Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 23:39

Putin anatuma wanajeshi 300,000 Ukraine, Ulaya umesema vita vimefikia kiwango cha hatari kubwa


Wanajeshi wa Ukraine baada ya kukomboa mki wa Kupiansk katika eneo la Kharkiv kutoka kwa wanajeshi wa Russia. Sept 23 2022. PICHA: AP
Wanajeshi wa Ukraine baada ya kukomboa mki wa Kupiansk katika eneo la Kharkiv kutoka kwa wanajeshi wa Russia. Sept 23 2022. PICHA: AP

Upigaji kura katika kura ya maoni yenye lengo la kuzitenga sehemu za Ukraine na kuzifanya kuwa sehemu ya Russia umeingia siku ya nne. Wanajeshi wa Russia katika mikoa ya Luhansk na Donetsk, mashariki mwa Ukraine na Zaporizhzhia na Kherson upande wa kusini zinazoshikiliwa na Russia.

Upigaji kura huo umetajwa kuwa uchaguzi wa ‘kihuni’ ambao matokeo yake ni lazima yaonyeshe kwamba wakaazi wa sehemu hizo wanataka kujiunga na Russia.

Uongozi wa Kremlin, wa Vladmir Putin, unapanga kutumia matokeo ya kura hiyo ya kihuni, na inayoongozwa na wanajeshi wa Russia, kutangaza kwamba unapigana ili kulinda maslahi ya Russia na kuwalinda watu wa sehemu hizo dhidi ya uchokozi wa Ukraine.

Uchaguzi utamalizika kesho jumanne. Wanajeshi wanatembea nyumba hadi nyumba hadi wakiwataka watu kupiga kura.

Uturuki, ambayo ni mshirika wa muda mrefu wa Russia, imesema kwamba haitatambua matokeo ya kura hiyo. Uturuki inakuwa nchi ya hivi karibuni kuongeza sauti yake kwa msimamo wa mataifa mengine yenye nguvu duniani ambayo yamekemea hatua ya Russia kutaka kujichukulia sehemu za Ukraine.

Msemaji wa rais wa Uturuki Ibrahim Kalin amesema kwamba Uturuki inatambua uhuru wa mipaka ya Ukraine na kwamba hawatambui hata hatua ya Russia ya mwaka 2014, kujichukulia sehemu ya Crimea. Kalin amesema kwamba Uturuki inaiunga mkono Ukraine.

“Kinachoonekana ni kwamba kubadilika kwa malengo ya Russia kumeifanya Russia kufikiria tena. Lengo lao la kuingia Ukraine lilikuwa ni kuubadilisha utawala ama uongozi wa nchi hiyo lakini baada ya kupata pingamizi nyingi za kivita, Russia imelazimika wabadili malengo yao na sasa wanataka kuchukua baadhi ya sehemu zinazokaliwa na watu wenye asili ya Russia nchini Ukraine.” Amesema Amin Mwidau, msomi wa diplomasia na uhusiano wa kimataifa akiwa Canada.

Putin anapeleka wanajeshi 300,000 zaidi kupigana Ukraine

Jumatano wiki iliyopita, Rais wa Russia Vladmir Putin alilihutubia taifa hilo na kutangaza kwamba anatuma wanajeshi wa akiba 300,000 kupigana nchini Ukraine. Putin pia alisema kwamba nchi yake itatumia kila aina ya silaha kulinda mipaka ya Russia.

Putin alisema kwamba hana wasiwasi wowote na kwamba atatumia kila mbinu inayowezekana kwa Russia kujilinda. Matamshi ya Putin yalipelekea viongozi wa dunia na wachambuzi kusema kwamba Putin anafikiria kutumia silaha za nyuklia katika vita vya Ukraine, baada ya kudhihirika kwamba amezidiwa katika vita alivyovianzisha.

Marekani imesema kwamba itajibu kwa uzito unaostahili endapo Russia itatumia silaha za nyuklia. Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani Jake Sullivan, amesema kwamba endapo Russia itatumia silaha hizo, itakumbana na athari ambazo haijawahi kuziona na zenye uharibifu mkubwa. Amesisitiza kwamba Marekani itajibu vipasavyo.

Mapigano makali yametokea Ukraine katika saa 24 Jumatatu

Zaidi ya miji 40 ya Ukraine imepigwa na mizinga ya Russia katika muda wa saa 24 zilizopita.

Jeshi la Ukraine limesema kwamba Russia imevurumisha mizinga 5, mabomu ya angani 12 na zaidi ya mashambulizi ya roketi 83.

Makaazi zaidi ya 40 yameathirika hasa katika sehemu za kusini na kusini mashariki mwa Ukraine.

Ndege mbili za kivita za Russia zisizo kuwa na rubani zimepigwa na jeshi la Ukraine na kuanguka katika eneo la Odesa. Hakuna ripoti za vifo zimeripotiwa.

Jeshi la Ukraine limejibu mashambulizi ya Russia kwa kuvurumisha makombora 33, na kupiga sehemu 25 ambapo wanajeshi wa Russia walikuwepo.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ukraine imesema kwamba hospitali katika mji wa Donetsk imeharibiwa vibaya baada ya kupigwa na roketi ya Russia.

Maafisa wamesema kwamba sehemu ya viwanda mashariki mwa Ukraine imeshambuliwa na makombora 26 ya Russia katika muda wa saa 24 zilizopita. Kuna ripoti za vifo na majeruhi lakini hakuna idadi kamili imetolewa hadi wakati tunaandaa kipindi hiki.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ukraine vile vile imesema kwamba roketi mbili za Russia zimepiga mji wa Kramatork, ulioko Donetsk.

Hospitali, nyumba moja binafsi na ghorofa yenye makazi ya watu kadhaa vimeharibiwa kutokana na mashambulizi hayo. Wizara hiyo imeonyesha picha za uharibifu huo.

Russia imeahidi kuwalinda watu katika sehemu uchaguzi unafanyika

Russia imeahidi kwamba itatoa ulinzi wa kutosha kwa watu wa Ukraine katika maeneo manne ambayo kura ya maoni kuhusu kujitenga inaendelea.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov alihutubia Umoja wa Mataifa siku ya Jumamosi na kujaribu kutetea msimamo na vita vya Russia nchini Ukraine.

Lavrov aliendelea kutetea madai ya Moscow kwamba serikali iliyochaguliwa nchini Ukraine iliingia madarakani kwa njia za kihuni na kwamba imejaa watu wenye misimamo mikali ya ubaguzi.

Mamilioni ya raia wa Ukraine wamekimbia makwao tangu Russia ilipoivamia nchi hiyo wakati vita vilipoanza mwezi Febrauri mwaka huu.

Raia wa Russia ambao wamefikisha umri wa kushiriki katika vita, wametumiwa barua na karatasi kutakiwa kujiunga katika jeshi kwa lazima kwa ajili ya kwenda kupigana nchini Ukraine.

Kuna pingamizi kubwa kwa hili. Baadhi ya raia wa Russia wanapinga hilo wakisema kwamba sheria inasema wanaweza kushiriki vita tu iwapo wamechokozwa kivita ndani ya nchi yao, lakini sasa wanaambiwa kwenda kuingia nchi nyingine kivita.

Foleni ndefu za raia wa Russia zimeonekana mipakani wakikimbia nchi yao. Hawataki kwenda Ukraine kupigana. Wanakimbilia Finland na Georgia. Maelfu ya raia wa Russia wamekimbia tangu rais Vladimir Putin alipotangaza kwamba atatuma wanajeshi 300,000 nchini Ukraine.

Viongozi wa Russia wamependekeza kwamba mipaka ya nchi hiyo ifungwe ili kuwazuia raia wake kuikimbia nchi hiyo na kuwalazimu kujiunga na jeshi.

“Hii ni dalili ya kuwepo udhaifu katika jeshi la Russia kwenye vita hivi walivyoanzisha. Waliona vita hivyo vitakuwa rahisi na vyepesi lakini wamepata kipigo ambacho kimewabadilisha maoni na kuwatia hofu,” amesema Amin Mwidau.

Raia wa Russia wameendelea kuonyesha hasira wakipinga tangazo la kutakiwa kwenda kupigana Ukraine

Mtu mmoja amejichoma moto katika kituo cha basi mjini Ryazan, wenye jumla ya wakazi nusu milioni, magharibi mwa Russia. Inaripotiwa kwamba amejichoma moto baada ya kupokea barua ya kumtaka kujiunga na jeshi kupigana Ukraine.

Akaunti ya telegram ya shirika moja la habari la Russia imeonyesha video ya mwanamme huyo akiwa amevalishwa mfuko wa plastiki baada ya moto kuzimwa. Akaunti hiyo imesema kwamba mwanamme huyo alipaaza sauti kwamba hataki kushiriki katika vita hivyo.

Zaidi ya watu 2,000 wanaripotiwa kukamatwa kote nchini Russia baada ya kupinga hatua ya kuwataka kujiunga na jeshi na kwenda kupigana Ukraine.

Raia wa Russia 17,000 wamevuka mpaka na kuingia Finland Jumamosi na Jumapili.

Serikali imeongeza marudufu bei ya tiketi ya ndege kuondoka Russia.

Mashambulizi dhidi ya vituo vya kusajili raia wa Russia kujiunga katika jeshi pia yameripotiwa. Jengo ambalo usajili unaendelea katika mji wa Uryupinsk limepigwa kwa mabomu ya moto mapema Jumatatu. Mtu mmoja amekamatwa. Hakuna kifo wala majeruhi vimeripotiwa.

Maandamano na visa vya uhalifu kama shule kushambuliwa kwa risasi vimeripotiwa nchini Russia.

