani ilipokatwa.
Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 17, mwaka 2019.