Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 16:30

Tanzania, Uganda zaongeza ushirikiano kibiashara, ulinzi na utangazaji


Rais Magufuli na Rais Museveni
Rais Magufuli na Rais Museveni

Tanzania na Uganda zimekubaliana kuongeza biashara ili kupata manufaa katika ushirikiano uliopo hivi sasa.

Rais John Magufuli wa Tanzania na mwenzake Rais Yoweri Museveni wa Uganda wamewaagiza mawaziri wao kuongeza wigo wa kibiashara na ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.

Hapo awali viongozi hao walishuhudia utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano kati ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na Shirika la Utangazaji la Uganda (UBC) na makubaliano kati ya Jeshi la Polisi la Tanzania na Jeshi la Polisi la Uganda. Rais Magufuli anazuru Uganda kwa ziara ya kikazi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu ya Tanzania biashara kati ya Tanzania na Uganda imefikia takriban Sh bilioni 200 kwa mwaka, kiasi ambacho ni kidogo ikilinganishwa na fursa zilizopo, uhusiano na ushirikiano wa kidugu uliojengwa tangu enzi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Nchi hizo mbili zimekubaliana kuangalia vikwazo vyote vinavyosababisha biashara kufanyika kwa kiasi kidogo, na jopo la wataalam kutoka pande mbili watapendekeza nini kifanyike. Pia zinataka kuona biashara ya Tanzania na Uganda inakua.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo hivi sasa Uganda imewekeza Dola za Marekani milioni 47 tu nchini Tanzania na kuzalisha ajira 146,000, Uganda imesema inahitaji kununua gesi ya Tanzania kwa ajili ya viwanda vyake vya mbolea na chuma na pia kurudisha historia ya kuwa mnunuzi mkubwa wa bidhaa kutoka hapa.

Tanzania tayari imechukua hatua ikianza na ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (standard gauge) kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, yenye umbali wa kilomita 726, lakini Serikali pia imekarabati reli iliyopo.

Hatua nyingine ni ya ukarabati wa kivuko cha mabehewa ya treni cha Umoja katika Ziwa Victoria, ili kuwezesha mizigo ya kutoka Bandari ya Dar es Salaam kufika Kampala kwa gharama nafuu, huku ikiendelea kujenga na kuimarisha barabara za mpakani.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa Uganda sasa itajenga kipande cha kilomita 11 za reli kutoka Portbell hadi Kampala, na Tanzania itaweka bandari kavu pale Mwanza ili wafanyabiashara wa Uganda wasisumbuke kwenda hadi Dar es Salaam, mizigo yao wataipata Mwanza, ikiwa ni njia ya uhakika na nafuu ya kusafirisha mizigo.

Pia Tanzania imejipanga kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano wake na Uganda kwa kuhakikisha miradi mbalimbali inakwenda vizuri, ukiwamo kituo cha pamoja cha huduma za mpakani (One Stop Border Post –OSBP) na mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga.

XS
SM
MD
LG