Ukraine imeitaja hatua ya Putin kutuma wanajeshi zaidi kuwa ishara ya kushindwa mkakati

Nchini Ukraine, rais Volodymr Zelenskyy amesema kwamba hatua ya Putin kuamuru kutumwa wanajeshi 300,000 zaidi, ni ishara kwamba jeshi la Russia limeshindwa.

Zelenskyy amesema kwamba “Russia haikutarajia kwamba jeshi la Ukraine litakuwa na nguvu kupigana.”

Ukraine inaamini kwamba Russia inapanga kuharibu mfumo wa umeme wa Ukraine na kwamba hali inaweza kuwa mbaya sana wakati wa baridi.

Makaburi 440 yamegunduliwa katika sehemu zilizokuwa zikishikiliwa na wanajeshi wa Russia, katika mji wa Izyum, mkoa wa Kharkiv. Kuna ripoti kwamba huenda makaburi kadhaa yatagundulika.

Alasiri ya leo, saa za Ukraine, naibu wa waziri mkuu wa Ukraine Iryna Vereshchuk amedai kwamba wanajeshi wa Russia wamewakamata raia pamoja na wanajeshi katika vita hivyo. VOA haijathibitisha madai hayo.

Kyiv and Moscow zimebadilishana wafungwa mara kadhaa tangu mwezi Februari, vita vilipoanza. Russia iliwaachilia huru wafungwa 215, raia wa Ukraine, siku tano zilizopita.

Kuna ripoti kwamba Russia inawazuia wafungwa 2,500, raia wa Ukraine.

Ukraine imedai kwamba Russia imekataa kuwarudisha raia wake wanaozuiliwa Russia katika hatua ya kubadilishana wafungwa.

Mkuu wa ofisi ya rais wa Ukraine Andriy Yermak, amesema kwamba Ukraine imebadilishana wafungwa na Victor Medvedchuk, ambaye ni rafiki mkubwa sana wa rais Vladmir Putin, na anaishi uhamishoni kwa sasa.

Mwanamme afyatua risasi katika kituo cha kusajili wanajeshi Russia

Nchini Russia, mwanamme mwenye umri wa miaka 25 amekamatwa hii leo baada ya kuingia katika ofisi ya kuwasajili wanajeshi na kuyatua risasi katika eneo la Irkutsk, katika mji wa Ust-ilimsk.

Video kwenye mitandao ya kijamii inaonyesha mwanamme huyo akijitambulisha kwa polisi kama Ruslan Zinin.

Alipigwa risasi na kujeruhiwa. Gavana wa eneo hilo Igor Kobzev ameandika ujumbe wa telegram kwamba mwanamme huyo yupo katika hali mahtuti hospitalini.

Aliingia katika ofisi hiyo, kufyatua risasi na kusema kwamba “hakuna mtu atakwenda Ukraine kupigana’ na kwamba kila mtu aliyekuwa akisajiliwa kwenye ofisi hiyo alikuwa “huru kurudi nyumbani.”

Maandamano yameripotiwa katika miji ya maeneo ya Dagestan na Yakutia kupinga hatua ya serikali ya Putin kutaka kutuma wanajeshi zaidi nchini Ukraine.

Baadhi ya raia wa Russia waliosajiliwa kwenda vitani wameanza kuondoka nchini humo wakiwa wamepanda mabasi. Wameondoka Bolsherechye, eneo la Omsk. Wizara ya Ulinzi ya Uingereza imeandika ujumbe wa Twitter kwamba wengi wao wameanza kuwasili katika kambi za kijeshi. Picha zimeonyesha watu wakiwaaga wana familia huku vilio vikitanda hewani na machozi kububujikwa.

Putin amekutana na rais wa Belarus ambaye ni rafiki mshirika wake mkubwa katika vita vya Ukraine

Hayo yakijiri, rais wa Russia Vladmir Putin anakutana na mwenzake wa Belarus Alexander Lukashenko mjini Moscow.

Russia na Belarus ni washirika wakubwa. Russia imekuwa ikitumia kambi za kijeshi za Belarus kupanga mashambulizi ndani ya Ukraine

Umoja wa Ulaya umeonya kwamba vita vya Ukraine vimeingia katika hatua hatari sana kwa sababu jeshi la Russia linaonekana kuzidiwa.

Mkuu wa sera za mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya Josep Borell amesema kwamba kuna wasiwasi mkubwa kwamba Putin anaweza kutekeleza tishio lake la kutumia silaha za nyuklia

Marekani imeionya Russia

Nchini Marekani, waziri wa Mambo ya Nje Antony Blinken amesema kwamba Marekani ina mpango maalum na mpana endapo Putin atafanya jambo ambalo haliwezi kufikiriwa.

Wiki iliyopita, rais Joe Biden, bila kutoa ufafanuzi, alisema kwamba Marekani itajibu kwa hatua zenye athari zake.

Silaha za nyuklia hazijawahi kutumika tangu mwaka 1945, mabomu mawili ya atomiki yalipoangushwa Japan. Athari zake zilikuwa kubwa.

XS
SM
MD
LG