Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Novemba 06, 2024 Local time: 05:55

Kirusi corona chaenea nchi mbalimbali duniani


Watu mitaani wamejifunika uso kujikinga na kirusi corona katikati ya mji wa Wuhan, China, Jumatano, Jan. 22, 2020.
Watu mitaani wamejifunika uso kujikinga na kirusi corona katikati ya mji wa Wuhan, China, Jumatano, Jan. 22, 2020.

Kirusi corona kimezuia sherehe za mwaka mpya unaotumia hisabu ya kalenda ya mwezi kufanyika ambazo huhudhuriwa na mamilioni ya watu wa China.

Kamisheni ya Afya ya Taifa ya China inasema idadi ya waliokufa kutokana na kirusi hicho kipya imefikia watu 41, na zaidi ya maambukizo 1200 yamerikodiwa katika majimbo 29 nchi nzima.

Wafanyakazi wa afya 15 ni kati ya wale walioambukizwa. Daktari mmoja amefariki kutokana na ugonjwa huo.

Mamia ya wafanyakazi wa afya wamepelekwa katika mji wa Wuhan, ambapo ndiko chanzo cha mlipuko wa ugonjwa huo, ambapo kirusi hicho kilijitokeza mwishoni mwa mwaka 2019.

Wuhan, kama ilivyo miji mingine 16 ya China, imetengwa katika juhudi ya kuzuia maambukizo ya kirusi corona.

Serikali ya mitaa katika mji ulioathirika na kirusi imesema Jumamosi, “Magari yatazuiliwa kuingia katikati ya maeneo ya mjini.”

Maeneo ya Forbidden City na Shanghai Disneyland katika mji wa Beijing yamefungwa kabisa.

Eneo maarufu la utalii la Sanya city katika jimbo la Hainan limefunga maeneo yote ya utalii ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa virusi hivyo..

Hong Kong imetangaza hali ya dharura, imesitisha sherehe zote za mwaka mpya unaofuata hisabu ya kalenda ya mwezi na kufunga mashule.

Kirusi hicho kinaendelea kuenea katika pande mbalimbali za dunia.

Watu watano wameripotiwa kuwa na ugonjwa huo nchini Thailand.

Australia imeripoti kuwa na wagonjwa wanne.

Ufaransa, Japan, Malaysia, na Taiwan, kila nchi kati ya hizi imeripoti kuwa na wagonjwa watatu

Pia Marekani na Vietnam imethibitisha kuwa na wagonjwa wawili.

XS
SM
MD
LG