Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Novemba 22, 2024 Local time: 20:30

Je, January Makamba ni tishio kwa Rais Magufuli?


Rais Magufuli na Januari Makamba wakati wa kampeni za uchaguzi wa rais September 2015.
Rais Magufuli na Januari Makamba wakati wa kampeni za uchaguzi wa rais September 2015.

Kile kilichoanza kama barua iliyochapishwa na makatibu wawili wa zamani wa Chama cha Mapinduzi, CCM, nchini Tanzania, wakijitetea dhidi ya madai kuwa wanajaribu kumzuia Rais John Magufuli kugombea nafasi ya urais mwaka 2020, kimepelekea kufukuzwa uwaziri January Makamba.

Makamba, 45, mtoto wa mmoja wa waandishi wa barua hiyo - Yusuf Makamba alikuwa waziri wa mazingira mpaka Julai 20, alipofukuzwa kazi kwa madai ya utekelezaji mbovu wa kazi yake.

Kwa mujibu wa gazeti la The East African nchini Kenya, wafuasi wake mwanasiasa huyu wanaeleza kuwa Makamba ni mtu mahiri ambaye alisaidia kubuni mbinu mpya za kuendesha kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Amesifika kwa kuweza kuwa mstari wa mbele katika kumsaidia Rais Magufuli kumshinda mpinzani wake katika uchaguzi wa urais 2015, ambaye sasa amerudi kuwa mshirika wake, waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

Hata hivyo mahasimu wake wanamtazama kama mwanasiasa mwenye uchu wa madaraka ambaye yuko nyuma ya kikundi ndani ya CCM kinachotaka kumzuia rais kugombea kipindi cha pili cha urais.

Wengine wadai alihusika katika kuandika barua ya malalamiko kwa Baraza la Wazee la CCM. Mwandishi mwenza alikuwa Abdulrahman Kinana.

Makatibu hao wastaafu waliwasilisha barua yao kwa katibu wa Wazee, Pius Msekwa, ambaye aliipeleka kwa sekretarieti ya chama.

Waziri wa zamani wa habari Nape Nnauye, Makamba na baba yake, na Kinana wanatuhumiwa kuchochea uasi dhidi ya mwenyekiti wa chama. Baadhi ya kada katika chama wanataka wote hawa waliohusishwa na madai ya uchochezi kufukuzwa CCM.

Mbunge wa jimbo la Mtera, Livingston Lusinde, anasema CCM lazima itoe ripoti ya ufuatiliaji wa rasimali za maafisa wanaotuhumiwa kwa ubadhirifu wa mali za chama, akisema baadhi ya viongozi hao wa zamani walihusishwa na ubadhirifu huo na kutolewa kwa waraka huo kutawanyamazisha.

Katibu Mkuu wa CCM aliyeko madarakani Bashiru Ally, wiki iliyopita Jumatatu aliwahakikishia wanachama kuwa hakuna mpasuko ndani ya chama na kuonya kuwa chama hakitawavumilia wale wote wanaotaka kunufaika kisiasa kutokana na migongano ya ndani ya chama.

“Tutamfukuza mtu yoyote kutoka katika chama kwa sababu tunazo taratibu, sheria, katiba na utamaduni wetu. Ninawaonya makada wote kuacha kutumia upumbavu huu unaoendelea kutaka kushinda katika kinyang’anyiro cha serikali za mitaa,” katibu mkuu huyo alieleza mjini Dodoma wakati akizindua biashara za CCM.

CCM ni mara chache kuwafukuza wanachama wake, lakini Machi 2017 iliwafukuza makada 12, akiwemo waziri Sophia Simba, baada ya kutuhumiwa kumuunga mkono Lowassa katika uchaguzi mkuu mwaka 2015.

Duru za siasa zinasema kuwa Makamba alikuwa anatarajiwa kumrithi Rais Magufuli. Kampeni yake ya hivi karibuni kupiga marufuku mifuko ya plastiki, ambayo ilipongezwa na wengi kwa kuwa na mafanikio kutokana na juhudi zake za kuuelimisha umma, ilionekana kama ni jaribio la kupata kuungwa mkono kisiasa.

Alikuwa ni mmoja wa watu watano walioteuliwa kwa tiketi ya CCM katika kumpata mgombea wa uchaguzi 2015. Lakini hivi sasa ametuhumiwa kwa hujuma ya kumpinga rais kugombea 2020.

Wateule wengine kati ya hao kugombea urais 2015 ndani ya CCM walikuwa Bernard Membe na Rais Magufuli ambaye alishinda na kuwa mgombea wa chama.

XS
SM
MD
LG