Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 04:17

Waandishi wa Tanzania wamchachamalia Waziri Mwakyembe


Waziri Harrison Mwakyembe
Waziri Harrison Mwakyembe

Kulikuwa na mvutano mkali kati ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na waandishi wa habari Jumatatu, baada ya msanii Roma Mkatoliki kuelezea mateso na vipigo waliovipata chini ya watekaji wao.

Washabiki wa muziki na watanzania kwa ujumla wameshtushwa na madhila na vitisho alivyokumbana navyo msanii na wenzie baada ya kuonesha majeraha na maumivu makali yaliyowapata.

Moja ya masuala yaliosababisha mvutano kati ya waziri na waandishi ni hoja iliyokuwa imetolewa bungeni na wabunge wawili ikidai kuwa hali ni mbaya sana kwani watu wamendelea kutekwa na kumtaka Naibu Spika wa Bunge kuahirisha.

Wabunge wawili walioomba kuwa shughuli za bunge ziahirishwe ilikujadili suala la dharura ambalo limehusisha watu kutekwa nyara.

“Naomba mheshimiwa naibu spika tulijadili suala hili kama bunge na ikikupendeza bunge hili liunde kamati maalumu yakuweza kuchunguza jambo hili linaloendelea katika nchi yetu,” amesema Hussein Bashe.

Chanzo cha mzozo

Hata hivyo mzozo huo ulianza pale Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alipokataa kujibu swali ambalo lilikuwa tayari limeongelewa bungeni akisema kuwa mimi siwezi kujibu.

“Unauliza masuala ya kina Bashe mimi hapa Mwakyembe, mimi siwezi kujibu, mnataka niseme nini, mnataka niseme mimi mambo ya Bashe yako Bungeni, Nape alisema hivi alisema hivi. Mimi hapa nashughulikia suala la huyu kijana, wameumizwa hawa watu, subiri upelelezi ukamilike, sawa, sio kama kupiga ramli. Nendeni Bagamoyo kuna ramli nzuri,” alisema kwa ukali.

Suala jingine lililoleta utata na mabishano ni kutaka kujua Waziri atachukua hatua gani iwapo itabainika kuwa vyombo vya dola ndio viliwateka.

Majibu ya Waziri

Waziri alijibu kwa kusema “yaani wewe unaamini hivyo.Wengine mnalipuka kufanya fujo kama watoto wadogo. Vyombo vya dola vikibainika, atabaini nani, tuacheni tupate fursa ya kupeleleza tujue kimetokea kitu gani,” alihoji Dr Mwakyembe.

Dr Mwakyembe pia alitetea kauli ya Mkuu wa Mkoa kwa wananchi kwamba “Nawapa imani tu mpaka ikifika Jumapili tutakuwa tumewapata watu wote wanne, na mimi naomba kwa dini zetu na Imani zetu popote pale alipo aombe. Tutahakikisha ndugu zetu hawa tunawarejesha wakiwa salama.

Waziri aliomba kusikiliza kauli hiyo tena na ndipo aliposema kuwa hakuona jambo lolote baya katika kauli ya mkuu wa mkoa, akisisitiza kuwa huyu ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa, anasema tuna nguvu ya kutosha ya kudhibiti aina yoyote ya matukio kama hayo. Mnyonge mnyongeni haki yake mpeni.

“Jamani hebu tusikilizeni vizuri waandishi wetu wa Tanzania masuala ya kupiga ramli sio mazuri sana…” aliwanasihi waandishi.

Waandishi waomba awape imani

Waandishi walitaka waziri awape Imani yake kuhusu jambo hili litachukua muda gani.

Waziri Mwakyembe amesema: “Mimi nashukuru kijana wangu (mwandishi). Mimi nimeacha kazi zote nimekuja hapa. Mimi nilikuwa nasumbuliwa kuna nini nilikuwa nasumbuliwa kuna nini kimetokea kuhusu hawa vijana. Kama nilivyo kwisha sema mimi nimeshatoa jibu.”

Aliongeza kuwa: “Kama kuna kitu chochote kinamhusu msanii natakiwa mimi nitaarifiwe kwanza, nataka kujenga mahusiano mapya katika jamii na wasanii katika nchi hii.”

Waziri Mwakyembe aliahidi kuwa kama kuna makosa makubwa tutachukua hatua, lakini kama ni makosa ya tafsiri, kwa kweli itabidi tujadiliane.

“Nimeshasema mara nyingi sana wasanii wetu wote wana haki ya kujieleza wana uhuru. Mimi nilisema zaidi ya mara tano wiki iliopita,” amesema waziri huyo.

Maelezo ya Roma Mkatoliki

Kabla ya hapo msanii Roma Mkatoliki alizungumza na waandishi na kusema: “Tulitekwa siku ya Jumatano na kufungwa pingu na kitambaa usoni na baadaye kusafirishwa hadi eneo tusilolijua,” amesema msanii huyo.

Akionekana mwenye hisia na machungu Roma amesema kuwa walipofikishwa walipopelekwa walipata mateso mengi kwa kupigwa hadi siku ya Ijumaa usiku.

Roma Mkatoliki: “Tulitolewa tulimokuwepo siku ya ijumaa jioni na kufungwa uso, na mikono na miguu. Tukapelekwa sehemu tukatupwa kwenye dimbwi la maji karibu na baharini.”

Roma amesema kuwa alipata fahamu na kuweza kuwafungua wenzake na kutembea mwendo mrefu ambapo walifika katika maeneo ya Ununio.”

Hata hivyo msanii huyo hakuweza kueleza baadhi ya maswali alioulizwa kuhusu mahojiano na waliowateka huku akisema kwamba tayari wamewasilisha malalmishi yao kwa polisi kwa ajili ya uchunguzi.

Mahojiano yagonga ukuta

Mahojiano hayo yaligonga ukuta wakati maafisa wa serikali walioandaa mazungumzo hayo wakionekana kumzuia msanii huyo kutoa maelezo zaidi kuhusu mateso aliopata.

Roma na wenzake tayari mwanzoni kabla ya kuanza mkutano walionyesha baadhi ya majeraha waliyopata chini ya watu waliowateka.

Wameitaka serikali kuwahakikishia usalama wao wakidai kwamba licha ya kuwepo katika eneo lililozungukwa na watu maarufu ikiwemo serikalini watekaji wao walifanikiwa kutekeleza tendo hilo bila wasiwasi.

XS
SM
MD
LG