Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 22:15

Ofisi ya Mkapa : Mazungumzo ya amani ya Burundi hayakuahirishwa


Wakimbizi wa Burundi wakiwa katika kambi za wakimbizi Tanzania
Wakimbizi wa Burundi wakiwa katika kambi za wakimbizi Tanzania

Mshauri wa msuluhishi katika mgogoro wa Burundi, Balozi David Kapya amesema, kikao cha mazungumzo ya kutafuta amani nchini Burundi, kitazinduliwa Alhamisi mjini Arusha, licha ya kutokuwepo wawakilishi wa serikali ya Burundi.

Mazungumzo yaliyo kuwa yafunguliwe Jumatano mjini Arusha, yanaendeshwa chini ya upatanishi wa Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin William Mkapa.

“ Hadi sasa, serikali haijajibu rasmi mualiko huo. Msuluhishi tayari ameshakutana na wawakilishi wa upinzani walioko ndani na nje ya Burundi, Marais wa zamani wa Burundi na wanasiasa waliofika hapa pamoja na wajumbe maalumu wa kimataifa wanaofuatilia suala la Burundi,” amesema Kapya.

“Na kesho, atazinduwa mazungumzo na wale waliohudhuriya, mazungumzo yataendelea hadi tarehe 30 Oktoba,” Kapya anasema, akiongeza kuwa lengo la msluhishi katika kikao hiki ni kusaini makubaliano ya pamoja na walioshiriki.

Tamko la Serikali

Kwa upande wa Serikali ya Burundi taarifa iliotolewa na msemaji wa serikali Prosper Ntahogwamiye kwa vyombo vya habari vya Burundi, imesema "tulituma taarifa kwa msuluhishi tukimuomba kuahirisha kikao sababu kati ya tarehe 13 na tarehe 21 Oktoba, Burundi inafanya maambolezo ya mashuja wa utetezi wa uhuru na demokrasiya.”

Hata chama tawala CNDD-FDD kimefahamisha kwamba hakitohudhuriya kikao ambacho kilikua kimepangwa kufanyika tangu tarehe 24 oktoba hadi tarehe 29 oktoba, kikiomba kabla ya yote, serekali ya Burundi na timu ya usuluhishi waafikiane kuhusu wajumbe watakaoshiriki mazungumzo hayo ya mjini Arusha.

Hoja ya Upinzani

Lakini upande wa upinzani, wanaona kwamba hoja hizo za serekali na chama tawala hazina msingi. Chauvineau Mugwengezo, mwenyekiti wa chama cha UPD ambaye anahudhuria kikao na wenzake kutoka kambi ya upinzani iliyo uhamishoni, anasema wataendelea kushiriki na kujadili na wasuluhishi kuhusu njia bora ya kutanzua mgogoro wa Burundi uliozuka April 2015.

Hii inafuatia hatua ya Rais Pierre Nkurunziza kuamua kuwania muhula wa tatu, hatua iliopingwa na wapinzani walioitisha maandamano makubwa, wakisema Nkurunziza alikiuka katiba ya nchi ambayo hairuhusu Rais kuwaniya mihula zaidi ya miwili.

Mzozo wa Burundi ulisababisha vifo vya mamia ya watu, na wengine zaidi ya laki nne kukimbilia katika nchi jirani, wengi wao wakiwa Tanzania.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Patrick Nduwimana, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG