Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 17:44

Majeshi ya Ukraine yaudhibiti tena mji wa Lyman, kituo kikuu cha usafirishaji


Mwanajeshi wa Ukraine akiondoa bendera ya Jamhuri ya Donetsk huko Lyman.
Mwanajeshi wa Ukraine akiondoa bendera ya Jamhuri ya Donetsk huko Lyman.

Ukraine ilisema Jumapili ina udhibiti kamili wa mji wa Lyman, kituo cha usafirishaji cha mashariki ambacho kilikuwa ni sehemu ya eneo lililochukuliwa na kutangazwa na Rais wa Russia Vladimir Putini wiki iliyopita kuwa ni eneo lake kinyume cha sheria.

“Lyman hivi sasa imekombolewa kikamilifu,” Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy alitangaza katika ujumbe mfupi wa kanda ya video katika mtandao wake wa Telegram.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy

Russia haikutoa kauli yoyote Jumapili juu ya hatma ya Lyman lakini ilisema siku ya Jumamosi kuwa majeshi yake yaliondoka kutoka katika eneo hilo kwa sababu walihofia majeshi ya Ukraine yalikuwa yamekaribia kuwazingira.

Russia iliukamata mji wa Lyman mwezi Mei na waliutumia kama kituo cha usafirishaji na mipango kwa ajili ya operesheni zake huko kaskazini mwa mkoa wa Donetsk.

Russia kuupoteza mji wa Lyman ilikuwa ni kushindwa vibaya katika vita yake tangu majeshi ya Ukraine mwezi uliopita kuuchukua mkoa wa Kharkiv kaskazini mashariki mwa Ukraine, na kuyasukuma majeshi ya Russia kurudi mpakani kwao.

Serhiy Haidai, gavana wa mkoa wa Luhansk uliojirani na Donetsk, alisema kuchukuliwa Lyman kunaweza kuwa ni msaada kwa Ukraine kuendelea kuyarejesha maeneo iliyopoteza katika mkoa wake, ambayo Moscow ilitangaza mapema mwezi Julai imeyateka.

Rais wa Russia Vladimir Putin akihutubia kupitia luninga katika uwanja wa Red Square, huku watu wamekusanyika katika maadhimisho ya kuingizwa mikoa ya Ukraine katika himaya ya Russia, huko Moscow Sept. 30, 2022.
Rais wa Russia Vladimir Putin akihutubia kupitia luninga katika uwanja wa Red Square, huku watu wamekusanyika katika maadhimisho ya kuingizwa mikoa ya Ukraine katika himaya ya Russia, huko Moscow Sept. 30, 2022.

Hatua ya Ukraine kuukamata tena mji wa Lyman imekuja kwa haraka licha ya Putin kutangaza, katika sherehe kubwa huko Kremlin Ijumaa, kuwa serikali yake ilikuwa inatangaza kujiingiza kimabavu katika mikoa minne ya Ukraine, ikiwa ni moja ya tano ya eneo la ardhi ya jirani yake, nchi huru tangu mwaka 1991 ambayo iliwahi kuwa sehemu ya Umoja wa Sovieti..

Hatua hiyo ya Putin ilikuwa kinyume cha sheria za kimataifa na ililaaniwa kwa kiasi kikubwa na Ukraine, Marekani na washirika wa Magharibi ambao wamekuwa wakiipatia silaha serikali ya Kyiv katika mwezi wake wa saba wa mapambano dhidi y uvamizi wa Moscow.

Wizara ya Ulinzi ya Uingereza imesema katika ripoti ya upelelezi iliyobandikwa katika Twitter Jumapili kuwa majeshi ya Russia yaliondoka Jumamosi katika maeneo muhimu ya mashariki mwa Ukraine.

Maeneo hayo yaliyopo katika mji wa Lyman kwenye mkoa wa Donetsk “kuna uwezekano (majeshi hayo) yalikumbwa na maafa makubwa wakati yakiondoka katika njia pekee nje ya mji huo ambao bado uko mikononi mwa Russia.”

Taarifa mpya pia zilisema: “Kuondoka kwao kumepelekea wimbi la ukosoaji zaidi wa umma kwa uongozi wa jeshi la Russia kutoka kwa maafisa waandamizi… Kadhalika kupoteza ardhi zaidi katika maeneo yanayokaliwa kimabavu kinyume cha sheria na bila shaka itaongeza ukosoaji wa umma na shinikizo zaidi kwa makamanda waandamizi.”

Hatua ya Ukraine kuukamata tena mji wa Lyman kumesababisha wanajeshi wa Russia kukimbia siku moja baada ya Moscow kuingia katika mkoa huo, pamoja na maeneo mengine matatu upande wa mashariki na kusini mashariki mwa Ukraine.

Wanajeshi wa Ukrainian wakiwa katika mji wa Lyman waliouteka.
Wanajeshi wa Ukrainian wakiwa katika mji wa Lyman waliouteka.

Kanda ya video iliyobandikwa katika mitandao ya kijamii Jumamosi iliwaonyesha wanajeshi wa Ukraine wakiwa nje ya mji huo wakipeperusha bendera, huku mwanajeshi mmoja akisema, “Lyman itakuwa ya Ukraine.” Mji huo, ulioko katika kingo za Mto Siversky Donets, ulitekwa na Russia mwezi Mei. Tangu wakati huo, kituo chake cha njia ya reli kimetumiwa na Russia kama eneo muhimu la usafirishaji kuwasaidia maelfu ya wanajeshi wake wanaopigana katika mkoa wa Donetsk mashariki mwa Ukraine.

Wakati huo huo, maafisa wa Ukraine walisema majeshi ya Russia yamewaua takriban watu 20, ikiwemo watoto kumi, katika shambulizi kwa msafara uliokuwa umewabeba watu wanaokimbia kutoka kaskazini mashariki mwa Ukraine. Ripoti haikuweza kuthibitishwa na vyanzo huru.

Shambulizi lililoripotiwa linafuatia kombora lililopigwa kwa msafara mwingine wa raia huko jimbo la Zaporizhzhia Ijumaa ambapo watu 30 waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Wizara ya Ulinzi ya Uingereza ilisema Jumamosi kuwa kombora lililotumika katika shambulizi la Ijumaa “inawezekana ni kombora la ulinzi wa anga la masafa marefu limetumiwa kwa shambulizi la ardhini.”

Wizara imesema katika ripoti ya upelelezi iliyobandikwa katika Twitter kuwa matumizi ya silaha “yenye thamani kubwa” katika shambulizi la ardhini karibu na Zaporizhzhia “ bila shaka linatokana na msukumo wa uhaba wa silaha, hususan makombora yenye shabaha ya masafa marefu.”

Baadhi ya taarifa katika habari hii inatokana na mashirika ya habari ya AP, AFP na Reuters

XS
SM
MD
LG