Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 10:01

Magufuli, Museveni waishukia ICC


Rais John Magufuli (wapili kushoto) akiutambulisha ujumbe aliofautana nao kwa Rais Museveni (kushoto) wakati wa ziara yake nchini Uganda.
Rais John Magufuli (wapili kushoto) akiutambulisha ujumbe aliofautana nao kwa Rais Museveni (kushoto) wakati wa ziara yake nchini Uganda.

Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) imekosolewa na viongozi wawili wa Afrika Mashariki, kwamba kitendo cha kuanzisha uchunguzi dhidi ya Burundi bila ya kuwashirikisha viongozi wa Jumuiya hiyo hakikubaliki.

Rais John Magufuli wa Tanzania amesema hatua hiyo inarudisha nyuma hatua zilizochukuliwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Jumuiya hiyo tayari iliunda kamati ya usuluhishi wa mgogoro wa Burundi inayoongozwa na Rais Yoweri Museveni wa Uganda na Rais Mstaafu wa awamu ya tatu wa Tanzania Benjamin Mkapa.

“Hali ya Burundi si mbaya kama inavyotangazwa kwa kuwa tayari wakimbizi wengi waliokuwa Tanzania wamerejea Burundi na wengine wanaendelea kurejea, na pia viongozi wanaosuluhisha mgogoro huo wamepanga kukutana Novemba 23, mwaka huu kwa lengo la kuendeleza mchakato wa kutatua mgogoro huo,” alisema Magufuli.

Kwa upande wake Rais Museveni wa Uganda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) amedai kuwa ICC inaingilia mambo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki bila kuwahusisha viongozi wa Jumuiya hiyo jambo ambalo si sahihi na linarudisha nyuma juhudi za kutafuta amani ya Burundi.

Majaji wa ICC walitoa uamuzi huo Novemba, 9 2017, na kumtaka Mwendesha Mashtaka wa Mahakama hiyo kuchunguza vitendo vya kihalifu dhidi binadamu vilivyotokea nchini Burundi tangu ulipozuka mgogoro nchini humo miaka miwili iliyopita.

Vyanzo vya habari nchini Uganda vimeripoti kuwa Mahakama ya ICC ilisema muda mfupi baada ya Burundi kuamua kujitoa katika taasisi hiyo, itachunguza madai ya kukiukwa kwa haki za binadamu katika nchi hiyo.

Taasisi moja ya Mahakama ya ICC ndiyo iliyotoa amri ya kufanyika kwa uchunguzi huo katika mji wa The Hague nchini Uholanzi ikidai kuwepo kwa madai ya mauaji, mateso, ubakaji na matukio mengine ya uhalifu.

Kwa mujibu wa Mahakama hiyo madai yatakayochunguzwa ni ya uhalifu uliotokea kati ya mwaka 2015 na 2017 ambapo Burundi ilikuwa mwanachama wa ICC. Uamuzi huo, kwa mujibu wa ICC ulipitishwa kabla ya Burundi kuamua kujitenga na Mahakama hiyo ya kimataifa.

Taarifa hiyo imesema uamuzi huo uliwekwa siri kwa sababu ya kuhakikisha usalama wa waathirika na mashahidi, hatua ambayo hata hivyo imetia shaka juu ya ukweli wa madai hayo ya Mahakama ya ICC.

Hata hivyo serikali ya Burundi hivi karibuni ilisema haitaruhusu uchunguzi huo ufanywe kama ICC inavyoshinikiza.

Rais Magufuli alikuwa katika ziara ya kiserikali nchini Uganda ambapo amekubaliana na Rais Museveni kuongeza wigo wa kibiashara na pia ushirikiano katika nyanja za ulinzi na habari baina ya nchi hizo mbili.

XS
SM
MD
LG