Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 17:44

Burundi yafunga ofisi ya Umoja wa Mataifa


Ravina Shamdasani
Ravina Shamdasani

Serikali ya Burundi imefunga ofisi ya Umoja wa Mataifa iliokuwa inafuatilia masuala ya haki za binadamu katika nchi hiyo.

Msemaji wa baraza la haki za binadamu la UN mjini Geneva, Ravina Shamdasani ameliambia shirika la habari la Associated Press (AP), kwamba Jumatano walipata barua kutoka serikali ya Burundi, ikiwaamrisha kufunga ofisi zao mjini Bujumbura.

Shamdasani amesema “tunasikitishwa na uamzi huu sababu tulikuwa tunapendelea kuendeleza ushirikiano na Burundi.”

Wanaharakati wa haki za binadamu nchini Burundi, wameelezea masikitiko yao kutokana na hatua hiyo ya serikali na wanahofia kwamba hali ya uvunjaji wa haki za binadamu itazidi kuongezeka katika nchi hiyo ya Afrika ya Mashariki.

“Tunahisi kuwa serikali imechukua uamzi huo ili kusiwepo shahidi yeyote wa kuripoti matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini,” amesema wakili Dieudonne Bashirahishize nchini Burundi.

Ametowa wito kwa Umoja wa Afrika (AU) na UN kuendelea kufuatilia suala la haki za binadamu nchini Burundi na kuchukua hatua zinazo stahiki dhidi ya wanao jihusisha na vitendo vya uvunjaji wa haki za binadamu.

Serikali ya Burundi haijatowa maelezo katika barua hiyo sababu za uamzi huo wa kufunga ofisi hiyo ya UN.

Uhusiano kati ya Burundi na baraza la umoja wa mataifa la haki za binadamu ulikuwa sio mzuri tangu nchi hiyo ilipoingia katika mgogoro wa kisiasa hapo mwaka wa 2015.

Baraza hilo liliteuwa timu ya wachunguzi wa kimataifa ambao wamekuwa wakifuatilia vitendo vya mauaji na uhalifu mwengine vinavyoripotiwa nchini Burundi.

Wachunguzi hao wa UN wamekuwa wakitoa ripoti ambazo zinai washutumu viongozi wa Burundi kuchochea mauaji na mateso dhidi ya wapinzani.

Serikali ya Burundi ilipinga vikali ripoti hizo na kuzitaja kuwa za uzushi na uongo. Pia imekuwa ikitishia kujiondowa kwenye baraza la UN la haki za binadamu kama mwanachama wa baraza hilo, ikidai kuwa ripoti za baraza hilo zinaegemea na zinalenga kuwapaka matope viongozi wa Burundi.

Mwezi Oktoba mwaka wa 2016, Burundi ilijiondowa kwenye mkataba wa ushirikiano na mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC, ikisema pia kwamba mahakama hiyo inaegemea.

XS
SM
MD
LG