Amnesty International
Kanda nzima ya Afrika Mashariki imeshuhudia sheria dhidi ya ugaidi na tishio la usalama wa taifa mara kadhaa vikitumika kukabili vyombo vya habari na kushamiri kwa kuvibana vyombo hivyo, anasema Mwakilishi wa kikanda wa shirika la kutetea haki za binadamu - Amnesty International Joan Nyanyuki, .
“Ukiangalia Kenya, Tanzania, Rwanda, na Burundi mpaka miaka mitatu ama minne iliyopita maudhuwi yao yalikuwa ya uhuru sana. Unajua kila mtu Afrika Magharibi alikuwa akiambiwa kwamba kwa nini msiige mfano wa wenzenu wa Afrika Mashariki, lakini kwa sasa mawazo hayo yameondoka sasa vichwani mwetu. Na sasa mataifa ya Magharibi yanapaswa kuacha kushangilia na kuanza kujiuliza maswali magumu,” ameeleza Nyanyuki.
Sheria kandamizi
Vyombo vya habari vya ukanda huo vinarudishwa nyuma na masuala ya kisheria na msukumo wa serekali. Kufungwa kwa vyombo vinne binafsi mwaka huu nchini Kenya kumezua ukosoaji mkubwa.
Akizungumzia hali hiyo Nyanyuki anasema: “Raia wanapaswa kusimama na kumiliki uhuru wa vyombo vya habari kama moja ya vitu vitakavyowalinda na kuwawezesha kwenda mbali katika maendeleo na ulinzi na usimamizi wa haki zao wenyewe. Kwa hiyo uhuru wa vyombo vya habari hakina ni wa kila raia wa kawaida katika ukanda.”
Watu wanaanza kuamka kuhusu umuhimu wa suala hili, anasema Nyanyuki, kwa hiyo kuna ari ya kukabiliana na hali hiyo.
Tanzania
Wakati huohuo nchini Tanzania vyombo vya habari ambavyo vimekuwa vikikosoa serikali vilifungiwa.
“Kuna baadhi ya magazeti yamefungiwa. Baadhi yao miaka mitatu. Na baadhi yao kwa miezi kadhaa. Na mengine yamefungiwa kabisa,” anasema mkuu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Tanzania, Hellen Kijo Bisimba.
Uganda
Nchini Uganda, mtandao wa haki za binadamu kwa wanahabari umekusanya video za polisi wakishambulia wanahabari. Kundi hilo la haki za binadamu linasema polisi walikuwa wakiukaji wakubwa wa uhuru wa vyombo vya habari kwa mwaka 2017.
“Polisi imelaumiwa vibaya sana kwa sababu ilihusika katika kesi 83 za ukatili kati ya 113, ikiwa ni sawa na asilimia 73,” anaeleza Robert Ssempala wa mtandao wa kusimamia haki za binadamu za waandishi wa habari nchini Uganda.
Akijibu hoja hizo msemaji wa polisi wa Uganda Emilian Kayima amekanusha kwamba polisi walihusika katika kushambulia vyombo vya habari.
Anasema: “Tumewapeleka mahakamani, tumechunguza kesi zote. Mahakama imewakuta na hatia, imewakamata na wameachiwa na hiyo inaonyesha polisi inavyotekeleza wajibu wake.”
Eritrea na Sudan
Wakati huohuo Mataifa ya Eritrea na Sudan yameshuhudia uhuru huo kuzorota kabisa na kufikia karibu na mwisho wa orodha ya mataifa yenye uhuru wa vyombo vya habari.
Hali kadhalika wanaharakati wanasema wameshuhudia kushuka kwa kiwango kikubwa cha uhuru huo katika nchi za Kenya na Tanzania.
Ethiopia
Mwandishi wa VOA anaripoti kuwa maafisa wa usalama, Ethiopia, walimkamata mwandishi wa habari Eskinder Nega kwa mara tisa kwa shutma ambazo zinajumuisha uhaini, ugaidi na mauaji ya halaiki.
Lakini Nega ambaye ni raia wa Ethiopia anasema licha ya kukabiliwa na shutma hizo hatoacha kabisa kuandika na kuikosoa serikali.
“Bila ya kuwa na uhuru wa kujieleza, uhuru hauwezekani. Unaanzia hapo. Unapaswa kuwa na nafasi ya kujieleza,” amesisitiza.
Nega ambaye aliachiliwa huru mara ya mwisho April 5, 2018 siku chache baada ya kuteuliwa Waziri Mkuu mpya Abiy Ahmed, anasema wanamatumiani kiongozi huyo mpya ataleta mabadiliko kama alivyo ahidi.