Timu ya Serikali ya Ukraine ya Kukabiliana na Dharura ya Kompyuta (CERT-UA) ilichapisha mapendekezo mapya Alhamisi, ikionya kwamba wataalam wake wametambua udhaifu wa programu, ambao unaweza kuruhusu wahusika wa mtandao wa Russia kuingia ndani kabisa ya mtandao wa kompyuta na kufanya udukuzi.
Ushauri huo ulitahadharisha kwamba udhaifu huo unaweza kuipatia Russia uwezo wa kuanza mfululizo mpya wa mashambulizi ya mtandaoni, yakilenga Ukraine, yenye nia ya kulemaza mifumo ya mawasiliano na habari.
Mapema wiki hii, shirika la kijasusi la kijeshi la Ukraine lilionya rasmi kwamba Moscow inapanga kuanzisha mashambulizi ya mtandaoni yenye lengo la pamoja na mashambulizi ya makombora, kudumaza sekta ya nishati ya Ukraine.
Kauli ya Jumatatu ilifuatia onyo kadhaa zilizotolewa na maafisa wakuu wa kuratibu mitandao ya Ukraine mapema mwezi huu kwamba Russia ilikuwa inalenga kutumia mashambulizi ya mtandaoni kulenga miundombinu muhimu, na sekta za nishati na fedha za Ukraine.