Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 15:17

Kushambuliwa Lissu kwaibua mjadala wa demokrasia Tanzania


Tundu Lissu akiongea na wafuasi wa chama chake.
Tundu Lissu akiongea na wafuasi wa chama chake.

Kiongozi wa kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe anasema hali ya demokrasia imetetereka sana nchini Tanzania baada ya utawala wa awamu ya tano wa Rais John Pombe Magufuli kuingia madarakani.

Akizungumza na Sauti ya Amerika akiwa mjini Nairobi kiongozi wa chama cha CHADEMA, Freeman Mbowe amesema, tangu kuingia madarakani Rais Magufuli amepiga marufuku shughuli za siasa, ikiwemo kuzuiwa maandamano nchini, kupigwa marufuku kwa mikutano ya ya hadhara ya vyama vya siasa, na kukatazwa kuonyeshwa vipindi vya bunge mubashara, ili serikali iweze kudhibiti habari.

Amesema kuwa sheria ya vyombo vya habari ilibadilishwa, sheria za mitandao zilianzishwa na kuanza kuwekewa nguvu kubwa. Kwa kweli uhuru wa kupata habari na kupewa habari ulianza kudhibitiwa.

Akiwa Nairobi ambako alifuatana na Lissu kwa ajili ya kupata matibabu Mbowe, amesema.

"Walianza kuwadhibiti wanasiasa wenyewe na kuwabamikia kesi mbalimbali, wengine kuharibiwa biashara zao, kufungwa na wengine kupotea bila ya kuwa na maelezo sahihi kutoka vyombo vya dola," ameeleza Mbowe.

“Wanakamata wabunge wa upinzani wanawapiga, wanawabughudi, wanawafunga. Pamoja na kujengwa misingi mizuri ya demokrasia imeporomoshwa mara moja,” amesema Mbowe.

Ameongeza kusema kuwa kuna kila viashiria kwamba jambo hili kuna watu wanalitambua katika vyombo vya ulinzi na usalama.

“Hatuwezi kuamini hili ni tukio la ujambazi. Kama lingekuwa tukio la ujambazi wangebeba kila kitu. Tukio liliotokea watu waliojitokeza na silaha walikuwa wanajiamini, wakiwa na silaha ya SMG, silaha ya kivita, silaha ya moto. Wamefanya mashambulizi wakati wa mchana, hakuna majambazi wanaokwenda katika tukio kwa namna hiyo,” alieleza Mbowe akiwa nchini Kenya.

“Sasa tunaitaka serikali itusaidie au iseme ni nani hao waliofanya tukio hilo. Kwa sababu huenda wanawafahamu na kama hawawafahamu wana vyombo vya kuwafahamu,” alisisitiza.

“Dodoma ni mji mkuu wa Tanzania ina vyombo vyote vya ulinzi na usalama. Lakini hata baada ya mashambulizi ya Lissu ilichukuwa masaa mawili kwa polisi kufika kwenye eneo la tukio hilo. Polisi walikuwa wapi hilo ni eneo wanaishi viongozi mbali mbali akiwemo Spika wa Bunge, sasa suala la kujiuliza,” amesema.

Hali ya Lissu bado ni tata lakini inaendelea kuimarika. Madaktari kwa kweli wanamshughulikia sana, tangu alipokuwa Dodoma hadi hapa Nairobi, ameeleza Mbowe.

“Tumepata ushirikiano mkubwa. Madaktari bado wanamchunguza vitu vingi, lakini bado hatujapata ripoti kamili ya madaktari hivyo sitoweza kutoa kauli juu ya hali yake ya matibabu,” amesema.

Mbowe amesema : “Hatukutegemea rais atoe kauli vyombo vianze uchunguzi tangu tokeo hilo vyombo vilistahili kuwa vinafanya uchunguzi. Na kunamatokeo mengi ya watu kuumizwa, watu kupotea, watu kutekwa nyara na tumelalamika na rais alikuwa kimya pengine leo ameamua kutoa kauli baada ya kuona uzito wa jambo hili kufanyika.”

“Sisi tunachosubiri ni wao waeleze nini kimetokea, nini kimempata mheshimiwa Lissu na kwa nini kimempata mheshimiwa Lissu.”

Rais kutoa kauli ni jambo jema lakini, kwetu sisi halitusaidii tunataka kujua wahusika ni kina nani. Sidhani katika matukio kama haya vyombo vya usalama vinatakiwa vingojee kauli ya rais. Vinatakiwa vianze kuchukua hatua mara moja, amedadisi Mbowe.

XS
SM
MD
LG