Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 04:15

Ebola yauwa 27 katika siku moja DRC


Rais wa DRC Felix Tshisekedi akitembelea kituo cha kutibu wagonjwa wa Ebola mjini Beni, Kivu Kaskazini, April 16, 2019.
Rais wa DRC Felix Tshisekedi akitembelea kituo cha kutibu wagonjwa wa Ebola mjini Beni, Kivu Kaskazini, April 16, 2019.

Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo imesema watu 27 walifariki kutokana na maambukizi ya Ebola katika jimbo la Kivu Kaskazini Jumapili, ikiwa ni idadi kubwa kuliko zote katika siku moja, na kufanya idadi ya vifo vya maambukizi ndani ya kipindi cha wiki moja kufikia 126.

Kabla ya vifo vya watu hao 27 Jumapili, idadi ya maambukizi ilikuwa watu 110, wiki chache zilizopita na wizara ya afya inasema kwamba mlipuko wa wiki iliyopita mashariki mwa nchi, katika mikoa ya kivu na Ituri, unasambaa kwa kasi kutokana na mashambulizi ya makundi ya waasi yanayotatiza juhudi za madaktari na msaada wa jumuiya ya kimataifa.

Mnusurika wa Jeanine Masika Mbuka Furana Katungu amemshikilia mtoto anyepata maambuziki ya ugonjwa huo, Kivu Kaskazini, DRC
Mnusurika wa Jeanine Masika Mbuka Furana Katungu amemshikilia mtoto anyepata maambuziki ya ugonjwa huo, Kivu Kaskazini, DRC

Katika mahojiano ya simu Dr Jean Christopher Shako, msimamizi wa juhudi za kukabiliana na Ebola mjini Butembo, ameambia Sauti ya Amerika kwamba japo maafisa wake wamejitolea kuangamiza ugonjwa huo, msaada wa jamii wanaotumikia ni mdogo sana, na wengi hawaamini kwamba kuna Ebola. Anasema kwamba wanafanya kazi kwa matumaini tu.

“Tunapambana na ugonjwa huo kwa uwezo wetu wote. Tuna matumaini kwamba utamalizika. Sote tuwe na imani kwa mungu, tumwombe Mungu tushinde ugonjwa huu”, amesema DR. Shako

Mashambulizi dhidi ya vituo vya matibabu

Vituo vitano vya kutibu wagonjwa wa Ebola vimeshambuliwa katika muda wa miezi miwili iliyopita, huku afisa wa ngazi ya juu wa shirika la afya duniani WHO akiuawa kwa kupigwa risasi na watu wenye silaha, siku 10 zilizopita.

Waliofanya mauaji hayo wanadaiwa kujulikana lakini wanaripotiwa kupewa kinga na makundi ya wapiganaji na watu kutoka katika jamii, wanaopinga juhudi zinazochukuliwa kukabiliana na ugonjwa huo.

Wakaazi wa Butembo kama Issa Misango, wanataka serikali kuonyesha nia ya dhati katika vita dhidi ya ebola.

“Huyo daktari aliuwawa na watu gani, wakati kikao alichokuwa anahudhuria kilikuwa kinajulikana na serikali? Vyombo vya usalama vilijua kwamba kikao hicho kilikuwa kinafanyika. Walikuwa wapi? Watu wanajiuliza maswali mengi wakitaka kujua waliomua daktari huyo. Kama ni wapiganaji wa mai mai au ni wale wale walinzi wa jeshi. Watuambie. Inakuaje walijua hadi mahali alikuwa amekaa wakati wa mkutano, wakaingia moja kwa moja na kumuua?” ameuliza Issa Misango, mkaazi wa Butembo.

Juhudi za uhamasishaji

Idadi kubwa ya watu katika maeneo yenye Ebola, wana imani kwamba Ebola ni fikra tu iliyoanzishwa na kuenezwa na serikali pamoja na jumuiya ya kimataifa.

“Tumejitwika majukumu kama watu wa kawaida katika jamii, kushirikiana na waandishi wa habari kueneza ujumbe jinsi ya watu kujikinga na maambukizi ya Ebola. Tunaeneza ujumbe kupitia vyombo vya habari lakini vyombo hivi vinataka kulipwa ili kupasha ujumbe wa afya. Imebidi tujitoe na kutembelea watu katika makao yao ili kuwaelimisha jinsi ya kuzingatia kanuni za afya, tuweze kuangamiza ugonjwa wa ebola”, ameeleza Issa Misango.

Vifo kutokana na Ebola

Mlipuko wa sasa wa virusi vya Ebola, vinavyosababisha mgonjwa hutapika, kuhara na kutokwa damu, ndio wa pili kwa ukubwa baada ya wa mwaka kati ya 2013 na 2016 uliotokea Afrika magharibi na kuuwa watu 11,000.

Ugonjwa wa ebola unaaminika kuua watu 891 na kuambukiza zaidi ya 500 katika mikoa ya Kivu kaskazini na Ituri nchini DRC.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, Sauti ya Amerika, Washington DC

XS
SM
MD
LG