Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 23:29

Ukraine yazihimiza nchi zinazoiunga mkono kuifahamisha Russia kile itakachopoteza


Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa njia ya video, Sept. 27, 2022, Makao Makuu ya U.N.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa njia ya video, Sept. 27, 2022, Makao Makuu ya U.N.

Ukraine imezihimiza nchi zinazoiunga mkono kuweka wazi kwa Russia kuwa “majaribio yake ya kuikalia kwa mabavu, kuhadaa watu na kutoa vitisho” itasababisha Ukraine kupata uungwaji mkono zaidi katika vita hivi viliyoanza kwa majeshi ya Russia kuvamia Ukraine mwezi Februari.

Katika taarifa yake Jumatano, wizara ya mambo ya nje ya Ukraine imesema “Ukraine imetoa wito kwa Umoja wa Ulaya na Umoja wa Kujihami wa Ulaya, NATO, na Kundi la G7 kuchukua hatua mara moja na kwa umuhimu kuongeza shinikizo kwa Russia, ikiwemo kuiwekea vikwazo vipya vikali, na kwa umuhimu kuongeza misaada yao ya kijeshi kwa Ukraine, ikiwemo kutupatia vifaru, ndege za kivita, magari ya ulinzi, makombora ya masafa marefu, vifaa vya kutungulia ndege na makombora ya ulinzi.”

Ombi hilo limetolewa wakati maafisa waliowekwa na Russia huko Luhansk na Kherson walimuomba Rais wa Russia Vladimir Putin siku ya Jumatano kuyakalia maeneo hayo kwa minajili ya kile walichosema ni uungwaji mkono wa wakazi.

Maafisa waliowekwa na Russia wamesema asilimia 93 za kura zilizopigwa katika siku tano za kupiga kura ya maoni huko Zaporizhzhia waliunga mkono kujiunga na Russia, pamoja na asilimia 87 huko Kherson, asilimia 98 Luhansk na asilimia 99 huko Donetsk. Zote kwa pamoja mikoa hiyo ni asilimia 15 ya taifa lote la Ukraine.

Ukraine, Marekani na nchi nyingine za Magharibi zimelaani kura hiyo ya maoni zikisema ni kinyume cha sheria. Haielekei kama kuna uwezekano mkubwa wa kutambuliwa kimataifa.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy aliliambia Baraza la Usalama la UN Jumanne kuwa Russia lazima itengewe kimataifa kwa ukusanyaji holela wa maoni katika nchi yake.

“Kuna njia moja tu ya kuzuia haya,” alisema kwa njia ya video. “Kwanza, ni Russia kutengwa kikamilifu ikiwa ni majibu kwa kila inachokifanya.”

Lazima vikwazo zaidi viwekwe dhidi ya Moscow, alisema, na kuwa inyang’anywe kura yake ya turufu kwenye Baraza la Usalama la UN na kuondolewa katika taasisi zote za kimataifa.

“Ushikiliaji huo wa ardhi zilizovamiwa… ni ukiukaji mkubwa wa kikatili wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa,” rais wa Ukraine alisema.

“Hili ni jaribio la kuiba ardhi ya nchi nyingine. Hili ni jaribio la kufuta viwango vya sheria za kimataifa.”

Iwapo Moscow itazishikilia ardhi hizi, Zelensky alisema, “itamaanisha kuwa hakuna kitu chochote cha kuzungumzia na rais wa Russia.”

XS
SM
MD
LG